Mama yake na marehemu Hussein Mkieti aka ‘Sharo Milionea’ .
Makubwa! Mama mzazi wa aliyekuwa nyota wa filamu na muziki, marehemu
Hussein Mkieti ‘Sharo Milionea’ amemtuhumu msanii wa vichekesho ambaye
alikuwa rafiki wa mwanaye, Musa Kitale kuwa alikula michango ya
kumbukumbu ya kifo cha mwanaye, mwaka jana.
Kwa mujibu wa chanzo makini, Mama Sharo amekuwa akimlalamikia Kitale
kwa watu kwamba alikula fedha za mchango wa mwanaye hivyo kupigwa
marufuku kwamba kitu chochote kinachomhusu Sharo asipewe.
Ilidaiwa kwamba, chanzo cha mama Sharo kutaka Kitale asipewe kitu
chochote kinachomhusu marehemu ni baada ya hivi karibuni Klabu ya Bongo
Movie Unity kutangaza kuwa litatoa Tuzo kwa Sharo Milionea kama
kumbukumbu kwani alikuwa ni mwenzao katika tasnia ya filamu.
Ilisemekana kuwa mama huyo alielezwa kwamba tuzo hiyo itapokelewa na
Kitale ndipo alipokataa na kusema hataki kabisa kitu chochote kipitie
kwa msanii huyo kwa sababu huwa hamfikishii.
Msanii wa vichekesho Musa Kitale.
“Mama Sharo amekuwa akilalamika kwa muda mrefu sana kwamba Kitale
anatumia vitu vya mwanaye, eti alichangisha michango ya kumbukumbu
hakumfikishia hivyo kwa sasa ameamua kupiga marufuku asikabidhiwe kitu
chochote,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kupata habari hizo, wanahabari wetu walimtafuta Kitale
ambapo kabla hata ya kujibu tuhuma hizo, alinyanyua simu na kumpigia
mama Sharo kumuuliza kama kweli amezungumza madai hayo.
Mama Sharo alikiri kuwa ni kweli alizungumza akidai alifikia uamuzi
huo baada ya kutonywa na watu kuwa Kitale amekuwa ‘akichikichia’ fedha
za marehemu mwanaye.
Kitale, baada ya kujiridhisha, alitoa ufafanuzi kuwa madai hayo
hayana ukweli na kudadavua kwamba wakati wa kumbukumbu ya Sharo mwaka
mmoja (Novemba) tangu alipofariki dunia, hakuna michango yoyote
iliyotolewa.
“Inaniuma sana kwa sababu enzi za uhai wa Sharo hatukuwahi kugombana
hata siku moja na mama Sharo alikuwa analitambua hilo, tuliishi kama
ndugu na mimi ndiye niliyemsaidia mpaka akapata umaarufu lakini sasa
namshangaa huyu mama kunishutumu vitu vya uongo,” alisema Kitale kwa
huzuni huku jasho likimtiririka.
0 comments:
Post a Comment