BAADA YA MAWAZIRI KUNG'OLEWA, WAKUU WA MIKOA NA WILAYA WATAPONA?, VIPI KUHUSU KAMATI ZA SIASA ZA MIKOA NA WILAYA?



HATUA ya kujiuzulu kwa mawaziri wanne kutokana na ‘uzembe’ uliojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ni ya uungwana.

 Ni heshima kwa kiongozi kuwajibika pale inapotokea anaowaongoza wamefanya uzembe uliosababisha maafa ama athari yoyote kwa taifa. Vifo, adhabu na udhalilishaji waliotendewa wananchi wenzetu si haki hata kidogo na katika hili hatuna maneno rahisi ya kusema yatakayoonyesha tumeumizwa na yaliyowapata wenzetu.

 

Upo mnyonyoro mrefu wa taasisi, viongozi na hata watendaji waliotekeleza Operesheni Tokomeza iliyoacha makovu ambao nao unatakiwa kuingia katika kundi la mawaziri hao.

Tunaamini kwamba wakati operesheni hiyo inatekelezwa kulikuwapo na wakuu wa mikoa na wilaya ambao kwa namna moja ama nyingine walijua kila kitu kilichokuwa kinaendelea.

Ni wazi kwamba kamati za siasa za mikoa na wilaya zilikuwa zikipewa taarifa za kila kilichokuwa kikitendekea kwenye maeneo yao, lakini walichukua hatua gani kuhakikisha wanazuia hali hiyo?.

Ushauri kwa Rais wetu wakati huu ambao anajipanga kuziba nafasi za mawaziri hao au kulivunja kabisa Baraza la Mawaziri awawajibishe pia wakuu wa mikoa na wilaya ili iwe fundisho kwa viongozi wengine na vizazi vijavyo.

kilichotokea katika Operesheni Tokomeza ni matokeo ya nidhamu mbovu kazini, ambayo imejengwa na utamaduni mbaya wa kuendesha ya kwa mazoea.

Nidhamu mbovu ya kazi kati ya viongozi na wanaowaongoza inachangia wafanyakazi wa ngazi ya chini kutowajibika na kufanya kazi kizembe na ndio matokeo ya operesheni Tokomeza.

Haiwezekani askari aliyefunzwa mbinu za kijeshi na nidhamu kazini afanye vitendo vya kubaka na kudhalilisha wananchi, Utu na heshima iko wapi?

Siku za nyuma niliwahi kuandika taratibu zinazotumika kuwapata vijana wanaokwenda kujiunga na vyombo vyetu ya ulinzi na usalama.

Uzembe unaanzia kwa viongozi kwa kuwapatia ajira watoto wa ndugu zao huku wakiamini pengine hawana sifa za kujiunga katika vyombo hivyo.

Siamini kama wote hao wanaweza kuwa hawana sifa la hasha lakini asilimia kubwa ya vijana wanaojiunga sasa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi yetu ukiangalia historia zao watakuwa wana undugu wa karibu na watendaji wa vyombo hivi.

Hii inawawia vigumu hawa kufanya kazi zao kwa ufanisi kwa kuamini kuwa uzembe wowote watakaoufanya watalindwa na dugu zao.

Hatukatai ndugu wa watendaji wa ngazi za serikali wasiajiriwe ikiwa wana sifa, hoja hapa ni kwamba wengi wao wanapewa ajira bila kuwa na sifa za kujiunga na majeshi hayo.

Ieleweke kwamba nidhamu mbovu si kwa watoto au ndugu wa watendaji hao tu bali ipo kwa vijana wengi wanaojiunga na majeshi yetu.

Kilichotokea katika Operesheni Tokomeza kiwefundisho katika katika uwajibikaji.

Mungu ibariki Tanzania.

0753 597500
MTANZANIA

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini