HONGERA WEMA SEPETU, SASA LINDA HESHIMA!


Wema Sepetu akiwa na tuzo pamoja na kitita cha shilingi milioni moja alichopatiwa na GPL kwa kuibuka Ijumaa Sexiest Girl 2013/14.
KWAKO,
Wema Sepetu, staa wa ukweli unayeng’ara kimataifa. Sina wasiwasi nikisema hivyo maana namaanisha.
Leo nimekukumbuka kwa barua; nimefanya hivyo mara kadhaa kila ninapokuwa na jambo la kukushauri.
Kwanza nakupongeza kwa kutwaa taji la msichana mwenye mvuto wa kimahaba iliyotolewa na Gazeti la Ijumaa ‘Ijumaa Sexiest Girl’ wikiendi iliyopita pale Dar Live, Mbagala – Zakhem, Dar.
Ushindi wako ni baada ya kuwaacha mastaa wenzako wengi pembeni hadi kufikia fainali iliyokukutanisha na Jacqueline Wolper, Elizabeth Michael, Jokate Mwegelo na Nelly Kamwelu.
Vigezo vilizingatiwa lakini kubwa ilikuwa ni kumsaka msichana mwenye mvuto kuliko wenzake. Wema, ukijaribu kuangalia safari yako ya mashindano ya urembo, mara zote umekuwa ukifanya vizuri. Hujawahi kuwaangusha mashabiki wako.
Kwanza ulivaa viatu vya Miss Dar Indian Ocean na baadaye ukawakilisha Kanda ya Kinondoni kabla ya kupanda Miss Tanzania mwaka 2006 ambapo uliwabwaga wote na kuibuka kidedea. Huo ni uwezo wa juu sana. Nakumbuka katika kipindi kilichokuwa na ushindani mkubwa ni pamoja na hicho.
Fainali yenu ilikuwa na wasichana wenye mvuto na sifa hasa, lakini uliweza kupenya na kufanikiwa kuibuka kidedea. Tangu hapo umeendelea kuutunza vyema mvuto wako na hujaonekana kuchuja.
Tangu mwaka 2006 ukiwa na umri wa miaka 18 (kama ulivyosema), leo hii miaka nane baadaye una miaka 26 na bado unaonekana katika mwonekano mzuri. Hilo ni jambo zuri na la kujivunia kwa hakika.
Kwa kuwa shindano lenyewe la Ijumaa Sexiest Girl lilihusisha wasomaji, bila shaka walikuchagua kwa sababu wanakukubali katika mambo mbalimbali ya kijamii ukiachana na mvuto ambao kilikuwa kigezo kikuu.
Jambo kubwa kwako ni kuhakikisha unaendelea kutunza mwonekano wako, unashiriki katika mambo mbalimbali ya kijamii na kufanya vizuri katika kazi yako ya sanaa ya uigizaji unayoifanya kwa sasa.
Lazima utambue kuwa una jina kubwa na unakubalika; kazi yako ni kuifanya jamii izidi kukuamini; wasione walifanya makosa kukuchagua kwa kura nyingi ili uwe mshindi.
Nakusihi Wema, wewe ni staa, jiweke mbali na mazingira yanayosababisha skendo. Ishi kama kijana anayetambua thamani yake.
Wewe ni kioo cha jamii, jitahidi jamii ijiangalie kupitia kwako.
Ijifunze mambo mengi kupitia wewe. Zile sarakasi zako, achana nazo ili uendelee kutunza heshima ya ustaa wako. Habari zako magazetini acha zitawale, lakini kwa mazuri tu! Skendo zikae mbali na wewe.
Ukiamua, inawezekana!

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini