Showing posts with label SIASA. Show all posts
Showing posts with label SIASA. Show all posts

RIDHIWANI KIKWETE ARUDISHA FOMU ZA UBUNGE CHALINZE


MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Ridhiwani Kikwete leo amerudisha fomu ya kugombea ubunge wa jimbo la Chalinze kupitia tiketi ya chama cha Mapinduzi, akisindikizwa na washindani wake katika kura za maoni, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Ramadhan Maneno pamoja na Imani Madega. 
 Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Ridhiwani Kikwete akiwa ameambatana na  washindani wake katika kura za maoni, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Ramadhan Maneno pamoja na Imani Madega wakifurahia jambo. 
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Ridhiwani Kikwete akiwa ameambatana na  washindani wake katika kura za maoni, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Ramadhan Maneno pamoja na Imani Madega na wadau wengine akielekea kurejesha fomu.
 Baadhi ya Wanahabari wakishuhudia tukio la Urudishwaji fomu wa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi mapema leo.

===========  ======== ======
Ridhiwani Kikwete  arudisha fomu za Ubunge Chalinze.

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Ridhiwani Kikwete leo amerudisha fomu ya kugombea ubunge wa jimbo la Chalinze kupitia tiketi ya chama cha Mapinduzi.

Akisindikizwa na washindani wake katika kura za maoni, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Ramadhan Maneno pamoja na Imani Madega, Ridhiwani aliwashukuru wana CCM na wakazi wa Chalinze kwa ujumla kwa kumuunga mkono.

Ridhiwani pia ameahidi kushirikiana na wanachalinze katika kutekeleza yote yaliyofanywa na wabunge waliotangulia lakini pia amewataka wakazi wa Chalinze kupuuza hoja inayotolewa na mgombe wa Chadema inayodhihaki kuwa yeye sio mkazi wa Chalinze. Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chadema Matayo Torongey alinukuliwa akisema kuwa Ridhwani hawezi kugombea Ubunge Chalinze kwa kuwa sio mkazi wa Jimbo hilo.

Aliongeza kuwa ili kuwahakikishia wakazi wa Chalinze maendeleo inatakiwa kwa wagombea kutangaza sera zinazotekelezeka na kuacha kutoa kauli zenye nia ya kuwapumbaza wakazi wa Chalinze.

Alisema kuwa hatotaka kutumia muda wake kufanya kampeni za kiubabaishaji kuanza kurumbana na kukejeli kwa kuwa amekuwa katika misingi mizuri ya kisiasa. Alisema hajatokea chumbani kugombania Ubunge badala yake amekuwa katika misingi ya kisiasa tangia mdogo na amechukua uamuzi wa kuingia katika siasa kwa lengo la kusaidia wananchi.

Alisema kuwa kero kubwa inayowakabili wakazi wa Chalinze ni kukosekana kwa maji ya uhakika, kero ambayo kwa sasa inatatuliwa kwa kuanzishwa kwa mradi wa maji ya uhakika. Aliongeza kuwa pia kuna tatizo kubwa la ukosefu wa huduma bora za afya uhakika za afya kwa wakazi wa eneo la Chalinze. "Najua awali wakazi wa eneo la Chalinze walikuwa wachache sana na kwa sasa kuna ongezeko kubwa la wakazi wa Chalinze hivyo hata mahitaji nayo yanaongezeka"alisema Ridhwani.

Aliongeza kuwa ongezeko hilo limepelekea kuongezeka kwa uhitaji wa huduma mbalimbali kama hizo za za kijamii na kuongeza kuwa akiwa Mbunge atatatua kero hizo."Watu wanadhania kuwa mimi nimetokea chumbani kuja kwenye siasa hapana yani tena hata sio kwa sababu ya kuwa mimi ni mtoto wa Rais ndio nimeona ngoja nije kuuza sura huku sio, ila ni kwa sababu nimekulia katika mazingira haya na ninaona kuwa ni wakati wa kutatua kero za wakazi wenzangu wa huku"alisema Ridhiwani.

Kuhusiana na tatizo la migogoro katika jimbo hilo alisema kuwa anaona kuwa analo jukumu kubwa la kuendelea kushiriki katika kutatua kero zao ambazo CCM kwa muda mrefu imekuwa ikifanya hivyo. Alisema kuwa atakuwa na haki ya kupata mikosi iwapo akipuuzia kutatua kero ya muda mrefu ya wafugaji na wakulima.

Ridhwani anatarajia kuzindua rasmi kampeni yake Jumamosi ijayo katika jimbo la Chalinze. Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze unafanyika kufuatia kifo cha aliekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Said Bwamdogo.

Soma Habari Kamili

TAARIFA YA PINGAMIZI DHIDI YA MGOMBEA WA CHADEMA KWENYE UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA CHALINZE


Mimi FABIAN L. SKAUKI, mgombea ubunge wa uchaguzi mdogo jimbo la CHALINZE kwa Ticket ya THE CIVIC UNITED FRONT (CUF) ninamwekea Pingamizi mgombea wa chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba amepoteza sifa za kuwa mgombea kwa sababu zifuatazo.

Ndugu MATHAYO. M. TORONGEY amejaza Taarifa za uongo kwenye Fomu yake kwamba kazi anayoifanya ni BIASHARA. Sio kweli, kwa sababu hajaweka vielelezo vya yeye kufanya hiyo kazi. Hajulikani anafanya kazi gani.

Ndugu MATHAYO .M. TORONGEY amejaza katika fomu kwamba anajua kusoma na kuandika  Kiswahili na kiingereza. Taarifa hizi ni za uongo, mgombea huyu hajui kusoma wala kuandika Kiswahili wala kiingereza, na kwamba amedanganya na amepoteza sifa za kuwa mgombea.

Ndugu MATHAYO .M.TORONGEY amedanganya kwa kughushi/kufoji sahihi za wadhamini,ambao amewaorodhesha kwenye fomu ya kuomba kuthibitishwa kuwa mgombea. Ambapo katika fomu hizo wadhamini wote sahihi zao zimefojiwa na hazifanani na zile zilizokuwepo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kwamba sahihi zote hizi zimesainiwa na mtu mmoja ambaye sio muhusika. Hivyo anapoteza sifa ya kuendelea kuwa mgombea.

Ndugu MATHAYO.M.TORONGEY ameshindwa kutimiza mahitaji ya kisheria ya kuwa na wadhamini wasiopungua 25, badala yake amedhaminiwa na wadhamini 28 ambao kati yao wadhamini 7 sio wapiga kura halali wa jimbo la CHALINZE, na kwamba Taarifa zao na namba zilizojazwa hazifanani.

Hivyo anabakiwa na wadhamini halali 21 ambao kisheria hawatoshi kutimiza matakwa ya kisheria.

Majina ya wadhamini hao ambao hawakidhi matakwa ya kisheria na namba zao ni:
 
JINA LA MDHAMINI                                                            NAMBA YA KADI KURA

1.    HABIBU ALLY SAIDI                                                     *16886275*
2.    MOHAMMED RAMADHANI                                       *30376567*
3.    ABDULKADIR ALLY                                                      *49264905*
4.    SHABANI SULEYMAN                                                  *16984045*
5.    JUMA MRISHO                                                            *48759563*
6.    RAJABU ALLY                                                              *16872368*
7.    MANENO MIRAJI                                                        *16872059*

Wananchi wenye namba na majina hayo hapo juu waliojazwa kama wadhamini kuanzia namba 1 hadi 7 kwenye fomu yake hawana sifa za kupiga kura kwenye maeneo ambayo wamejazwa wanatokea.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba idadi halali ya wadhamini wanaobaki ukiwaondoa hao saba watabaki 21, hawakizi vigezo vya kuwa wadhamini.

Ndugu MATHAYO.M.TORONGEY amedanganya Uraia wake, na kwamba yeye si Mtanzania wa kuzaliwa ndio maana hana vielelezo halali vinavyohusu uraia wake. Hivyo anakosa sifa ya kuwa mgombea.

Hivyo ninaomba Tume ya Uchaguzi kutengua uteuzi wa mgombea wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ndugu MATHAYO.M.TORONGEY kwa kuwa anakosa sifa za yeye kuendelea kuwa mgombea.

Wako katika ujenzi wa Taifa

FABIAN LEONARD SKAUKI
……………………………………………………..
MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA CHALINZE.
THE CIVIC UNITED FRONT

Soma Habari Kamili

CCM YAHOJI UWEPO WA HELIKOPTA YA CHADEMA SIKU YA KUPIGA KURA KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA KALENGA


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimehoji matumizi ya helikopta ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), siku ya kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa Kalenga, Jumapili ijayo.
 
Mratibu wa Kampeni za CCM katika jimbo hilo, Miraji Mtaturo, aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kutoa msimamo kuhusu tangazo la Chadema kuwa watatumia helikopta siku ya kupiga kura.
 
“Mwenyekiti, wenzetu Chadema wametangaza kwamba siku ya uchaguzi, wataleta watu zaidi ya 1,000 wakiwemo wabunge wao kulinda kura, lakini pia wamesema watatumia helikopta yao kufanya doria, hiyo haiwezi kuwa doria itakuwa ni kampeni,” alisema.
 
Mtaturo alisema matumizi ya helikopta hiyo ni kinyume na Sheria ya Uchaguzi inayokataza vyama kufanya kampeni siku ya uchaguzi, na pia akataka kujua kama vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka vikundi vyake vya ulinzi karibu na vituo vya kupigia kura.
 
Akijibu hoja hiyo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema ni muhimu kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo vikazingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
 
Jaji Lubuva alisema hayo katika mkutano wa Nec na viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo, uliofanyika jana katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, mjini hapa.
 
Hata hivyo, hakufafanua kama ni makosa au la kutumia helikopta siku ya uchaguzi. Chombo hicho ni cha usafiri kama ilivyo gari, pikipiki au baiskeli, ambavyo havizuiwi na sheria kutumia siku ya kupiga kura
 
Kwa kawaida, hata magari yaliyokuwa yakitumika wakati wa kampeni, siku ya uchaguzi yanaruhusiwa kutumika lakini bila vipeperushi au alama yoyote ya mgombea.
 
Helikopta kisiasa
Hata hivyo, pamoja na kuwa helikopta imekuwa ikitumika kama nyenzo ya usafiri, katika siasa za Tanzania imekuwa ikitumika kama nyenzo ya kukusanya vijana na wasikilizaji katika mikutano ya kampeni.
 
Hilo linadhihirisha na matumizi ya helkopta za kisiasa kupaa kutoka katika kiwanja kimoja kwenda katika kiwanja kingine kilicho umbali usiozidi kilometa moja, kusindikiza maandamano na hata kuvutia watazamaji kwa kusimama angani.
 
Walinzi wa chama
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limeahidi kuwakamata na kuwafungulia mashitaka walinzi wa vyama vya siasa watakaonekana kuzagaa karibu na vituo vya kupigia kura.
 
“Kazi ya Polisi ni pamoja na kuhakikisha amani inakuwepo wakati wa upigaji kura na utangazaji wa matokeo; sitaki kusikia habari ya vikundi vya ulinzi vya CCM Green Guard na Chadema Red Brigade,” alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi.
 
Uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili Machi 16, mwaka huu unahusisha vyama vitatu vya siasa; CCM ambayo imemsimamisha Godfrey Mgimwa, Chadema Grace Tendega na Chausta Richard Minja.
 
Vituo vya kura
Pia Lubuva aliwataka wananchi kuondoka katika vituo vya kupigia kura mara baada ya kupiga kura kwani kazi ya kulinda na kuhesabu kura itafanywa na mawakala wa vyama pamoja na maofisa wa Tume

>>Habari Leo

Soma Habari Kamili

CHADEMA WAMPITISHA RASMI MGOMBEA UBUNGE CHALINZE


Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimempitisha Mathayo Torongey kuwa mgombea rasmi wa ubunge kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze. 
 
Akimtambulisha mgombea huyo kwa Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chadema, John Mrema alisema Torongey alipitishwa juzi na Sekretariati ya chama kwa niaba ya kamati kuu.
 
“Kikao cha Sekretariati kilizingatia maoni na ushauri wa wanachama na viongozi wetu wa ngazi za chini, Hivyo kwa kuwa hakukuwa na kipingamizi chochote juu ya agombea, chama kilimpitisha Torongey” alisema Mrema.
 
Torongey alishinda kura za maoni za chama hicho jimboni Chalinze kwa kupata kura 280 dhidi ya 510 zilizopigwa. Aliwashinda wapinzani wake, Omar Mvambo aliyepata kura 84, Francis Mgasa 61 na Frank Mzoo alijinyakulia kura 23.
 
Mgombea huyo anatarajia kushindana na Fabian Leonard aliyepitishwa na chama cha CUF pamoja na Ridhiwani Kikwete anayesubiriwa kupitishwa na kamati kuu ya CCM (CC-CCM).
 
Mshindi wa uchaguzi huo anatarajia kuziba pengo la aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo aliyefariki Januari 22 mwaka huu.
 
Mrema ambaye pia ameteuliwa kuwa Mkuu wa Operesheni wa Uchaguzi mdogo wa Chalinze, alisema Chadema kina imani kubwa na Torongey kushinda uchaguzi wa jimbo hilo unaotarajia kufanyika Aprili 6.
 
Alisema uchaguzi wa jimbo hilo ni muhimu sana kwa chama kwa kuwa limeshawahi kuongozwa na Rais Jakaya Kikwete kwa miaka 15 bila ya kuwa na maendeleo yoyote.
 
Mrema alisema Chadema hakitishwi na historia ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuwapitisha baadhi ya watoto wa vigogo katika chaguzi ndogo mbalimbali za ubunge zilizowahi kufanyika nchini kama njia ya kuwarithi wazazi wao.
 
Alizitaja chaguzi zile za Arumeru Mashariki ambapo CCM kilimpitisha Sioi Sumari kumrithi baba yake marehemu Jeremia Sumari, Kalenga; Godfery Mgimwa kumrithi William Mgimwa, na hatimaye uchaguzi wa Chalinze ambapo mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani anatarajia kuwania.
 
Naye aliyekuwa mgombea katika kura za maoni katika kinyang’anyiro cha ubunge ndani ya chama hicho, Omari Mvambo alisema aliridhishwa na matokeo na mchakato mzima wa uchaguzi.
 
“Mchakato mzima wa uchaguzi ulienda vizuri na wagombea wote tuliridhika na matokeo yalikuwa sahihi. Kwa hiyo nimeamua kujidhihirisha kuwa ntampa nguvu mgombea aliyepitishwa kushinda uchaguzi,” alibainisha Mvambo.


Mgombea aliyepitishwa na Chadema, Torongey alisema kuwa anatarajia sifa yake ya uenyeji na historia ya maisha yake duni vitakuwa moja ya chachu za kushinda wapinzani wake katika uchaguzi unaotarajiwa kuwa na upinzani mkubwa.
 
Alisema akipata ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo, atahakikisha anatatua changamoto za maji, elimu na pia kushughulikia masuala ya mgogoro baina ya wafugaji na wakulima uliodumu kwa muda mrefu.Mgombea huyo alichukua fomu maalumu ya tume ya uchaguzi Mjini Bagamoyo jana ya kugombea ubunge wa jimbo hilo la Chalinze.

Soma Habari Kamili

CCM YAMPA JESHI LA USHINDI RIDHIWANI KIKWETE


KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemteua, Ridhiwani Kikwete, kuwa mgombea katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, unaotarajiwa kufanyika Aprili 6, mwaka huu.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, uzinduzi wa kampeni za CCM utafanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, Abdulrahaman Kinana na kufungwa na Makamu Mwenyekiti CCM Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
 
Alisema kampeni katika jimbo hilo zitaendeshwa na chama hicho ngazi husika na kuratibiwa na yeye mwenyewe Nnauye.
 
“Aidha kikao hicho cha Kamati Kuu, kilipokea taarifa ya maendeleo ya kampeni zinazoendelea huko Kalenga, huku ikisema imeridhika na mwenendo wa kampeni hizo, ambapo CCM inatarajia kupata ushindi,” alisema.
 
Katika uchaguzi wa kuwania nafasi hiyo ya ubunge Chalinze, Ridhiwani alishinda katika kura ya maoni kwa kupata kura 758, akifuatiwa na Shaban Madega kura 335, Athuman Maneno kura 206 na Changwa Mkwazu aliyepata kura 12.
 
 Ifuatayo chini ni Taarifa Rasmi ya CCM:



Soma Habari Kamili

KALENGA KWACHAFUKA


DEREVA wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, Mohamed Kunambi, ameshambuliwa na kujeruhiwa na watu wanaodhaniwakuwa wafuasi wa chama cha CHADEMA.

Tukio hilo liletokea usiku wa kumkia jana eneo la Ifunda jimbo la Kalenga wilaya ya Iringa Vijijini mkoa wa Iringa.

Mbali na dereva huyo diwani wa kata ya Ifunda, Eliya Mngwila, naye amejeruhiwa na watu hao waliposhambulia gari alilopanda.

Hayo yalielezwa jana na Katibu wa CCM mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya mchakato wa kampeni.

Mtenga alisema tukio hilo lilitokea eneo Ifunda ambapo vijana wa CHADEMA waliokuwa kwenye gari lenye namba za usajili T 156 CDA iliyokuwa na nembo ya M4C inayotumiwa na chama hicho.

Alisema vijana hao wakiwa na silaha mbalimbali yakiwemo mapangawalimkuta dereva huyo pamoja na viongozi wengine wa CCM akiwemo diwani huyo na kuanza kuwashambulia.

Alisema baada ya tukio hilo waliojeruhiwa walipelekwa Makao Makuu ya Polisi mkoa wa Iringa abako waliandika maelezo na kupewa kibali cha kwenda hospitali (PF3).

"Walishambulia magari yetu kwa kuyavunja vioo hivi sasa yako polisi, tunauhakika waliofanya hivi ni wafuasi wa CHADEMA na hayo ni maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa chama hicho," alisema.

Kwa mujibu wa Mtenga, gari la CCM lililoshambuliwa ni lenye namba za usajili T 139 CKS ambalo pia liko Polisi.

Wakati huo huo, CCM imesema CHADEMA imeingiza mkoani humo vijana 120 kwa ajili ya kufanya vurugu ili kuvuruga mchakato wa uchaguzi huo.

Mtenga, alisema taarifa za uhakika walizonazo, zinasema vijana hao wameingia mkoani humo juzi na watasambazwa kwenye kata mbalimbali za jimbo hilo.

"Hivi sasa vijana hao wako Iringa mjini wakijiandaa kutekeleza malengo yao ambapo miongoni mwake ni haya yanayotokea sasa," alisema.

Mtenga alikionya chama hicho na kusema kisithubutu kufanya vurugu hizo kwa lengo la kumwaga damu kwa wananchi wasio na hatia kwani hakitavumiliwa.

"Kazi ya CCM ni kulinda amani, hivyo hatutakuwa tayari kuona damu ya mkazi yeyote wa Kalenga inamwagika," alisema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu madai ya kutekwa Paroko wa Kanisa la Orthodox, Parokia ya Mtakatifu Basil Mkuu , Costantino Mbilinyi, Mtenga alisema ni za uongo.

Akifafanua kuhusu tukio hilo alisema CCM ina watu wenye akili timamu ambao hawawezi kufanya tukio hilo.

Kwa mujibu wa Mtenga, siku ya tukio Paroko huyo aliongozana na vijana saba wa CHADEMA kutoka Arusha kwa ajili ya kufanya vurugu.

Alisema gari alilokuwemo paroko huyo lilikutwa na silaha za jadi yakiwemo mapanga ambazo zinadhaniwa zilikuwa maalumu kwa ajili ya kufanyia uhalifu.

"Mwaka 2010 paroko huyo alikuwa mpambe wa Grace Tendega wakati huo akiwa cha cha Jahazi Asilia ambaye kwa sasa ndiye mgombea ubunge kupitia chama cha CHADEMA," alisema.


>>Gazeti la Mzalendo

Soma Habari Kamili

MSHINDANI WA JK KUPAMBANA NA RIDHIWANI KIKWETE CHALINZE


Aliyekuwa mshindani wa Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi wa Jimbo la Chalinze mwaka 2000 kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (Cuf), Fabian Leonard atapambana na mtoto wa rais huyo, Ridhiwani Kikwete katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo utakaofanyika Aprili 6, mwaka huu. 
 
Chama hicho, kikimtangaza mgombea huyo Makao Makuu ya Cuf yaliyopo Buguruni Dar es Salaam jana, kilisema kinakwenda kulichukua jimbo hilo kutokana na wananchi wake kuendelea kuishi maisha magumu wakati rais wa nchi anatokea jimbo hilo.
 
Uchaguzi huo unafanyika kujaza nafasi iliyobaki wazi baada ya aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo, Said Bwanamdogo kufariki dunia. Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Abdul Kambaya akimtambulisha mgombea huyo alisema, Leonard alipambana na Rais Kikwete mwaka 2000 wakati huo Rais Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nje.
 
