Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Bagamoyo, anayetarajiwa kuwania ubunge Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amesema habebwi na baba yake, Rais Jakaya Kikwete, katika harakati zake za kisiasa.
Ridhiwani aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari juzi jioni
baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura za maoni katika jimbo hilo
kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Msata.
Alisema anafanya siasa bila kupitia mgongo wa baba yake, Rais Kikwete.
“Siasa ninayofanya haina mahusiano na baba yangu, nafanya siasa kwa
maisha yangu na sina ubia na baba yangu katika hili,” alisisitiza.
Akijibu swali la kwanini amejiingiza katika siasa tofauti na maneno yake
mwaka 2010 kuwa hawezi kushiriki katika kinyang’anyiro cha ubunge
kwenye jimbo hilo, Ridhiwani alisema hakuwa tayari kujitangaza kwa
kipindi hicho ili kutowapa nafasi maadui kutawala kabla ya wakati.
Aidha, Ridhiwani aliomba mshikamano na ushirikiano kwa wana-CCM
kufanikisha azima ya kutetea jimbo hilo katika uchaguzi unaotarajiwa
kufanyika mwezi ujao.
Katika kura za maoni, Ridhiwani alipata kura 758, Imani Madega, kura
335, Maneno kura 206 na mwanamke pekee aliyeshiriki katika mchakato huo,
Mkwazu Changwa, alipata kura 17.
Kamati Kuu (CC) ya CCM inatarajia kukutana Machi 8, mwaka huu kupitisha
jina moja litakaloshiriki kumpata mbunge wa Jimbo la Chalinze kufuatia
kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment