MR NICE ABONDWA TENA

Mwanzilishi wa staili ya Takeu kwenye Bongo Fleva, Nice Lucas Mkenda ‘Mr Nice’.
Ooh! Noo! Mwanzilishi wa staili ya Takeu kwenye Bongo Fleva, Nice Lucas Mkenda ‘Mr Nice’ amebondwa kwa mara nyingine na kusababishiwa majeraha makubwa mwilini, Ijumaa Wikienda lina kisa cha kusikitisha.
Habari za uhakika zilieleza kwamba tukio hilo lilijiri maeneo ya Sinza Afrika-Sana, Dar katika Klabu ya Ambiance.

Kikizungumza na Ijumaa Wikienda, chanzo makini cha habari ambacho kilishuhudia tukio hilo, kilisema kuwa Nice alikuwa maeneo hayo akifanya yake katika kipengele cha moja moto na moja baridi, ndipo akaanza kumshobokea demu wa jamaa aliyekuwa meza ya jirani.
Shuhuda huyo alidai kwamba baada ya Nice kukolea maji, alianza kumsarandia mwanamke huyo aliyekuwa na midume kadhaa wakifanya yao.
Hata hivyo, ilisemekana kwamba Nice alitaka kutumia ustaa wake kunyang’anya demu ndipo mwenye mwanamke wake akahisi kudhalilishwa.
Ilidaiwa kuwa kilichofuata ni kwamba yule jamaa akishirikiana na washkaji zake walimshushia Nice kipigo cha shetani hadi akapoteza fahamu kisha wakaingia mitini.
“Aisee jamaa walimpa kipigo cha hatari utadhani wanaua mwizi kisha wakatimua zao.
“Ndipo watu wakaanza kumpa msaada lakini alikuwa tayari ameumizwa vibaya.
“Kiukweli jamaa walidhamiria vibaya, sijui walitaka kumuua maana hadi watu wanashtuka tayari Nice alikuwa nyang’anyang’a kwa kipigo hicho cha kutisha.
“Kilichofuata ilikuwa ni kukimbizwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar kwa ajili ya matibabu,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kupata taarifa hizo, Ijumaa Wikienda lilifika hospitalini hapo ili kutaka kujihakikishia kile kisemwacho ambapo wanahabari wetu waliambiwa kuwa mtu huyo yuko katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) hivyo haruhusiwi mtu kuingia.
“Ni kweli Nice yupo hapa hospitalini ameletwa akiwa hajitambui, ameumizwa vibaya mno hivyo vuta subira kidogo aendelee kupewa matibabu, akipelekwa wodini utaenda kumuona,” alisikika nesi mmoja.
Pamoja na ugumu huo, wanahabari wetu hawakukata tamaa ambapo walijipenyeza ‘kimafia’ hadi hadi ndani ambapo walimkuta Nice amelazwa, hali yake ikiwa ni ya kusikitisha mno.
“Kaka wamenipiga sana, nimeumizwa bila hata sababu yoyote, sijui kosa langu ni nini, hapa nilipo nina maumivu makali kila sehemu ya kiungo cha mwili wangu, kila nikifikiria sijui nimewakosea nini wale jamaa,” alisema Nice kwa taabu.
Hata hivyo, kabla ya kukimbizwa hospitali alipitishwa katika Kituo cha Kijitonyama maarufu kwa jina la Mabatini na kupewa RB yenye namba KJN/RB/2698/014- SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI.
Si mara ya kwanza kwa Nice kupigwa na kutolewa ngeu kwani miaka kadhaa iliyopita aliwahi kubondwa mara mbili hadi watu wakahisi amekata kamba (amekufa) kisha akapigwa picha za aibu. 

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini