JIJI LA ARUSHA LAVUNJA NYUMBA ZAIDI YA 330 ILI KUPISHA UJENZI WA MIRADI MBALIMBALI KATIKA MAENEO HAYO

Halimashauri  ya jiji   la  Arusha  imebomoa  nyumba  zaidi  ya  330  baada  ya  kushinda  kesi  iliyofunguliwa  na  waliokuwa  wapangaji  waliokuwa  wakipinga  amri ya  kuhama  kupisha  zoezi  la  ujenzi  wa  nyumba  za  kisasa.

Mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa unatekelezwa  na Halmashauri ya jiji  kwa  kushirikiana  na wadau  mbali mbali.

Bomoa bomoa hiyo ilianza jana alfajiri na wananchi   wakiwemo  vijana  walitoa ushirikiano   wa  kufanikisha zoezi hilo  huku  baadhi ya wapangaji   wakiwalaumu   wanasiasa  kwa  kuwapotezea  muda  na gharama  kubwa  ya  kwenda  mahakamani wakijua  wazi  kuwa  hawatashinda kesi hiyo.

Abdalah Hassan Mmbaga  na zainabu  jabiri  ambao ni miongoni mwa wananchi ambao nyumba zao zilibomolewa, walisema inashangaza  kuona  wakati wa  zoezi  hilo  wanasiasa  wanajiweka  pembeni  wakati  wao  ndio  waliokuwa  vinara  wa  kuwapa  wananchi moyo  kuwa  watawasaidia  na  hawatahamishwa. 

“Kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani wa Kata nne, tukiwa eneo la Ilboru Naibu Meya wa Jiji la Arusha alituhakikishia kwamba notisi zimesimamishwa hivyo wapangaji tusubirie mpaka tamko litakapotoka.

Mwanasheria  wa  jiji  la  Arusha, Kiomoni  Kiburwa    na  Mkuu wa  wilaya,  John Mongela  wamesema  zoezi  la ubomoaji limezingatia  taratibu zote  za  kisheria  na  haki  za  pande  zote  zikiwemo  za  wapangaji  ambao  walipewa  muda  wa  kutosha  wa  kuhamisha  vitu vyao.

Kibamba alisema uamuzi huo umekuja baada ya kuwapo kwa majibizano ya muda mrefu baina ya wapangaji wao 216 na Halmashauri hiyo waliokuwa wakiongozwa na Sumari.

Alisema kwa miaka mingi Halmashauri hiyo ilipanga kuyaendeleza maeneo hayo kwa kuvunja nyumba za zamani na kukaribisha uwekezaji mkubwa lakini waliokuwa wapangaji wao waligoma na kukimbilia mahakamani.

Kiomoni alisema kabla ya kukimbilia mahakamani kufungua kesi wapangaji wao waliweka masharti magumu matatu dhidi ya mwenye nyumba wakitaka kupewa fidia ya kukaa kwenye nyumba hizo.

Alisema masharti mengine yalikuwa ni Halmashauri iwajibike kuwatafutia viwanja kwingine ili wakajenge na  la mwisho kuwa waangaji hao walitaka kupangishwa kwenye uwekezaji utakaofanywa,” alisema  Kiomoni.

 “Tumewahi kuiomba Mahakama iwape notisi ya miezi sita kuanzia Januari 11, Mwaka 2013 wakae bila malipo wakati wakitafuta nyumba kwingine. Juni 10, Mwaka 2013 ilikuwa ukomo wa notisi iliyotolewa hivyo Jiji lilitaka kuvunja nyumba zake.

“Wapangaji walikwenda Mahakama Kuu wakafungua kesi namba 23 ya 2013 hivyo ilitolewa amri ya zuio la muda hadi hapo madai yao yatakaposikilizwa. Lakini na sisi tuliweka pingamizi kwamba hapakuwa na mgogoro kati yetu na wapangaji.

Hata hivyo kuvunjwa kwa nyumba hizo kumeleta neema kwa baadhi ya watu wakiwamo vijana wanaokusanya vyuma chakavu kuvamia maeneo hayo na kuokota kila aina ya chumba au kitu ambacho waliamini kinaweza kuuzwa na kuwapatia fedha.

Mkuu  wa  Mkoa  wa  Arusha,   Magesa  Mulongo amewataka wakazi wa  arusha  wakiwamo  wanaohamishwa  kutambua  kuwa  zoezi  hilo  linafanyika  kwa  nia  njema ya  kuboresha jiji  kwa  maslahi  wananchi  wote  na  taifa na kuomba kuendelea  kutoa   ushirikiano  wa  kukabiliana  na changamoto mbali mbali  zinazokwamisha maendeleo .
 

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini