CHADEMA NA CCM WAZIDI KUTOANA JASHO KALENGA

Kinamama wa Kijiji cha Makongati, Kata ya maboga, wakishangilia kumpokea Godfrey Mgimwa alipowasili kufanya mkutano wa kampeni...

*****
VYAMA vya CCM na CHADEMA vimeendelea kuchuana vikali kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, unaotarajia kufanyika Machi 16, mwaka huu, huku kila chama kikipinga hoja zinazotolewa na mpinzani wake.
 
Kampeni za vyama hivyo zinazidi kushika kasi, huku wapiga debe wa wagombea wa vyama hivyo wakiwanadi kwa nguvu zote wagombea wao.
 
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, Said Issa Mohamed, amepinga ahadi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Jimbo la Kalenga iliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, kwamba chama hicho hakiwezi kuitekeleza kwa kipindi kifupi kilichobaki, badala yake aeleze CCM imetumiaje zaidi ya sh. bilioni 300 za miradi hiyo katika halmashauri zote nchini.
 
Akizungumza juzi na wakazi wa Kijiji cha Ugwachanya kilichopo Kata ya Mseke, Wilaya ya Iringa wakati wa kampeni za kumnadi mgombea wa chama hicho, Grace Tendega, alisema ni kitu cha ajabu kumuona mtu mwenye dhamana, akitoa ahadi hewa ambazo hawezi kuzitekeleza.
 
Alisema walishindwa kutekeleza miradi hiyo ya barabara kupitia halmashauri kwa miaka 52 ya Uhuru, leo wataweza kutekeleza ahadi hizo. Alisema wanatafuta huruma ya wananchi wapigiwe kura, wakati CCM imeshindwa kutekeleza ahadi zake tangu uchaguzi mkuu ulipomalizika mwaka 2010.
 
"Mwigulu akija tena hapa muulizeni mbona tangu mwaka 2005 hadi 2014 hadi wanakuja kwenye uchaguzi huu hamuoni zaidi ya sh. bilioni 300 zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara?"Alihoji na kuongeza kuwa ahadi kwamba watajenga barabara kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani haiwezekani.
 
Alisema katika kipindi cha miaka takribani tisa, Serikali imetenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika halmashauri zote nchini lakini hakuna tija inayoonekana kutokana na matumizi ya mabilioni hayo ya fedha.
 
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Delfina Mtavalilo, amewataka wananchi wa Jimbo la Kalenga kuhakikisha wanamchagua, Godfrey Mgimwa, kuwa mbunge wa Jimbo hilo ili aweze kumalizia ahadi ambazo aliziahidi mbunge aliyefariki, Marehemu Dkt. William Mgimwa.
 
Hayo aliyabainisha jana jimboni hapa katika Kijiji cha Kikombwe wakati akimnadi mgombea wa CCM, Godfrey Mgimwa.
 
Alisema wananchi wa Kalenga ni vema wakamchagua mgombea wa CCM (Godfrey) katika uchaguzi unaotarajia kufanyika Machi 16, mwaka huu, kwani kufanya hivyo watakuwa wameonesha msimamo wa kukipenda chama hicho.
 
"Tunawashukuru kwani 2010 katika uchaguzi mkuu mlionesha msimamo wenu kwa kuifanya CCM ishinde katika nafasi ya Rais , mbunge na diwani. Hivyo tunaomba katika uchaguzi huu mdogo mchagueni mbunge wa CCM ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi," alisema.
 
Pia alisema kwa hali ilivyo katika kipindi hiki cha kampeni CCM itashinda kwa kishindo na moja ya sababu kubwa wananchi wanaridhishwa na utendaji kazi wa Serikali.
 
Alisema kuwa barabara nyingi za jimbo hilo zinapitika licha ya kutokuwa na lami, huku changamoto nyingine zikiendelea kutafutiwa ufumbuzi wake kupitia utekelezaji wa ilani.
 
Naye Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mtela Mwampamba, alisema mgombea wa chama hicho, si Mzungu kama wanavyodai.
 
Alisema CHADEMA baada ya kukosa ajenda katika kampeni wameanza kuzusha kuwa Godfrey si raia wa Tanzania.
 
"CHADEMA wanadai kuwa Mgimwa si Mtanzania.Huu ni uzushi mkubwa maana wenyewe mnaomuona Mgimwa ni Mtanzania na mzaliwa wa Kalenga," alisema.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini