KANISA Katoliki limekanusha taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari kuwa msimamo wa kanisa hilo ni kuwepo kwa serikali tatu katika katiba mpya.
Askofu Mkuu wa
Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
amesema taarifa hiyo si sahihi bali ilitolewa na Tume ya Haki ya Baraza
la Maaskofu pasipo kumshirikisha.
“Wao kama
Watanzania wanayo haki ya kutoa maoni, hivyo si kosa wakiwa kama
Watanzania maoni yao kuwa ni kuwepo serikali tatu, ilichokosea tume hiyo
ni kusema kwamba huo ni msimamo wa Kanisa Katoliki jambo ambalo si
kweli,” alisema.
Pengo alisema
anakanusha vikali taaifa hiyo iliyotolewa juzi na vyombo mbalimbali vya
habari hususan magazeti na kuwa Kanisa Katoliki lina wajibu wa kutoa
msimamo wake katika mambo mawili tu yanayohusu imani na maadili.
“Kwa mfano
ikitokea hoja kwamba kuwepo na vipengele kwenye katiba vinavyosema
hakuna Mungu, kuwepo kwa ndoa za jinsia moja au kuhalalisha utoaji mimba
hapo kanisa lina haki ya kusimama na kutoa msimamo wake kwani masuala
hayo yanagusa imani na maadili,”alisema.
Aliongeza kuwa
anatumia nafasi hiyo katika mkutano na waandishi wa habari kutoa msimamo
wake kama Mtanzania wa kawaida kuwa mapendekezo yake ni kuendelea
kuwepo kwa serikali mbili yaani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
ile ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Kama kuna
dosari zozote zilizojitokeza wakati wa kuasisi Muungano zinazotishia
umoja wa kitaifa ni heri zikarekebishwa ili uendelee mfumo wa serikali
mbili kwani serikali tatu ni mzigo,” alisema.
Vilevile alitoa
maoni kuhusu suala la kura katika bunge la katiba na kusema kwamba
anaunga mkono kutumika kwa kura ya siri kwani ni ya uhakika zaidi kuliko
ya wazi ambayo wengine wanaweza kufuata mkumbo ili mradi wasionekane
wasaliti.
Mwishoni mwa
wiki iliyopita, Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Tanzania
(TEC) ilitoa tamko ikitaka Bunge Maalumu la Katiba kuepuka kukashifu
mapendekezo ya muundo wa serikali tatu.
0 comments:
Post a Comment