Chama kipya cha siasa cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania) kimeanzishwa na kupewa usajili wa muda huku kikitamba kuwa mbadala wa vyama vyote vilivyopo sasa kwa maelezo kuwa vimekosa demokrasia ya kweli.
Miongoni mwa viongozi wa muda wa chama hicho ni
Samson Mwigamba aliyetimuliwa uanachama wa Chadema kutokana na
kuhusishwa na waraka uliotaka kumwandaa Zitto Kabwe kuwania uenyekiti wa
chama hicho....
Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, alitimuliwa
pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, huku
uanachama wa Zitto aliyevuliwa nyadhifa zake zote zikiwamo za Naibu
Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, ukisubiri kesi
aliyofungua mahakamani.
Ifuatayo ni taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana wakati wa ufunguzi rasmi wa chama hicho....
******************************************************
Ifuatayo ni taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana wakati wa ufunguzi rasmi wa chama hicho....
******************************************************
ALLIANCE
FOR CHANGE AND TRANSPARENCY
(ACT
– TANZANIA)
“MABADILIKO NA UWAZI”
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Jumatatu, 03 Machi 2014, Dar es
Salaam
1.
Utangulizi
Ndugu wana habari,
Naomba nichukue fursa hii kuwashukuru kwa kuitikia
wito wa kuhudhuria mkutano wetu, ambao ni wa kwanza tangu chama chetu
kianzishwe. Tunatambua na kuheshimu kazi yenu kama mhimili wa nne wa dola, na
leo tunaomba kuzungumza na watanzania kupitia kwenu.
Lengo kuu la mkutano huu ni kukitambulisha kwenu
chama kipya cha siasa kinachoitwa Alliance for Change Tanzania (ACT Tanzania)
na kuwaombeni kukitambulisha chama hiki kwa watanzania kupitia vyombo vyenu vya
habari.
2. ACT Tanzania ni nini?
Ndugu Wanahabari,
ACT – Tanzania ni kifupi cha maneno: Alliance for
Change and Transparency, yaaani Umoja wa Mabadiliko na Uwazi. Ni chama kipya
cha siasa kilichoanzishwa kwa lengo mahsusi la kuwaleta pamoja watanzania
wanaoamini kwamba nguvu ya pamoja inahitajika katika kuleta mabadiliko ya
kweli katika nchi hii, na kwamba uwazi na uadilifu ni tunu ambazo taifa hili linazihitaji
sana kwa sasa na baadaye.
3. Itikadi na Misingi ya ACT Tanzania
ACT Tanzania ni chama
kinachoaamini katika demokrasia jamii na chenye shabaha
kuu ya kupigania na kusimamia mabadiliko
na uwazi nchini Tanzania.
ACT-Tanzania inaamini kuwa mabadiliko yoyote katika jamii lazima yainufaishe
jamii husika, na kwamba wananchi wenyewe ni lazima washiriki katika kuleta
mabadiliko hayo kwa uwazi na uzalendo. Mwongozo wa sera za ACT-Tanzania ni maendeleo shirikishi na kuhakikisha uwepo
wa uongozi adili katika ngazi zote.
ACT Tanzania inaongozwa
na misingi mikuu mitano ifuatayo:
i)
Uzalendo
ACT-Tanzania inaamini kwamba kila
mwananchi ana wajibu wa msingi kabisa wa kutoa mchango wake katika jamii na
Taifa kwa ajili ya kuhifadhi ustawi wa nchi kwa ajili ya kizazi cha leo na cha
baadaye. Ili wananchi waweze kutoa mchango huu kwa dhati na kwa moyo, ni muhimu
mazingira yawepo ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaipenda nchi yao. Kwa msingi
huu, ACT-Tanzania itajenga mazingira mwafaka ya wananchi kuipenda nchi yao ili
wajitoe kikamilifu katika kuijenga na kuilinda. ACT-Tanzania itajenga mazingira
yatakayoongeza uzalendo wa wananchi kwa kuhakikisha uwepo wa uwazi, ulinzi na
utumiaji bora wa rasilimali za taifa na uadilifu wa viongozi.
ii)
Usawa
ACT-Tanzania inaamini katika usawa katika
yyanja zote. Tunaamini kwamba mafanikio ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla
yatatokana na bidii katika kazi. Kwahiyo, ACT Tanzania kitapigania kuwepo usawa
wa fursa na mazingira mazuri kwa wote katika kuhakikisha kwamba kila mtu na
kila kundi katika jamii linakuwa na fursa sawa ya kufanya kazi za kujiajiri au
kuajiriwa, na kwamba kipato kitokanacho na kazi halali ndicho kitakuwa kipimo
cha mchango wake katika jamii na taifa.
iii)
Uadilifu
Uadilifu katika maisha
binafsi na katika jamii utakuwa ndio msingi na mwongozo mkuu wa viongozi na
wanachama wa ACT-Tanzania. ACT-Tanzania inaamini kwamba uadilifu ndio msingi na
nguzo kuu ya mapambano dhidi ya rushwa na maovu mengine katika jamii.
iv)
Uwazi na uwajibikaji
ACT Tanzania inaamini katika uwazi kwenye
mambo yote ya kijamii na kitaifa. Hivyo basi viongozi na wanachama wa
ACT-Tanzania wana wajibu wa kupigania uwazi katika mambo yote wanayofanya kwa
ajili ya umma. Sambamba na uwazi, ACT- Tanzania inaamini kwamba kila mwananchi
na kiongozi mwenye dhamana katika umma ana wajibu katika jamii na Taifa kwa
ujumla na ni jukumu lake kutekeleza wajibu huo bila kinyongo. Aidha, mwanachama
na kiongozi atokanaye na ACT Tanzania anapaswa kuwajibika kwa maneno na matendo
yake katika utumishi au nje ya utumishi wa chama au taasisi yeyote ya umma. ACT
Tanzania inaamini kwamba bidii katika kazi ndiyo njia pekee ya kujipatia
maendeleo.. Hivyo basi wajibu mkuu wa
mwanachama wa ACT Tanzania utakuwa ni: BIDII KATIKA KAZI.
v)
Demokrasia ya Kweli
ACT-Tanzania
inaamini demokrasia ndiyo msingi wa kujenga fikra pevu na kueneza uhuru wa mtu,
jamii na Taifa kwa ujumla. Hivyo basi, viongozi na wanachama wa ACT-Tanzania
watapigania uwepo wa demokrasia ya kweli katika kila ngazi, ndani na nje ya
chama. Kila jambo lenye maslahi mapana katika chama na katika umma litaamuliwa
kwa njia ya kidemokrasia ya moja kwa moja au kupitia kwa wawakilishi
waliochaguliwa.
4.
Taarifa ya Kazi na mipango ya mbele
ACT Tanzania imekwisha kukamilisha
rasimu ya awali ya Katiba ambaye iliwezesha kupata usajili wa muda
·
Zoezi la kuandikisha wanachama katika
mikoa kwa ajili ya kuomba usajili wa kudumu kwa mujibu wa sheria
limekwishakamilika. Tumewapata wanachama katika mikoa yote ya Tanzania Bara na
Zanzibar. Hata hivyo, tumechagua mikoa kumi ambayo tungependa msajili akahakiki
kama sheria inavyotaka.
Baada ya kukamilisha zoezi la
kuandikisha wanachama, wiki hii kabla ya Ijumaa tutapeleka fomu na mahitaji
mengine husika kwa Msajili wa vyama ili aweze kupanga ratiba ya zoezi la
uhakiki.
Mara baada ya msajili kutoa usajili wa
kudumu kwa muda atakaopanga, tutafanya uchaguzi wa kwanza mkuu
Kama itampendeza msajili akatupatia
usajili wa kudumu mapema, tunatarajia kushiriki kwa nguvu zote katika chaguzi
zote ndogo zitakazojitokeza, uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu
mwakani.
5.
Shukrani
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru
waratibu wote wa zoezi zima la uandikishaji wanachama waliojitolea kwenye mikoa
na wilaya mbalimbali katika kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa kwa wakati uliopangwa.
Natoa wito kwa wanachama na wapenzi wa
chama popote walipo waendelee kukichangia chama kwa nguvu zao, muda wao,
taaluma zao na kwa kila hali kadri uwezo unavyomruhsu kila moja wetu.
Nawashukuru sana wataalam na watafiti wetu
mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea kutumia utaalam wao kutushauri katika
maeneo mbalimbali ya utafiti, uongozi, sera, raslimali, usimamizi wa fedha,
mawasiliano, sheria, sayansi ya siasa, na kadhalika.
6.
Wito kwa wanachama na watanzania
Tunatoa wito kwa kila mwanachama, mfuasi na mpenzi
wa ACT-Tanzania popote walipo nchini kuhakikisha kwamba:
-wanazingatia misingi ya chama
iliyoanishwa hapo juu katika shughuli zao zote. Wakukumbuke kila mara kwamba lengo
kuu la chama hiki ni kupigania na kusimamia mabadiliko na uwazi katika
kila ngazi. Tungependa kila shughuli ya chama iwe shirikishi na wazi kwa
wanachama na wananchi kwa ujumla.
-anafanya kazi kwa bidii katika kukijenga
chama na kushiriki maendeleo katika jamii aliyomo, akizingatia kwamba chama
hiki kinaamini kwamba bidii katika kazi ndiyo njia pekee ya kujipatia maendeleo
kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Hivyo, kila mwanachama ahakikishe
anatoa mchango wake katika kukijenga chama na kuleta maendeleo katika jamii
husika aliyomo.
Tunawakaribisha watanzania wote popote
walipo na wanaoamini katika misingi tuliyoainisha hapo juu kujiunga na ACT
Tanzania. Kila mtanzania anayejiunga na chama hiki akumbuke kuchukua wajibu wake
katika kukijenga chama popote pale alipo. Na akumbuke wajibu mkuu kwa mujibu wa
chama hiki kuwa ni: BIDII KATIKA KAZI.
Mungu
ibariki Tanzania, Mungu ibariki ACT-Tanzania, ahsanteni kwa kunisikiliza!
Kadawi
Lucas Limbu,
Mwenyekiti
wa Taifa
0 comments:
Post a Comment