CHADEMA YAANZA MCHAKATO WA KUMTAFUTA MPINZANI WA RIDHIWANI KIKWETE KATIKA JIMBO LA CHALINZE


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza mchakato wa kutafuta mgombea wa kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Chalinze, ambapo jana fomu za kuwania nafasi hiyo kupitia chama hicho zilianza kutolewa.
 
Tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishaanza mchakato wa kutafutia mgombea wa kuwania nafasi hiyo, ambapo Ridhiwani Kikwete, alishinda kura ya maoni ya wanachama wa chama hicho na sasa anasubiri uamuzi ya vikao vya juu vya chama hicho.
 
Akizungumza nasi jana, Ofisa Uhusiano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema fomu hizo zinatolewa na kurejeshwa katika ofisi za Kanda ya Pwani ya chama hicho.
 
“Baada ya kurejesha fomu, walioomba kuwania nafasi hizo watapigiwa kura ya maoni na wanachama wa Chadema wa eneo husika, na baada ya hapo uamuzi wa mwisho utakuwa ni wa vikao vya juu,” alisema Makene.
 
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Uenezi wa Halmashauri ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, alisema bado chama hicho kipo kwenye mchakato wa kuandaa vikao vya juu, vitakavyoyachuja majina ya waliopigiwa kura za maoni na kuteua mgombea wa ubunge kupitia chama hicho.
 
“Tarehe rasmi ya vikao hivi vya juu bado haijapangwa, ndio tuko kwenye mchakato tukikamilisha tutawajulisha,” alisema Nape.
 
Juzi Ridhiwani alishinda kura ya maoni ya kumpata mgombea wa CCM katika jimbo hilo baada ya kupata kura 758, akifuatiwa na Shaban Madega aliyepata kura 335, Athuman Maneno kura 206 na Changwa Mkwazu aliyepata kura 12.
 
Uchaguzi mdogo wa Jimbo hilo la Chalinze, unatarajiwa kufanyika Aprili 6, mwaka huu na Machi 12, vyama vya siasa vitawasilisha majina ya wagombea wake kwa ajili ya kuthibitisha uteuzi wao.
 
Kampeni rasmi za uchaguzi huo zitaanza Machi 13, mwaka huu. Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo kufariki dunia.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini