KWA NINI UJUTE BAADAYE? WAKATI NI HUU WA KUTIMIZA WAJIBU -3


MSINGI wa makala haya ni kukutaka ubaki njia kuu. Usiupuuze uhusiano wako unaokupa faraja kwa tamaa za muda mfupi. Tupo sehemu ya tatu, na ni imani yangu kubwa kwamba mwisho wa somo hili, utajifunza kitu kikubwa sana.
Ni ukweli ulio wazi kuwa huna sababu ya kujuta, badala yake unachotakiwa kufanya ni kutimiza wajibu wako leo. Siku zote ni lazima ukumbuke kuwa mapenzi uliyonayo au unayopata kutoka kwa mwenzi wako hivi sasa, yanaweza kuendelea au kukoma kutokana na uhusika wako.
Janga kuu ambalo limeendelea kusumbua ni kuwa mtu akiwa nacho anaweza kukifuja utadhani hakitaondoka. Ni kosa kubwa kushindwa kumtunza mwenzi wako kwa kiburi tu kuwa kwako ameshafika na hataondoka. Usicheze na moyo wa mwenzio. Usifanye majaribio ya kujuta baadaye.
Kufanya jambo lolote la maudhi kwa mwenzi wako kwa makusudi ni jaribio la wewe kujuta baadaye. Unayemuudhi ni binadamu, ana moyo kama ulionao wewe. Siku atakapofanya uamuzi ambao anaona unafaa, itakuwa ndiyo mwanzo wa majuto yako. Majuto ni mjukuu!
TWENDE KWA MIFANO
Kuna uhusiano wa Hawa na Matali, vilevile Gaudensia na Reina. Kila mmoja una somo lake. Hawa alimchezea sana Matali ambaye alipoona yamezidi aliondoka. Reina naye alijiona kidume, akamtenda sana Gaudensia, alipoona mazito, akatimka. Baadaye kila mtenda alilia kwa kusaga meno.

Kabla sijaenda zaidi kudadavua mifano hiyo, nieleze tu kwa kifupi kwamba tamaa na fedha ni sababu kuu ya majuto. Mwanamke au mwanaume, anaweza kudharau heshima na mapenzi anayopewa na mwenzi wake kwa sababu ya fedha au ‘upofu’ wa kudhani aliye mbele yake ana mvuto zaidi.
Ni shida! Mwenzi wako upo naye siku zote lakini macho yanakudanganya kwamba uliyekutana naye barabarani au katika mkusanyiko mwingine wowote ni mzuri kuliko mpenzi wako. Akili yako inaamini hivyo, matokeo yake unafanya uamuzi ambao baadaye unaujutia.
Mapenzi yana tabia ya kisasi, utakaposoma mifano ya Gaudensia na Reina, vilevile Hawa na Matali, utaelewa hili katika sura pana. Siku zote za maisha yako, jitahidi kubaki njia kuu. Uliyenaye ndiye mwenzi wako, umetoka naye mbali, kwa hiyo mpende na kumheshimu, achana tamaa zisizo na kichwa wala miguu.
Ni kweli ana mvuto lakini kabla hajakutana na wewe, ameshavutia wangapi? Je, unadhani aliyekuwa naye kwa nini aliinua mikono na kumwacha aende? Ikiwa yeye ndiye katendwa, ameshaumizwa mara ngapi? Kwa nini yeye? Unadhani nafasi yako inatosha kumfanya awe na furaha?
Utaingia kwake kwa kuona ana mvuto unaosuuza moyo wako, kumbe mwenzio ni mkali wa kuwapanga, hajui kukataa mtu! Siku za baadaye unakuja kugundua mpo kama sita lakini mwenyewe anajua jinsi ya kucheza karata zake, kwa hiyo hukuwahi kulijua hilo kabla.
Umeona pesa zake ni bora kuliko penzi safi na salama unalopata kutoka kwa mwenzi wako. Miezi miwili baadaye unajikuta upo kwenye kundi la wengine wengi ambao wanamtazama mtu mmoja kwa sababu ya fedha zake. Tayari unajigundua kwamba uliyenaye si wa uhakika, hana mapenzi, isipokuwa jeuri ya fedha inamuongoza kufanya uamuzi.
Labda ni fedha zako ndizo zinakufanya uwe na kiburi, unaamua kumtenda anayekupenda kwa dhati kwa hisia kuwa fedha ndiyo kila kitu. Itaendelea wiki ijayo.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini