NDUGU wawili wa kiume wa familia moja wilayani Mlele mkoa wa Katavi, wanatuhumiwa kumuua mpenzi wa mama yao kwa kumchinja, kisha kutelekeza mwili wake porini.
Wakazi hao ambao mmoja ni mtoto mwenye
umri wa miaka 16 ni wakazi wa Kitongoji cha Milumba Kata ya Kibaoni na
aliyeuawa ni Kitungulu Luhende (65).
Inadaiwa mama yao, Sai Mponje (65) ambaye
ni mjane anayeshikiliwa na polisi kwa sasa, alikuwa na uhusiano wa
kimapenzi na Luhende, jambo ambalo watoto hao hawakufurahishwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi,
Dhahiri Kidavashari alitaja watuhumiwa hao ni Nyengu Kashele (19) na
nduguye mwenye umri wa miaka 16.
Mtoto huyo anashikiliwa wakati Nyengu
amejificha kusikojulikana. Mwili wa marehemu uligundulika Machi 3, mwaka
huu saa 3:30 asubuhi katika milima ya kitongoji hicho cha Milumba ukiwa
umeharibika.
Mwili huo uligundulika kutokana na msako
uliofanywa na askari wa jadi (sungusungu) kwa kushirikiana na polisi na
wananchi. Kidavashari alisema Februari 22, mwaka huu saa 2 asubuhi,
Luhende ambaye pia ni mkazi wa kitongoji hicho cha Milumba, alimuaga
mkewe kwamba anakwenda kijiji cha Kirida ambako ana mke mwingine.
Hata hivyo, Kamanda alidai kuwa badala ya
kwenda kijijini Kirida, aliko mke wake mwingine, kwanza alipitia
nyumbani kwa rafiki yake katika kitongoji hicho cha Milumba, aitwae
Milembe Katembeni ambako aliacha pikipiki yake yenye nambari za usajili T449 BAF. Inadaiwa kisha alikwenda moja kwa moja kwa Sai (mama wa watuhumiwa).
Kamanda alisema tangu hapo hakuonekana
hadharani hadi mwili ulipokutwa umetelekezwa eneo la milimani huku
pembeni kukiwa na leseni yake ya udereva.
Akielezea sababu za kuanza kumtafuta,
Kamanda alisema baada ya kutorejea kwa rafiki yake kuchukua pikipiki,
Katembeni aliingiwa wasiwasi ndipo Machi 2 , mwaka huu aliamua kutoa
taarifa kwa kiongozi wa sungusungu na kisha polisi, na msako ukaanza.
Source: Habarileo
0 comments:
Post a Comment