MTOTO WA MIAKA 13 ANUSURIKA KUCHINJWA NA BABA YAKE MZAZI


Mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Majengo, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga amelazwa katika Hospitali ya wilaya baada ya kunusurika kifo kutokana na jaribio la kuchinjwa na baba yake mzazi. 
 
Tukio hilo limekuja siku 10 baada ya mtu mmoja, Ustadh Mohamed Kurangwa (36), kumuua mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nzasa, Jamal Salum (12) kisha naye kuuawa, Mbagala, Dar es Salaam.
 
Kurangwa alimuua Jamal nyumbani kwake Mbagala Charambe Mianzini kwa kumchinja na kuweka kichwa cha marehemu kwenye miguu ya mtoto huyo, kisha kuupeleka mwili wake choo cha nyumba anayoishi muuaji. Muuaji huyo alizoa damu na kuijaza kwenye ndoo kisha kuiweka pembeni ya nyumba yake kabla ya kuingia chumbani kwake, kujifungia na kusoma Koran.

 Katika tukio la Kahama, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Joseph Fwoma alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Said Siraji (13) na alifikishwa hospitalini hapo jana alfajiri baada ya kuokotwa na wasamaria mwema akivuja damu shingoni.
 
Dk Fwoma alisema baada ya kufikishwa hospitalini, madaktari walimfanyia upasuaji na kumshona sehemu ya koromeo aliyokatwa na hadi jana alasiri hali yakeilikuwa inaendelea vizuri baada ya kuongezwa damu.
 
Mama mzazi wa mtoto huyo, Mariamu Idd (35) alisema mwanaye alichukuliwa na baba yake mzazi, Siraji Salvatory (45) juzi na kwenda naye nyumbani kwake Mtaa wa Majengo kwa kuwa walitengana siku nyingi.
 
Hata hivyo, jana asubuhi alipigiwa simu kuelezwa taarifa za mtoto wake kunusurika kuchinjwa na baba yake mzazi ambaye baada ya tukio hilo alijisalimisha polisi anakoshikiliwa hadi sasa.
 
Idd alisema mzazi huyo mwenziwe alikuwa akimchukua mara kwa mara na kwenda naye nyumbani kwake Malunga na baadaye kumrudisha akidai kuchoshwa na huduma za matibabu kutokana na mtoto huyo kuwa na matatizo ya kiafya mara kwa mara.
 
Polisi wilayani Kahama wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa wanafanya uchunguzi na wakati wowote watamfikisha mahakamani baba mzazi wa mtoto huyo

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini