MAJIBU YA VIPIMO VYA DNA YAHATARISHA NDOA JIJINI MBEYA


ASILIMIA 40 ya Wanaume waliopima vinasaba ili kubaini uhusiano wa kibaiolojia na watoto wanaowalea, wamebainika kuwa watoto hao si wao licha ya kuzaliwa na wake zao au wapenzi wao.

Taarifa hiyo imetolewa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutokana na wanaume waliotaka kufahamu ukweli kuhusu watoto wao hadi Januari mwaka huu kwa mujibu wa Sheria ya Vinasaba vya Binadamu namba 8 ya mwaka 2009.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sabanitho Mtega, bado kuna tatizo la wanaume wengi kubebeshwa mzigo wa kuwalea watoto ambao si halali yao, licha ya kuaminishwa na wenzao wao kuwa ni damu yao.

Mtega, ametoa taarifa hiyo kwenye mahojiano na waandishi wa habari jijini Mbeya wakati wa Warsha ya siku Moja ya kuwaelimisha Wateja wa huduma za Mkemia Mkuu wa Serikali, lakini pembezoni mwa warsha hiyo, wanaume wanaona ni bora kulea mtoto bila ya kupima DNA kwani hatua hiyo ni hatari kwa uimara wa ndoa zao.

Hata hivyo, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Robert Mayala, amesema vipimo hivyo vimesaidia kutatua kesi nyingi za kubaini uhusiano baina ya baba na mtoto.

Warsha hiyo imewahusisha Waingizaji, Mawakala, Wasafirishaji, Wauzaji na Watumiaji wa kemikali na wadau wengine wa sekta hiyo wakiwemo TRA, Jeshi la Polisi, Madaktari na Waandishi wa Habari.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini