MIPAKA YA HAUSIGELI NDANI YA NYUMBA!-3


Ni matumaini yangu kwamba umzima na unaendelea vyema na shughuli zako za kila siku kama kawaida. Mimi niko poa, namshukuru Mungu kwa kunifanya kuwa miongoni mwa wale wanaoendelea kupumua hadi leo.
Mpenzi msomaji wangu, wiki iliyopita utakumbuka nilianza kuzungumzia mada hii. Leo nitaenda moja kwa moja kwenye ile mipaka ya hausigeli ndani ya nyumba nikiamini mwisho wa siku wanandoa watajifunza kitu kitakachoziboresha ndoa zao.
Yapo mambo mengi sana ambayo hausigeli hapaswi kuyafanya ili kuilinda ndoa lakini baadhi ya wanawake aidha kwa kudharau au kutojua wamekuwa wakiyapotezea, matokeo yake unaweza kuingia ndani ya nyumba na kushindwa kujua hausigeli ni nani na mke ni nani.
Hapo ndipo unaweza kusikia habari za hausigeli kutembea na baba mwenye nyumba.
Kuepukana na matatizo hayo, ifuatayo ni mipaka ya hausigeli ndani ya nyumba.
Kwanza; Asiguse kabisa mlango wa kuingia chumbani kwa mabosi wake. Hapa nazungumzia suala la kutoingia chumbani kama ambapo baadhi wamekuwa wakiwaruhusu mahausigeli kuingia na kufanya usafi, jambo ambalo kimaadili halikubaliki.

Msichana wa kazi afanye usafi kote lakini chumbani asiruhusiwe kwani kule kuna siri ambazo hatakiwi kuzijua. Wanaolegeza kamba katika hili ndiyo ambao wanaishia kuvuna mabua.
Pili; Hausigeli asiwe na mawasiliano ya karibu na baba mwenye nyumba. Sasa hivi zipo simu za mkononi ambazo zinatumika katika kurahisisha mawasiliano lakini hausigeli hata siku moja asipewe mwanya wa kumpigia simu baba mwenye nyumba au kumtumia sms.
Baadhi wamekuwa wakiona si jambo baya, matokeo yake inapotokea msichana wa kazi ni mcharuko na baba mwenye nyumba naye hajatulia, wawili hao wanaweza kufungua ukurasa wa dhambi.
Tatu; Hausigeli asihusike katika suala la kufua nguo za ndani za mume. Hapa namaanisha soksi, boksa, ‘singland’ na nyinginezo. Jukumu hili libaki kuwa la mke!
Nne; Hausigeli asiruhusiwe kukaa sebuleni kama baba mwenye nyumba yupo. Wapo ambao wanajifanya wanaishi kizungu, baba yupo lakini na hausigeli naye ameganda sebuleni eti anaangalia tamthiliya, hii siyo sawa kabisa hasa kinidhamu.
Tano; Wakati hausigeli anakwenda bafuni kuoga, kwanza asiwe amevaa nguo nyepesi kama vile kanga moja na pia ahakikishe haonani na baba mwenye nyumba.
Sita; Hausigeli asipewe nafasi kumuandalia kitu chochote mume, kwa mfano chakula, maji ya kuoga, nguo za kuvaa na vinginevyo. Hii ni kazi ya mke lakini utashangaa baadhi yao wamekuwa wakibweteka na matokeo yake wanajikuta wameporwa waume zao.
Saba; Kama baba anakwenda sokoni kununua mahitaji ya nyumbani ya mwezi au wiki, asiongozane na hausigeli na kama kuna ulazima, hausigeli aende lakini asikae siti ya mbele.
Nane; Kama familia ina gari, hausigeli asipande akiwa na mtoto mdogo kwenda bichi, kanisani au ‘shopping’ bila kuwepo mama. Hii ni kwa sababu inakuwa rahisi mume ambaye hajatulia kumtongoza hausigeli na mtoto asijue kitu.
Akipanda na mtoto mkubwa mwenye akili ya kutambua mambo haina shida kwani wengi wao huwa wafichuaji wa siri hivyo baba ni vigumu kuongea upuuzi wowote kwa hausigeli.
Tisa; Hausigeli hata kama ana shida vipi, asipewe nafasi ya kumweleza shida zake baba mwenye nyumba. Hata mshahara inashauriwa kuwa mama mwenye nyumba ndiye wa kumkabidhi na si vinginevyo.
 Katika hili pia mke ahakikishe hakuna mwanya wa baba mwenye nyumba kumnunulia vijizawadi msichana wa kazi kwani madhara yake ni kuingia kwenye mapenzi.
Kumi; Hausigeli asimzoee baba mwenye nyumba kiasi cha kuona ni sawa kuzungumza naye wakati wowote na kutaniana kunakostahili kufanywa na wapenzi.
Hayo ni baadhi ya mambo machache ambayo ni vyema yakatiliwa maanani ili kuweza kuzitunza ndoa zetu na kupunguza uwezekano wa baadhi ya mahausigeli kuzipindua.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini