Wananchi kadhaa wameeleza kusikitishwa na mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba, huku wakimtaka Rais Jakaya Kikwete aikemee hali hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.
Hellen-Kijo Bisimba, amesema, ni aibu kwa kinachoendelea katika bunge
hilo.
“Leo (jana) niliacha kazi zangu na kujipa muda wa kuangalia shughuli ya
hilo bunge na kwa kweli nimeishia kuwa dis-appointed (nimekatishwa tama)
na nilichokiona, kiasi cha kuandika kwenye ukurasa wetu wa face book,”
alisema.
Alisema alishangaa sana jinsi wajumbe wanavyozomeana, kiasi cha
kutomsikiliza hata mwenyekiti, kinyume na utaratibu unaowataka wajumbe
wakae pale mwenyekiti anaposimama.
“Mivutano yao haina tija na badala yake wanapoteza hela za Watanzania
bure…yaani kama kwa kipindi chote cha wiki tatu bado wanahangaika na
kanuni, itakuwaje wakiifikia rasimu yenyewe,” alisema.
Dk. Bisimba alisema ili kuwaweka kwenye msitari, ni wakati wa Rais
Kikwete aliyewateua sasa kuikemea hali, ili warudi kufanya kazi
iliyowapeleka ya kutupatia katiba tunayoitaka.
Profesa Mwesiga Baregu alisema hali hiyo inatokana na wajumbe kutopata semina ya kuwaandaa.
“Tungekwenda sawa kama wangepata semina ya kuwafunda ili wajue
kilichowapeleka kule, na kitu gani wananchi wanakitarajia kutoka kwao,
bahati mbaya haikuwepo,” alisema na kwua kinachoonekana katika kadhia
hiyo, ni kutokuwepo kwa ratiba ya kuliongoza hilo bunge.
“Nasema hivyo kwa sababu ukiwa na ratiba, itakuongoza katika shughuli
zako kwa kuwa utaangalia shughuli ulizo nazo na muda ulio nao, na
itakusaidia kujitathmini kama unaenda vizuri,” alisema.
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema
mambo yanayofanyika Dodoma katika Bunge la Katiba yanawahuzunisha
wananchi.
Pia, alisema bunge hilo halikufanyiwa maandalizi mazuri kabla ya kuanza na ndiyo maana mambo hayo yanatokea.
Aidha, Dk. Bana alisema Bunge hilo linayumba kwa sababu bado halijapata
Mwenyekiti wa kudumu na kwamba anaamini akipatikana Mwenyekiti wa kudumu
litatulia na kuendeshwa vizuri.
Aliitaka Kamati inayomshauri Mwenyekiti wa muda izingatie suala la muda
kwa sababu kuahirishaahirisha kunaweza kuchelewesha kufanikisha
shughuli hiyo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alisema
wabunge wanatakiwa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili waweze
kufanikisha kazi hiyo.
Alisema watanzania wanahitaji kupata Katiba nzuri, lakini wabunge wa
bunge hilo wanatakiwa kuzingatia muda na kutolifanya bunge hilo kuwa
mzigo mkubwa kwa kuwa gharama inayotumika ni kubwa.
“Naelewa umuhimu wa kupata muafaka, lakini ninaomba usicheleweshwe sana
na ukasababisha mambo mengine yashindwe kufanyika, wakumbuke pia kwamba
hapo baadae watahitaji kuingia katika bunge la bajeti,” alisema Kinana
na kuongeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema
tatizo kubwa linalosabisha kutokea kwa vurugu katika bunge hilo ni
kutokana na wajumbe kutakunguliza maslahi ya vyama vyao na kusahau
kwamba kilichowapeleka ni kwa ajili ya Watanzania.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment