Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tatu kwa ufaulu kitaifa katika Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne wa 2013, jana alipoteza fahamu kwa muda baada ya kupata matokeo hayo.
Mwanafunzi huyo, Joyceline Marealle wa Shule ya
Sekondari Canossa ya Dar es Salaam, alipatwa na mkasa huo muda mfupi
baada ya mwandishi wa gazeti hili kumpigia simu na kumweleza matokeo
hayo.
Baada ya kupigiwa simu yake ya mkononi
iliyopokelewa na mama yake mzazi (Caroline Munuo), ambaye alisema mtoto
wake hajapata taarifa hiyo na kumtaka mwandishi aitoe mwenyewe kwa binti
huyo kisha kumpa simu hiyo Joyceline.
Baada ya binti huyo kupewa simu na kuanza
mazungumzo na mwandishi alisema: “Naomba usiniambie! Ni kitu kikubwa
Mungu amenifanyia.”
Joyceline aliyesikika akitamka maneno hayo huku
akilia ghafla sauti yake ilikatika na kukaa kimya kwa sekunde kadhaa,
kabla ya mama yake kuchukua simu hiyo, ambapo alieleza kuwa binti yake
anaishiwa nguvu.
“Naomba umpigie simu baadaye ameishiwa nguvu anataka kuanguka,” alisema mama huyo wa Joyceline.
Mama yake alisema alitegemea matokeo hayo kwa
sababu binti yake na mwenzake ambao ni pacha wamekuwa wakifanya vyema
kwa kushika nafasi mbili za kwanza darasani.
Naye mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa, Robina Nicholaus wa Sekondari ya Wasichana Marian ya Pwani, alisema:
“Mimi ni wa kwanza na wa mwisho kwenye familia
yetu, pia nimekuwa kwa kwanza kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne,
namshukuru Mungu.”
Aliongeza: “Nilitarajia kufaulu, lakini siyo kuwa
mwanafunzi wa kwanza. Mungu amenisaidia kuelekea kutimiza ndoto yangu ya
kuwa daktari wa watoto.”
Mama mzazi wa Robina, Pili Mogasa alisema
anamshukuru Mungu kwa kumsaidia binti yake kufaulu na kuongoza kitaifa
na kwamba hayo ni majibu ya maombi yake.
Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya nne kutoka Shule
ya Sekondari ya Wasichana ya Marian, Sarafina Mariki, alisema alitarajia
kufaulu huku malengo yake yakiwa kuwa miongoni mwa wanafunzi watano
bora kitaifa.
“Ndoto zangu zimetimia nilitaka kuwa kati ya wanafunzi wa kwanza hadi watano bora, namshukuru Mungu nimefanikiwa,” alisema.
Baba mzazi wa Sarafina, Wilfred Mariki akizungumza
kwa simu kutoka Kigoma alisema anafuraha kubwa kiasi kwamba anajisikia
kushiba siku nzima.
“Furaha niliyonayo hata tusipokula chakula leo
sawa,” alisema Mariki huku mama mzazi wa Sarafina, Jane Mariki akisema
binti yao alikuwa na tabia ya kuamka usiku kujisomea tangu akiwa shule
ya msingi.
Mwanafunzi Janeth Urassa akiyeibuka namba tisa,
ambaye anaishi Tanga alisema hakutarajia kuwa miongoni mwa kundi la
wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa, lakini matokeo hayo yanamwezesha
kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari wa moyo.
>>Kwa hisani ya Mwananchi.
>>Kwa hisani ya Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment