TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU BARAZA LA MAASKOFU WA KIPENTEKOSTE TANZANIA (PENTECOSTAL COUNCIL OF TANZANIA) KUTOKUWA NA UWALIKILISHI KATIKA BUNGE MAALUM LA KATIBA
1. Uteuzi
wa Wajumbe wa Bunge la Katiba unafanywa kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura, 83 (The Constitutional Review Act, Cap 83).
Sheria hii inaweka mamlaka ya uteuzi, masharti, taratibu, vigezo na
mambo mengine yote yanayopaswa kuzingatiwa katika uteuzi wa Wajumbe wa
Bunge la Katiba. Kwa mujibu wa Kifungu cha 22 (2A) na (2B) vigezo hivi
vinajumuisha umri, jinsia, uzoefu, sifa na mahali anapotoka mjumbe
husika.
2, Sheria hii imeainisha aina tatu za Wajumbe wa Bunge la Katiba kama ifuatavyo:
- Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
- Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar; na
- Wajumbe 201 kwa mujibu wa Kifungu Na. 22(1c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inaonyesha makundi mbalimbali 10 yanayohusika.
3. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, wajumbe 201 wanatakiwa kuteuliwa kutoka
Taasisi zisizokuwa za Kiserikali (20)
Taasisi za Kidini (20)
Vyama vyote vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu (42);
Taasisi za Elimu (20);
Watu wenye Ulemavu (20);
Vyama vya Wafanyakazi (19);
Vyama vinavyowakilisha Wafugaji (10);
Vyama vinavyowakilisha wavuvi (10);
Vyama vya Wakulima (20); na
Vikundi vya Watu wenye Malengo yanayofanana (20).
Mchakato
wa uteuzi ulianza kwa kutoa Tangazo la Mwaliko katika Gazeti la
Serikali, Tangazo la Serikali Na. 443 la tarehe 13 Desemba, 2013.
Tangazo hilo lilitolewa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza ili
kuyaalika makundi yaliyotajwa kisheria kuwasilisha mapendekezo ya majina
kwa ajili ya uteuzi katika Bunge Maalum la Katiba. Aidha, Tangazo hilo
lilitangazwa pia katika magazeti mbalimbali yanayosomwa hapa nchini.
Pamoja na mambo mengine, Tangazo hilo lilitamka ukomo wa muda wa taasisi
na makundi kuwasilisha mapendekezo ya majina ya wajumbe kuwa ni tarehe
02 Januari 2014.
Mapendekezo
hayo yalitakiwa kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au kwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar. Mapendekezo hayo yalitakiwa kuwasilishwa kwa njia
ya barua ya posta au barua inayoletwa kwa mkono. Sheria haikutoa njia
nyingine ya kuwasilisha mapendekezo. Ninafahamu, wengine wangeweza
kutumia barua pepe au hata ujumbe mfupi wa maneno. Sheria haisemi hivyo!
Kufuatia
mwaliko huo, taasisi 554 kutoka Tanzania Bara na 178 kutoka Zanzibar
ziliwasilisha mapendekezo yao. Mapendekezo hayo yalijumuisha majina
2,762 kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar mapendekezo
hayo yalihusisha watu 874. Hivyo basi, taasisi na makundi mbalimbali
yalipendekeza jumla ya majina 3,636. Aidha, watu 118 walijipendekeza
wenyewe kinyume na matakwa ya kisheria na kufanya idadi ya majina
yaliyopendekezwa kuwa 3,754.
Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba imeweka masharti katika uteuzi wa wajumbe 201 wa
Bunge Maalum la Katiba. Masharti hayo, ni pamoja na wajumbe wasiopungua
theluthi moja wanatakiwa kutoka Zanzibar na theluthi mbili kutoka
Tanzania Bara. Kwa sababu hiyo, katika wajumbe 201, wajumbe 67
wanatakiwa kutoka Zanzibar na wajumbe 134 wanatakiwa kutoka Tanzania
Bara. Aidha, uteuzi huo unatakiwa kuzingatia idadi ya wajumbe kutoka
katika kila kundi kama ilivyoainishwa kisheria. Vilevile, mgawanyo wa
wajumbe wanawake na wanaume unatakiwa uwe nusu kwa nusu. Pamoja na hayo,
wajumbe hao wawakilishe sura ya wananchi wa Tanzania kwa ufuasi wa
vyama vya siasa, dini, umri, na maeneo wanayotoka.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar walikamilisha uteuzi wa
wajumbe 201 na majina ya walioteuliwa yalitangazwa tarehe 7 Februari
2014. Majina hayo yalitangazwa kupitia taarifa kwa vyombo vya habari na
pia Gazeti la Serikali kwa Tangazo la Serikali Na. 29 la tarehe 7
Februari 2014.
BARAZA LA MAASKOFU WA KIPENTEKOSTE TANZANIA
Tarehe 11
Februari 2014, Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania lilitoa
taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu uteuzi wa Wabunge wa Bunge Maalum
la Katiba. Baraza liliomba vyombo vya habari lifikishe masikitiko ya
Baraza kwa viongozi na waamini wa Kipentekoste wote na jamii ya wapenda
haki hapa nchini, kutokana na kitendo cha Serikali wanayoiheshimu,
wanayoipenda na kuiombea, kwa kulibagua na kulitenga Baraza lisihusike
na Bunge Maalum la Katiba.
Katika
Taarifa yake kwa vyombo vya habari, Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste
Tanzania limeeleza kuwa kwa …”utaratibu tuliojiwekea katika utawala wa
Baraza letu, hakuna Kanisa moja, mchungaji binafsi, mwamini, anaweza
kujitwalia heshima, kuchukuliwa au kupewa haki na chombo chochote cha
Serikali katika nchi yetu kwa nia ya kuwakilisha wapentekoste, bila
kupata idhini toka kikao halali cha Kamati Kuu ya Utendaji ya
PCT-Taifa”.
Kwa kuzingatia utaratibu huu
“Kamati Kuu ya Utendaji ya PCT-Taifa katika kikao chake cha tarehe
5/12/2013 ilipendekeza kwa Mheshimiwa Rais majina ya wajumbe wake
iliowaona kuwa wanafaa kuchaguliwa katika Bunge Maalum la Katiba, lakini
cha kusikitisha kati ya hao hakuna jina la mjumbe hata mmoja ambaye
alichaguliwa na Mheshimiwa Rais katika Bunge Maalum la Katiba”.
Taarifa
hiyo imeeleza pia, “… Serikali imeona hatufai na hatuna sifa za kuweza
kuchaguliwa katika Bunge Maalum la Katiba, na badala yake ikaamua kuteua
majina ya wajumbe toka katika taasisi nyingine za kidini zenye hadhi
kama yetu za Waislamu, Wakatoliki, Waprotestanti na Wajumbe wengine
binafsi kwa Tanzania Bara na Visiwani na kuwaacha Wapentekoste…”
UFAFANUZI WA SERIKALI
Kwanza
kabisa, napenda kuwahakikishia watanzania na hasa wale waliolengwa na
taarifa ya Baraza, kwamba Serikali haikuupuzia kundi lolote
lililoanishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuwasilisha
mapendekezo ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Serikali inaliheshimu
Baraza na tunalishukuru sana katika juhudi inazozifanya kwa pamoja na
Serikali katika kuwaendeleza wananchi wa Tanzania.
Kutokana
na umuhimu wa makundi mbalimbali, jumla ya makundi 850 yaliwasilisha
mapendekezo ya majina 3,636. Katika makundi haya 850, kulikuwa na
mapendekezo kutoka taasisi au makundi ya kidini 72 ambayo yalipendekeza
jumla ya majina 429. Kwa upande wa Tanzania Bara, taasisi za kidini 55
ziliwasilisha mapendekezo yenye jumla ya majina 344. Aidha, Serikali
ilipokea mapendekezo 118 kutoka kwa waliojipendekeza wenyewe! Hivyo,
siyo kweli kuwa Serikali ilipuuza mapendekezo kutoka kundi fulani ikiwa
ni pamoja na Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania. Serikali hii
ni kwa ajili ya watu na makundi yote. Aidha, Katiba yetu haibagui watu
au makundi ya watu kwa lengo la kuwanyima au kuwakosesha haki.
Kufuatia
taarifa ya Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania kwa vyombo vya
habari kuwa mapendekezo yao yamepuuzwa, kwa kuanzia Serikali imefuatilia
kama kweli Baraza hilo liliwasilisha mapendekezo. Kwa kuwa mapendekezo
yote yaliyowasilishwa yaliwekwa katika kanzi data ya msingi (primary
data base) kwa ajili ya uchambuzi, utafutaji kwa kutumia kompyuta
(computer search or find) ulifanywa ili kubaini kama kulikuwa na
mapendekezo kutoka Baraza kati ya mapendekezo 850 yaliyowasilishwa.
Kwa kuwa
hakukuwa na taarifa za majina ya waliopendekezwa, jina la taasisi na
majina ya maaskofu watano (5) walioshiriki katika utoaji taarifa kwa
vyombo vya habari yalitumika katika kubaini kama wao pia walikuwa
miongoni mwa waliopendekezwa. Utafutaji wa huu
haukubaini kuwa Baraza ilikuwa moja ya taasisi zilizowasilisha maombi.
Aidha, hapakuwa na jina hata moja la viongozi wa Baraza walioitisha
vyombo vya habari kutoa taarifa.
Pamoja na
kwamba haikutarajiwa kuwa viongozi wa taasisi hii kujipendekeza
wenyewe, na hivyo kuwa miongoni mwa watu 118 waliojipendekeza wenyewe,
juhudi za Serikali zilijielekeza kutafuta endapo kulikuwa na mapendekezo
kundi hili. Hata hivyo, utafutaji haukubaini majina ya viongozi hawa
kuwepo katika orodha hiyo.
Kulikuwa
na uwezekano pia, Baraza liliwasilisha mapendekezo ambayo yalifika kwa
Katibu Mkuu Kiongozi nje ya muda uliopangwa kisheria wa tarehe 2 Januari
2014. Uchambuzi wa mapendekezo 52 ambayo yaliwasilishwa nje ya muda
haukubaini kuwepo kwa mapendekezo kutoka Baraza la Maaskofu wa
Kipentekoste Tanzania.
Hivyo,
juhudi za Serikali katika kufuatilia uwepo wa mapendekezo kutoka Baraza
la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania hazikuweza kuthibitisha kuwa Baraza
lilituma mapendekezo yake kama ilivyokuwa imeagizwa na Sheria ya
mabadiliko ya Katiba!
UWAKILISHI WA MADHEHEBU YANAYOUNDA BARAZA LA MAASKOFU WA KIPENTEKOSTE TANZANIA
Kwa
kufahamu umuhimu wa makundi mbalimbali ya kidini ikiwa ni pamoja na
Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania unaoundwa na Maaskofu Wakuu
wa madhehebu ya kipentekoste yapatayo 75, uteuzi wa wajumbe wa Bunge
Maalum la Katiba ulihakikisha kuwa makundi ya kidini yanawakilishwa
ipasavyo.
Mgawanyo
wa idadi ya wajumbe 20 kutokana na makundi ya kidini baina ya Tanzania
Bara na Zanzibar kwa kuzingatia uwiano wa moja ya tatu ya wajumbe kutoka
Zanzibar ulimaanisha kuwa katika kundi hili, wajumbe 7 wangekuwa
wanatoka Zanzibar na wajumbe 13 wangekuwa wanatoka Tanzania Bara. Uteuzi
wa wajumbe katika kundi hili umezingatia kigezo hiki.
Kufuatia
uteuzi uliofanywa tarehe 7 Februari 2014, uchambuzi wa majina ya wajumbe
wa Bunge Maalum la Katiba umebaini kuwa kati ya wajumbe 13 kutoka
taasisi za kidini wa Tanzania Bara walioteuliwa, mjumbe mmoja (1)
aitwaye Bibi Respa Miguma Adam ameteuliwa kutoka Evangelistic Assemblies
of God Tanzania (EAGT), Patmos Vision, Kigamboni Church. Evangelistic
Assemblies of God Tanzania ni moja ya madhehebu ambayo maaskofu wake
wakuu wanaunda Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania.
Hivyo,
tamko la Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste kuwa wanabaguliwa halina
ukweli kwa kuwa uchunguzi tulioufanya haujathibitisha kuwa Baraza
lilileta mapendekezo. Ni vyema Baraza likafanyia kazi kwa nini kama
kulikuwa na mapendekezo, hayakufikishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi (Dar es
Salaam) au Katibu Mkuu Kiongozi (Zanzibar). Ninaamini kabisa kama
mapendekezo hayo yangekuwa yamewasilishwa, Mhe. Rais angechagua
mwakilishi kutokana na mapendekezo hayo.
HITIMISHO
Uteuzi wa
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba uliofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mhe. Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar tarehe 7 Februari 2014, kwa
namna yoyote ile haukuwa na nia ya kulibagua Baraza la Maaskofu wa
Kipentekoste Tanzania.
Kuna kila
sababu ya kuamini kuwa mapendekezo ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
kutoka Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania hayakuwasilishwa kwa
Katibu Mkuu Kiongozi kama sheria ilivyohitaji.
Pamoja na
kuwa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania hawakuweza kuwasilisha
mapendekezo yao kama ilivyotakiwa, tunaamini kuwa Baraza, kama ilivyo
kwa wananchi wote, litawakilishwa vyema na wajumbe walioteuliwa ambao
wanajumuisha mjumbe aliyeteuliwa kutoka moja ya madhehebu yanayounda
Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Februari 2014
---

0 comments:
Post a Comment