“Huyu Leonard ni mzaliwa wa Chalinze anayajua matatizo ya wanachalinze, alipambana na Rais Kikwete lakini kutokana na sababu mbalimbali alishindwa, sasa ni zamu yake kumpambana na mwana,”alisema Kambaya
 
Leonard alisema, jimbo hilo limekuwa nyuma kimaendeleo huku likiwa na kiongozi wa nchi ndani yake, hivyo endapo baba alishindwa hata mtoto naye hataweza. Alisema Mkoa wa Pwani katika matokeo ya kidato cha Nne mwaka jana imekuwa ya tatu kutoka mwisho, huduma za afya duni na barabara hazifai. “Nimejipanga, nilipambana na baba yake sasa kama napambana na mtoto ni dhahiri ushindi upo hadharani”alisema Leonard.

Soma Habari Kamili

CUF YAPINGA WATANZANIA BARA KUMILIKI ARDHI VISIWANI ZANZIBAR


Chama Cha Wananchi(CUF) kimepinga wazo na rai ya kupunguza masharti ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ili kulegeza nguvu zake kisheria na kuwapa fursa Watanzania Bara kumiliki ardhi Visiwani Zanzibar. 
 
Msimamo huo umetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Mwasiliano ya Umma wa CUF Salum Bimani katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana visiwani humo, siku chache baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(Muungano) Samia Suluhu Hassan, kushauri Katiba ya Zanzibar kuangaliwa upya na kuwapa nafasi Watanzania Bara kumiliki ardhi Zanzibar.
 
Bimani alisema kuwa suala la ardhi siyo la Muungano tangu mkataba wa awali wenye orodha ya mambo ya Muungano na siyo sahihi kufanyika marekebisho ili kuwapa nafasi Watanzania Bara kumiliki ardhi Zanzibar kwani ni ndogo na ndiyo sababu hata waasisi wa Muumgano waliamua ardhi hiyo imilikiwe na wazanzibari pekee. 

Soma Habari Kamili

KIONGOZI WA UVCCM AFUNGA TAWI LA CHADEMA LUSHOTO NA KUPANDISHA BENDERA YA CCM


Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kutoka Mkoa wa Tanga Ndugu Husna Mbwambo Sekiboko amefunga tawi la Chadema katika Kijiji Cha Lukozi na kupandisha Bendera ya Chama Cha Mapinduzi kutangaza Ufalme mpya wa Chama hicho cha siasa.

Tukio hilo limetokea jana tarehe 6th March 2014 katika kijiji cha Lukozi, wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga, ambapo sambamba na kuasisi tawi hilo la Chama Cha Mapinduzi pia kiongozi huyo wa UVCCM ameingiza wanachama wapya 206 ambapo wengi wao walikuwa ni wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)

Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la Taifa la UVCCM, alifungua mashina sita yakiwemo ya Manyara, bodaboda, n.k pia alifanya vikao vinne vya ndani ambapo alizungumza na wanaCCM juu ya hali ya Uimara wa Chama na kuhoji kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika Kijiji hicho ndani ya Wilaya ya Lushoto pamoja na kufanya mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na wananchi wengi wa Lukozi.

Pamoja na vikao hivyo lakini pia Husna alitembelea vikundi vya ujasiriamali vya  akinamama pamoja na kambi ya JUDO ya Vijana wilayani Lushoto na kujadili nao Changamoto wanazokutana nao na kushirikiana nao kuzipatia ufumbuzi.

Husna anafanya ziara za kawaida katika Mkoa mzima wa Tanga katika kuhamasisha Vijana kujiunga na Chama Cha Mapinduzi pamoja na Jumuiya ya Umoja wa Vijana.
 Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kutoka Mkoa wa Tanga,Ndugu Husna Mbwambo Sekiboko akikabidhi kadi UVCCM kwa mmoja wa vijana wa kambi ya JUDO ya Vijana wilayani Lushoto.
 Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kutoka Mkoa wa Tanga,Ndugu Husna Mbwambo Sekiboko akipandisha bendera ya CCM kwenye moja ya mashina ya chama hicho.

Soma Habari Kamili

KAMPENI ZA CCM JIMBO LA KALENGA ZAZIDI KUPAMBA MOTO


Mgombea kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mdogo jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, Godfrey Mgimwa (wapili kushoto), Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Bara Mwigulu Nchemba, wakiserebuka na wananchi baada ya kuwasili katika Kijiji ya Kibebe Kata ya Ulanda kwa ajili ya mkutano wa kampeni, jana.
Mgombea kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mdogo jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, Godfrey Mgimwa (kushoto) akiwasalimia wananchi kwa kuwapungia mkono, baada ya kuwasili katika Kijiji ya Kibebe Kata ya Ulanda kwa ajili ya mkutano wa kampeni. pamoja naye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wsa Iringa, Jesca Msambatavangu na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Mwigulu Nchemba.
Wananchi wa Kijiji ya Kibebe Kata ya Ulanda, wakiwa wamembeba kumpeleka kitini mgombea wa CCM jimbo la Kalenga Godfrey Mgimwa, alipowasili kwenye kijiji hicho kufanya mkutano wa hadhara.
Mwenyekiti wa CCM Iringa, Jesca Msambatavangu akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la kalenga, katika Kijiji ya Kibebe Kata ya Ulanda.
Ni shangwe na nderemo kwa wananchi wa kijiji ya Kibebe ya Ulanda katika mapokezi ya mgombea wa CCM alipowasili eneo lao.
Mwana-CCM Maria Geofrey, akiwa ameketi kivulini na mtoto wake, wakati wa mkutano wa kampeni ulipokuwa kifanyika katika Kijiji ya Kibebe Kata ya Ulanda.
Mama akichota maji safi na salama, Kijiji ya Kibebe Kata ya Ulanda, jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, wakati CCM wakiendelea na mkutano wa kampeni katika eneo hili. Kwa mujibu wa wenyeji kisima hicho cha maji kilichimbwa na Mbunge wa zamani wa jimbo la Kalenga, Marehemu Dk. William Mgimwa, ambaye alifariji Januari Mosi, mwaka huu, na kusababisha jimbo kuingia katika uchaguzi mdogo. PICHA ZOTE NA BASHIR NKOROMO.

Soma Habari Kamili

CHADEMA YAANZA MCHAKATO WA KUMTAFUTA MPINZANI WA RIDHIWANI KIKWETE KATIKA JIMBO LA CHALINZE


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza mchakato wa kutafuta mgombea wa kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Chalinze, ambapo jana fomu za kuwania nafasi hiyo kupitia chama hicho zilianza kutolewa.
 
Tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishaanza mchakato wa kutafutia mgombea wa kuwania nafasi hiyo, ambapo Ridhiwani Kikwete, alishinda kura ya maoni ya wanachama wa chama hicho na sasa anasubiri uamuzi ya vikao vya juu vya chama hicho.
 
Akizungumza nasi jana, Ofisa Uhusiano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema fomu hizo zinatolewa na kurejeshwa katika ofisi za Kanda ya Pwani ya chama hicho.
 
“Baada ya kurejesha fomu, walioomba kuwania nafasi hizo watapigiwa kura ya maoni na wanachama wa Chadema wa eneo husika, na baada ya hapo uamuzi wa mwisho utakuwa ni wa vikao vya juu,” alisema Makene.
 
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Uenezi wa Halmashauri ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, alisema bado chama hicho kipo kwenye mchakato wa kuandaa vikao vya juu, vitakavyoyachuja majina ya waliopigiwa kura za maoni na kuteua mgombea wa ubunge kupitia chama hicho.
 
“Tarehe rasmi ya vikao hivi vya juu bado haijapangwa, ndio tuko kwenye mchakato tukikamilisha tutawajulisha,” alisema Nape.
 
Juzi Ridhiwani alishinda kura ya maoni ya kumpata mgombea wa CCM katika jimbo hilo baada ya kupata kura 758, akifuatiwa na Shaban Madega aliyepata kura 335, Athuman Maneno kura 206 na Changwa Mkwazu aliyepata kura 12.
 
Uchaguzi mdogo wa Jimbo hilo la Chalinze, unatarajiwa kufanyika Aprili 6, mwaka huu na Machi 12, vyama vya siasa vitawasilisha majina ya wagombea wake kwa ajili ya kuthibitisha uteuzi wao.
 
Kampeni rasmi za uchaguzi huo zitaanza Machi 13, mwaka huu. Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo kufariki dunia.

Soma Habari Kamili

RIDHIWANI KIKWETE AMEDAI HABEBWI NA BABA YAKE, RAIS JAKAYA KIKWETE

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiv_0O-0Vre3T9RIyUneNRFcosG4tRm5IaX7mgxRPeiNNfsFsMhBf51Kii-MfKhjlpKQepQh2WIaKidnLlQIcjQjdw5tRxHGTnu7SejTD5bDnCHxHuQTvkX7gdY1uVZg-i7lCIy1oRsuYk/s640/RidhiwaniKikwete.jpg

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Bagamoyo, anayetarajiwa kuwania ubunge Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amesema habebwi na baba yake, Rais Jakaya Kikwete, katika harakati zake za kisiasa.

Ridhiwani aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari juzi jioni baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura za maoni katika jimbo hilo kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Msata.

Alisema anafanya siasa bila kupitia mgongo wa baba yake, Rais Kikwete.

“Siasa ninayofanya haina mahusiano na baba yangu, nafanya siasa kwa maisha yangu na sina ubia na baba yangu katika hili,” alisisitiza.

Akijibu swali la kwanini amejiingiza katika siasa tofauti na maneno yake mwaka 2010 kuwa hawezi kushiriki katika kinyang’anyiro cha ubunge kwenye jimbo hilo, Ridhiwani alisema hakuwa tayari kujitangaza kwa kipindi hicho ili kutowapa nafasi maadui kutawala kabla ya wakati.

Aidha, Ridhiwani aliomba mshikamano na ushirikiano kwa wana-CCM kufanikisha azima ya kutetea jimbo hilo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Katika kura za maoni, Ridhiwani alipata kura 758, Imani Madega, kura 335, Maneno kura 206 na mwanamke pekee aliyeshiriki katika mchakato huo, Mkwazu Changwa, alipata kura 17.

Kamati Kuu (CC) ya CCM inatarajia kukutana Machi 8, mwaka huu  kupitisha jina moja litakaloshiriki kumpata mbunge wa Jimbo la Chalinze kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo.
 
CHANZO: NIPASHE

Soma Habari Kamili

SAMSON: CHADEMA NI KIKUNDI CHA WAHUNI NA SI WANASIASA


WAKATI maandalizi yote ya uzinduzi wa chama kipya cha ACT-Tanzania yakiwa yamekamilika, Katibu Mkuu wake Samson Mwigamba, ameiponda CHADEMA kuwa ni kusanyiko la wahuni na si wanasiasa, Hamis Shimye  wa  Gazeti la  Uhuru  anaripoti..

Mwigamba amewatahadharisha Watanzania kutokubali kurubuniwa na kauli kuwa CHADEMA ndio mkombozi wa taifa. Amesema viongozi wa chama hicho asilimia kubwa wapo kwa ajili ya maslahi binafsi.
 
“Watanzania wawangalie na ikibidi wawapuuze, nilikuwepo nafahamu kila kinachoendelea, pale hakuna chama licha ya kujinadi kuwa wakombozi wa wananchi, ni waongo wakubwa. 
“Kuna watu wapo pale kwa ajili ya maslahi binafsi na familia zao, hakuna mtanzania atakayetetewa wala kuletewa maisha bora kama watakiweka madarakani,’’ alisema Mwigamba katika mahojiano na gazeti hili jana.
Alisema CHADEMA inatumia mabavu na kuchochea vurugu kwa kuwa hakuna kiongozi bora mwenye uwezo wa kuwaongoza wananchi zaidi ya kusheheni viongozi wa matukio na si wa kuwazungumzia wananchi.
 
Mwigamba alisema kupitia chama chao, wamejipanga kuleta mabadiliko ya kisiasa hasa kwa vyama vya upinzani nchini, ambapo alisema muda wowote kuanzia leo, wanatarajia kupewa usajili wa kudumu wa chama hicho.
 
Alisema hawajakianzisha chama hicho ili kuhujumu upinzani, bali kukidhi haja ya watanzania.
 
Alikanusha uvumi kuwa wanatumiwa na CCM kuvuruga upinzani nchini. Alisema hayo ni mawazo ya watu wasio na ufahamu mzuri.
“Tulikuwa na mipango ya kwenda mkoani Mwanza kufanya mkutano wa hadhara, tumeshindwa baada ya kukosa fedha, ila tutafika kwa nguvu zetu wenyewe mkoani humo na mikoa mingine nchini,” alisema Mwigamba.
Akizungumzia madai ya chama hicho kufadhiliwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, Mwigamba alisema si za kweli.
 
“Hatufadhiliwi na Zitto na tutasimama kwa nguvu yetu, japokuwa tunamuhitaji na tumeanza naye mazungumzo ili kumuomba ashirikiane nasi katika harakati za kuleta mabadiliko,” alisema Mwigamba.
 
Alisema bado hawajafanikiwa kumshawishi Zitto, licha ya kuwa wamejipanga kuwa na wanasiasa makini wenye mtazamo wa mabadiliko.
“Sheria haziruhusu Zitto kuwa na vyama viwili, yeye ni mwanachama halali wa CHADEMA kwa kuwa ana kesi mahakamani. Kama akipenda kuja aje na asifikirie ubunge wake kwani tunamuhitaji,” alisema.
Pia, alisema mbali ya kumshawishi Zitto kujiunga na Chama hicho, walikuwa na mpango wa kumshawishi Dk. Kittila Mkumbo ajiunge na chama hicho, wamekwama.
 
Alisema Dk. Kittila aliwaambia hataki tena kujihusisha na masuala ya siasa.
 
Mwigamba na Mkumbo walifukuzwa CHADEMA kwa madai ya kuandaa waraka wa siri waliouita wa mabadiliko ya uongozi uliokuwa ukieleza harakati za kuwang’oa viongozi walioota mizizi.

MATUKIO YA VURUGU YA CHADEMA
Viongozi na wafuasi wa chama hicho wanatuhumiwa kushiriki kwenye matukio ya vurugu ambazo baadhi zimekuwa zikigharimu maisha ya watanzania. 
 
Vurugu nyingi hutokea kwenye mikutano ya hadhara hasa wakati wa kampeni za uchaguzi.
 
Kwa sasa wanadaiwa kupeleka makundi ya vijana kutoka mikoa mbalimbali katika jimbo la Kalanga mkoani Iringa, ambako kunatarajia kufanyika uchaguzi mdogo wa ubunge.
 
Inadaiwa chama kiliingiza silaha mbalimbali jimboni humo vikiwemo visu, mapanga na marungu, ambazo zimekamatwa.

Soma Habari Kamili

CHADEMA NA CCM WAZIDI KUTOANA JASHO KALENGA

Kinamama wa Kijiji cha Makongati, Kata ya maboga, wakishangilia kumpokea Godfrey Mgimwa alipowasili kufanya mkutano wa kampeni...

*****
VYAMA vya CCM na CHADEMA vimeendelea kuchuana vikali kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, unaotarajia kufanyika Machi 16, mwaka huu, huku kila chama kikipinga hoja zinazotolewa na mpinzani wake.
 
Kampeni za vyama hivyo zinazidi kushika kasi, huku wapiga debe wa wagombea wa vyama hivyo wakiwanadi kwa nguvu zote wagombea wao.
 
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, Said Issa Mohamed, amepinga ahadi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Jimbo la Kalenga iliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, kwamba chama hicho hakiwezi kuitekeleza kwa kipindi kifupi kilichobaki, badala yake aeleze CCM imetumiaje zaidi ya sh. bilioni 300 za miradi hiyo katika halmashauri zote nchini.
 
Akizungumza juzi na wakazi wa Kijiji cha Ugwachanya kilichopo Kata ya Mseke, Wilaya ya Iringa wakati wa kampeni za kumnadi mgombea wa chama hicho, Grace Tendega, alisema ni kitu cha ajabu kumuona mtu mwenye dhamana, akitoa ahadi hewa ambazo hawezi kuzitekeleza.
 
Alisema walishindwa kutekeleza miradi hiyo ya barabara kupitia halmashauri kwa miaka 52 ya Uhuru, leo wataweza kutekeleza ahadi hizo. Alisema wanatafuta huruma ya wananchi wapigiwe kura, wakati CCM imeshindwa kutekeleza ahadi zake tangu uchaguzi mkuu ulipomalizika mwaka 2010.
 
"Mwigulu akija tena hapa muulizeni mbona tangu mwaka 2005 hadi 2014 hadi wanakuja kwenye uchaguzi huu hamuoni zaidi ya sh. bilioni 300 zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara?"Alihoji na kuongeza kuwa ahadi kwamba watajenga barabara kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani haiwezekani.
 
Alisema katika kipindi cha miaka takribani tisa, Serikali imetenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika halmashauri zote nchini lakini hakuna tija inayoonekana kutokana na matumizi ya mabilioni hayo ya fedha.
 
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Delfina Mtavalilo, amewataka wananchi wa Jimbo la Kalenga kuhakikisha wanamchagua, Godfrey Mgimwa, kuwa mbunge wa Jimbo hilo ili aweze kumalizia ahadi ambazo aliziahidi mbunge aliyefariki, Marehemu Dkt. William Mgimwa.
 
Hayo aliyabainisha jana jimboni hapa katika Kijiji cha Kikombwe wakati akimnadi mgombea wa CCM, Godfrey Mgimwa.
 
Alisema wananchi wa Kalenga ni vema wakamchagua mgombea wa CCM (Godfrey) katika uchaguzi unaotarajia kufanyika Machi 16, mwaka huu, kwani kufanya hivyo watakuwa wameonesha msimamo wa kukipenda chama hicho.
 
"Tunawashukuru kwani 2010 katika uchaguzi mkuu mlionesha msimamo wenu kwa kuifanya CCM ishinde katika nafasi ya Rais , mbunge na diwani. Hivyo tunaomba katika uchaguzi huu mdogo mchagueni mbunge wa CCM ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi," alisema.
 
Pia alisema kwa hali ilivyo katika kipindi hiki cha kampeni CCM itashinda kwa kishindo na moja ya sababu kubwa wananchi wanaridhishwa na utendaji kazi wa Serikali.
 
Alisema kuwa barabara nyingi za jimbo hilo zinapitika licha ya kutokuwa na lami, huku changamoto nyingine zikiendelea kutafutiwa ufumbuzi wake kupitia utekelezaji wa ilani.
 
Naye Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mtela Mwampamba, alisema mgombea wa chama hicho, si Mzungu kama wanavyodai.
 
Alisema CHADEMA baada ya kukosa ajenda katika kampeni wameanza kuzusha kuwa Godfrey si raia wa Tanzania.
 
"CHADEMA wanadai kuwa Mgimwa si Mtanzania.Huu ni uzushi mkubwa maana wenyewe mnaomuona Mgimwa ni Mtanzania na mzaliwa wa Kalenga," alisema.

Soma Habari Kamili

KAULI YA WAZIRI WA ELIMU YAWACHEFUA WALIMU


Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimekerwa na kauli ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa , kuwa serikali inaendelea kujadiliana na taasisi za fedha juu ya namna ya kulipa deni la malimbikizo ya mishahara ya  walimu yanayofikia Sh. bilioni 61.

CWT  imesema kauli hiyo ya serikali ni kutafuta visingizio baada ya  kushindwa kutekeleza ahadi yake kuwa ifikapo Februari, mwaka huu deni la walimu litakuwa limelipwa.

Rais wa CWT, Gration Mkoba,  alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema majadiliano ya mishahara ya walimu yalitokana na mgomo wa  2012 baada ya kukaa kwenye meza ya majadiliano na serikali ilikubali kulipa deni na kuandaa utaratibu wa kupandisha walimu madaraja.

“Inasikitisha kuona majadiliano yanahusisha waandishi wa habari bila ya kujua kuwa kwa kauli yake waziri tayari  walimu wameingia kwenye mgogoro na serikali, lakini  nawasihi walimu wasubiri tamko rasmi la mgogoro,” alisema.

Mkoba alisema tangu serikali ilipoahidi kutekeleza madai yao, hakuna hata dai moja  lililotekelezwa  lakini imewashangaza kuona ikijinadi kuwa inaendelea na majadiliano ya kulipa deni hilo wakati majadiliano hayana tija kwa mwalimu.

Alisema Novemba, mwaka jana mkutano mkuu wa CWT ulitoa siku 60 kwa serikali kukamilisha taratibu zote la kulipa malimbikizo ya mishahara ya walimu nchini.

Pia Januari mwaka huu kwenye kikao cha Baraza  la Taifa la CWT kiliazimia kuwa ifikapo mwishoni mwa Februari, mwaka huu, ikiwa serikali itashindwa kulipa malimbikizo hayo litakuwa tayari kuongoza mgomo.
 
CHANZO: NIPASHE

Soma Habari Kamili

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini