MTIKILA AWA BURUDANI BUNGENI


MWENYEKITI wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amekuwa burudani ya aina yake katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma kutokana na misimamo na misemo yake wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Mtikila hukusanya idadi kubwa ya waandishi kila anapozungumza huku baadhi ya wanasiasa na wajumbe wengine wa Bunge la Katiba wakimshangaa.
Jumatatu iliyopita, Mtikila alishangaza alipodai kwamba Baba wa Taifa, hayati  Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, hayati mzee Abeid Amani Karume hawakuziunganisha Zanzibar na Tanganyika, bali kitendo hicho kilifanywa na majasusi wa CIA wa Marekani, kwa ajili ya kuhofia hali ya usalama wakati ule wa vita baridi kati ya Mataifa ya Magharibi na iliyokuwa dola ya Urusi, USSR.
“CIA hawakutaka yatokee ya Cuba, walisema kabisa kwamba we don’t want another Cuba in Africa (hatutaki Cuba nyingine Afrika), isipokuwa hawa akina Nyerere walitumiwa tu,” alisema na kusababisha vicheko kutoka kwa waandishi na wengine waliomsikia.
Kuhusu suala la posho, Mtikila alizidi kuwa burudani alipodai wao wanastahili nyingi zaidi kwani wajumbe wa Tume ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba walilamba fedha nyingi wakati kazi yao ilikuwa ndogo kuliko wao watakayoifanya kwenye Bunge Maalum la Katiba. 

credit: GPL

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini