Zaidi ya wakazi 300 wa kitongoji cha Olmapinuu katika kijiji cha Bwawani wilaya ya Arumeru, juzi waliwashikilia kwa saa sita askari wanne wastaafu wa Jeshi la Wananchgi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa na trekta lao wakidai kuwa wamevamia eneo la shamba la wanakijiji hao.
Wananchi hao waliwatishia wastaafu hao kuwa watawateketeza kwa moto endapo wataendelea kulima shamba hilo.
Sakata hilo la ni mwendelezo wa migogoro ya ardhi wilayani Arumeru.
Hata hivyo, lilimalizika kwa amani baada ya viongozi wa Halmashauri ya
Arusha Vijijini wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Bwawani, Lazaro
Orasirasi, kuingilia kati na kuwapoza wananchi hao ambao walikuwa
wamejiandaa kwa shari wakiwa na silaha za jadi za aina mbalimbali.
Kwa upande wao, wanajeshi hao wastaafu walidai kupewa shamba hilo kihalali na mamlaka zinazohusika.
Walifika shambani hapo wakiwa na trekta lenye namba za usajili T 814 CDZ
huku wakiwa na bunduki tatu aina ya rifle tayari kwa lolote.
Mmoja wao ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alisema walipewa
eneo hilo mwaka 2012 lakini tangu wakati huo wameshindwa kufanya lolote
kutokana na wananchi kudai kuwa eneo hilo ni lao walilopimiwa na
kumilikishwa kihalali na kufuata taratibu zote za kisheria.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Saanay Mesiaki, aliwaambia waandishi wa
habari waliofika katika shamba hilo kuwa wamekuwa wakiishi katika eneo
hilo kwa miaka zaidi ya 50 na mwaka 2005 walichangishwa Shilingi milioni
tatu kwa ajili ya kupimiwa eneo hilo lakini tangu wakati huo hawajapewa
hati yoyote zaidi ya kuona kwamba wanavamiwa na wastaafu hao.
"Sisi tumezaliwa na kukulia hapa na tumezika wazazi wetu na hata mababu
zetu hapa na tulichangishwa Shilingi milioni tatu na kutoa mbuzi saba
kwa ajili ya kupimiwa eneo hili, sasa hawa wanaotuvamia na mabunduki
wametoka wapi na wanataka nini hapa?,” Alihoji.
Aliongeza: "Baada ya eneo letu kuvamiwa tulilalamika hadi wilayani kwa
mkuu wa wilaya na amri tuliyopewa ni kwamba sote (sisi na wavamizi),
tusifanye lolote hadi ufumbuzi wa suala hilo utakapopatikana.
Sasa tunashangaa wenzetu wanakuja na matrekta na bunduki…sisi hatuogopi
na tuko tayari kufa kwa ajili ya eneo letu," alisisitiza Mwenyekiti huyo
huku akishangiliwa na wananchi.
“Hatutaki damu imwagike hapa lakini pia tueleweke kwamba tunadai haki
yetu na kamwe hatutishwi na lolote wala hatumwogopi yeyote,” alisema.
Alisema kwamba wanajeshi hao wastaafu 30 waliingia katika shamba hilo
bila kufuata taratibu kwa kuwa si serikali ya kijiji wala kitongoji
iliyopewa taarifa zozote za ujio wa wao.
Alisema kwamba shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 708.9 ambalo awali
lilikuwa linamilikiwa na Kampuni ya Lucy Estate, ni mali halali ya
wananchi wa kitongoji hicho ambao ni wafugaji wa Kimasai.
Aliongeza kuwa uamuzi wa wananchi hao kuwaweka chini ya ulinzi wanajeshi
wastaafu hao na trekta lao, umetokana na hatua walizochukua mwaka jana
ambapo wanadaiwa kufyeka ekari 35 walizolima wananchi hao zikiwa na
mahindi na ngwara na kuwasababishia ukosefu wa chakula bila sababu
yoyote.
Akizungumza na wananchi hao, Diwani Orasirasi ambaye alifuatana na
baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo, alithibitisha wananchi hao
kuchangishwa kwa ajili ya upimaji wa eneo hilo, lakini akasema kuwa
taratibu za kisheria bado hazijakamilika ili kuwakabidhi eneo hilo.
Hata hivyo, alipoulizwa kuwa ilikuwaje kuwachangisha wananchi kupimiwa
eneo ambalo lina mmiliki halali kisheria, Diwani huyo hakujibu swali
hilo zaidi ya kusema kwamba taratibu za kisheria zinaendelea ikiwa ni
pamoja na kumshawishi mmiliki huyo kuwagawia wananchi sehemu ya shamba
hilo.
Migogoro ya ardhi wilayani Arumeru imekuwa ni tatizo sugu kutokana na
wamiiliki wachache wa mashamba makubwa kuhodhi eneo kubwa huku wananchi
wakikabiliwa na uhaba wa ardhi.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment