AJALI YAUA, MAGARI YAKWAMA KWA SAA TATU BARABARA YA DAR- MORO


Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa baada ya basi dogo kugongana uso kwa uso na lori katika eneo la Bwawani Barabara ya Chalinze - Morogoro. 
 
Ajali hiyo ilitokea jana saa 4.30 asubuhi baada ya basi hilo aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Ifakara kugongana na lori la mafuta lililokuwa likitoka Morogoro kuelekea Chalinze.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alimtaja aliyefariki dunia katika ajali hiyo ni dereva wa lori, Ally Ngoma (62).
 
Kamanda Matei alisema majeruhi 14 wa ajali hiyo ni abiria waliokuwa kwenye basi. Alisema wote walipelekwa katika Kituo cha Afya Chalinze kwa matibabu.
 
Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa basi kujaribu kuyapita magari mengine katika eneo la Sekondari ya Bwawani sehemu ambayo ina mwinuko.
 
Alisema wakati dereva huyo akijaribu kuyapita magari hayo, alikutana na lori hilo na kugongana uso kwa uso na kusababisha kifo na majeruhi hao.
 
Alisema dereva wa basi hilo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kujibu tuhuma zinazomkabili.
 
Barabara yafungwa
Mbali ya kusababisha kifo na majeruhi hao, ajali hiyo ilisababisha adha kwa waliokuwa wakitumia barabara hiyo hasa wale wanaosafiri kati ya Dar es Salaam na Morogoro kwani zaidi ya magari 200 yalikwama kwa zaidi ya saa tatu.
 
Ajali hiyo imetokea siku moja baada ya nyingine iliyosababisha vifo vya watu saba baada ya basi dogo la abiria kugongana na lori katika eneo la Chalinze Mzee na kujeruhi tisa.
 
Akizungumzia ajali hiyo ya juzi, Ofisa Habari wa Hospitali ya Tumbi, Kibaha, Gerald Chami alisema majeruhi sita hali yao wanaendelea vyema.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini