MADENTI HAWAWEZI KAMA MATICHA MIZINGUO


Mimi nipo vizuri, kwa sababu safari hii Pasaka ilikuwa bomba sana, nilishinda nyumbani na familia yangu.
Ni matumaini yangu pia kwamba hata nyinyi mliimaliza vizuri kabisa sikukuu hii ya kumbukumbu ya kifo cha Yesu Kristo na kwa wale ambao kwa namna moja au nyingine walikumbwa na masaibu yoyote, nachukua nafasi hii kuwapa pole na kuwatakia afya njema.
Tukirejea kwenye mada yetu ya leo, mara nyingi sana nimekuwa nikiwazungumzia zaidi wanafunzi kuliko walimu, hii yote ni kwa vile naamini kwamba madenti ndiyo wenye matatizo zaidi, hasa kwa kuwa ni kundi ambalo na mimi nimewahi kuwa miongoni mwao.
Lakini tuwajadili kidogo walimu. Kama kichwa cha habari pale juu kinavyosema, madenti hata wawe na bidii vipi, wajitoe kwa kiasi chote, ni nadra sana kufanikiwa kama maticha ‘wanazingua’, hakuna kinachofanyika.
Na hii sana ni kwa shule za serikali. Katika shule hizi, walimu hawana cha kupoteza, usome, usisome kwao ni sawa tu, mwisho wa mwezi ukifika, wanakwenda kukinga chao, maisha yanaendelea. Ni afadhali shule za binafsi ambako mwalimu anapimwa kwa kiwango cha taaluma cha wanafunzi wake, wakiona ‘analeta za kuleta’ wanaachana naye.
Katika hali ya kawaida, tunategemea kwamba mwalimu atakuwa ni mkubwa kiumri kuliko mwanafunzi wake na inapotokea kinyume chake, basi huwa ni jambo la kushtua kidogo, ingawa pia mwanafunzi wa namna hiyo, atakuwa ni mwenye kuelewa anachopaswa kukifanya akiwa shule.
Kwa maana hiyo, mwalimu anao uwezo wa kumsoma denti wake na kujua ni kwa namna gani atamfanya kulipenda somo lake. Kupenda kusoma ni jambo la kufundishwa, haliji tu lenyewe. Mwalimu anayefanikiwa kuwashawishi wanafunzi wake ni yule anayetumia mifano rahisi kwa anaowafundisha.
Wapo wanafunzi ambao hawayapendi baadhi ya masomo flani, hasa wengi wao huwa ni hesabu.
Masomo yanayochukiwa na wanafunzi ni yale ambayo walimu wake hawajui kufundisha.
Mimi ni shuhuda wa hili. Siku zote tokea nikiwa kidato cha kwanza sikuwahi kupenda hesabu, lakini nilikuja kulipenda somo hili nikiwa kidato cha nne baada ya kuja mwalimu wetu mmoja hivi ambaye alitufanya tulione ni somo rahisi.
Matokeo yake tukaona ni kama tumepata mwokozi, tukawa tunaomba vipindi zaidi vya hesabu kuliko masomo mengine na wanafunzi tulijazana darasani kusikiliza.
Walimu wanaofanikiwa ni wale wanaoonekana kujali kazi yao na wanaopenda wanaowafundisha waelewe, lakini wengi wao hulipua na kutupa lawama kwa wanafunzi. Wapo baadhi ya maticha huwafukuza hata madenti wanapotaka ufafanuzi wa masuala mbalimbali ambayo hawajaelewa.
Yapo masomo ambayo kutokana na mfumo wetu mbovu wa elimu, huonekana ni magumu. Lakini ukweli ni kwamba hakuna masomo magumu, isipokuwa yapo yenye changamoto.
Na tunajua kwamba walimu hufundishwa mbinu mbalimbali za kumrejesha mwanafunzi aliyetoka darasani kimawazo au ambaye amepotea njia.
Baadhi ya walimu waliofanikiwa, ni wale ambao wana mizaha mingi ya kuburudisha katika kutolea mifano ya masomo wanayofundisha kuliko wale wakali wanaotembea na fimbo mkononi.
Walimu wetu ni lazima wahakikishe wanatimiza vyema wajibu wao kwetu, kwa kutupatia tulichokifuata shuleni, kabla ya kututupia lawama kwa kuwa tu madenti hawana pa kusemea!

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini