Sabrina au Habiba enzi za uhai wake.
AMA kweli dunia hadaa, ulimwengu shujaa! Kumeibuka mchezo mchafu, kuna
Watanzania wanawachukua warembo nchini na kuwapeleka China kwa ahadi
kwamba wanakwenda kufanya kazi saluni, wakifika kule wanawanyang’anya
paspoti na kuwauza kwa wanaume (ukahaba), sasa yamemkuta Mbongo aitwaye
Sabrina au Habiba, Ijumaa Wikienda lina mkasa wa kusikitisha.
Habari za uhakika kutoka kwa chanzo chetu nchini humo zilisema kuwa,
Sabrina (24), alifariki dunia Alhamisi iliyopita kufuatia kubakwa na
wanaume watano, raia wa Nigeria ambao wamo nchini humo kibiashara.
Tukio hilo lilijiri kwenye hoteli moja iliyopo kwenye Mji wa Guangzhou ambao umejaa wageni wengi, wakiwemo Watanzania.
SIKU YA TUKIO
Rafiki wa karibu wa Sabrina, Saada
alisema siku ya tukio, marehemu akiwa katika harakati zake za kutafuta
wateja alikutana na Mnigeria mmoja ambaye walipatana kulala wote kwa
usiku mzima.
“Kumbe yule Mnaigeria alikuwa na wenzake wanne. Usiku
walimwingilia wote kwa nguvu kwa kumbaka mpaka akapoteza maisha
palepale. Ni ukatili mkubwa.
“Wale watu walipogundua Sabrina amekufa waliuchukua mwili wake na kuutupa chini kutoka ghorofa ya tano,” alisema rafiki huyo.
MAITI YAKUTWA HAINA FIGO, MOYO
Habari zaidi
zilidai kuwa mpaka juzi (Jumamosi) madaktari waliokuwa wakiuchunguza
mwili wa Sabrina waligundua hauna figo na moyo, jambo linalozidi kuzua
hofu juu ya muaji yake.
NI BIASHARA ILIYOIBUKA CHINA?
Ilidaiwa kuwa
nchini China imeibuka biashara ya viungo mbalimbali vya binadamu ambapo
ili vipatikane ni lazima mwenye viungo hivyo auawe kwa njia yoyote.
SABRINA AFA, MGANDA APOTEA
Mtoa habari wetu
alisema wakati Wabongo wakiwa kwenye maombolezo ya kifo cha Mtanzania
huyo, mrembo mwingine raia wa Uganda, nchi ambayo imo ndani ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki amepotea katika mazingira ya kutatanisha nchini
humo.
Baadhi ya watu wana wasiwasi kuwa kupotea kwa msichana huyo kunahusiana na kushamiri kwa biashara ya viungo vya binadamu.
SABRINA ALIKWENDAJE CHINA?
Mwezi Julai, mwaka
jana, Sabrina alikwenda nchini humo akidanganywa na mwanamke mmoja
kwamba atapata kazi kwenye saluni ya wanawake lakini baada ya kufika
alijikuta akiingizwa kwenye biashara ya ukahaba bila ridhaa yake mpaka
alipokutwa na mkasa huo uliopoteza maisha yake.
TAHADHARI KWA WAREMBO WANAOKWENDA CHINA KUFANYA KAZI SALUNI
Imebainika kuwa, kumeibuka wimbi la Wabongo wanaofanya ‘uwakala’ wa
kuwachukua wasichana wa Kitanzania kwa kuwadanganya kwamba wanakwenda
kufanya kazi za saluni nchini humo.
Mara baada ya kufika, wasichana hao hunyang’anywa paspoti ili
washindwe kuondoka nchini humo na kushinikizwa kujiuza (ukahaba) huku
waliowapeleka wakipokea fedha kutoka kwa wateja.
KUIKOMBOA PASPOTI
Habari zilisema kuwa mhusika
hurejeshewa paspoti yake baada ya malipo yake kwa ‘wakala’ kufikia dola
za Marekani 8,000 (kama shilingi milioni 12), ndipo huachiwa ‘huru’
kuendelea na maisha yake.
Wengi wakishaachiwa hushindwa kurejea Bongo na kujikuta wakiendelea
kuuza miili katika mahoteli na klabu huku wakikutana na majanga
mbalimbali.
MASOGANGE, KAJALA NA DIDA
Watanzania waishio
nchini humo wamewatahadharisha mastaa wa Bongo, wakiwemo Mtangazaji wa
Radio TimesFM, Khadija Shaibu ‘Dida’, msanii wa filamu Kajala Masanja na
Video Queen Agnes Gerald ‘Masogange’ ambao hupenda kwenda nchini humo
kwa shughuli zao, kutokubali kuwa karibu na mawakala wa kuchukua
wasichana Bongo kwa kuwadanganyia kazi ya saluni kwani wanaweza kujikuta
pabaya siku moja.
DIDA
Ijumaa Wikienda lilimsaka Dida siku ya
Jumamosi iliyopita na kumuuliza kuhusu kuwepo kwa mawakala hao ambapo
alikiri kusikia huku akisema warembo wenyewe wanapaswa kuwa macho na
udanganyifu huo.
“Najua wapo Wabongo wanaofanya shughuli hiyo, si China tu hata India,
unapelekwa kwa ahadi ya kazi ya saluni, ukifika hamna cha saluni wala
nini? Warembo wawe makini jamani, nenda China kama una uwezo wako
mwenyewe kufanya ‘shoping’ lakini si kupelekwa,” alisema Dida.
BALOZI WA TANZANIA-CHINA
Juzi, Ijumaa Wikienda
lilimtafuta Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali Mstaafu
Abdulrahman Shimbo ili azungumze lolote kuhusu tukio la Sabrina, lakini
simu yake ilionekana kutokuwa hewani kwa muda mrefu.