MPEKUZI: PADRI WA KANISA KATOLIKI ALIYEMZALISHA MUUMINI WAKE NA KISHA KUMTELEKEZA AKUBALI KULIPA SH. 580, 000 IKIWA NI GHARAMA ZA MATUNZO YA MTOTO HUYO



KESI iliyokuwa ikimkabili Padri Deogratius Makuri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Singida kushindwa kutoa fedha za matunzo kwa mwanawe, jana ilifikia ukingoni baada ya mlalamikiwa kuamua kulipa jumla ya Sh 580,000 taslimu ikiwa ni gharama za matunzo, matibabu na mavazi kwa ajili ya mtoto huyo.
 
Kiasi hicho cha fedha kilikabidhiwa kwa mlalamikaji Maria Boniphace na dadake Padre ajulikanaye kwa jina la Bahati Michael mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Utemini mjini Singida, Ferdinand Njau.
 
Awali Hakimu Njau aliionesha  barua kutoka kwa Padri Makuri ambapo alisema hawezi kufika mahakamani hapo kutokana na kile alichodai ni sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.
 
Katika barua hiyo, Padri Makuri amekiri kuwa jukumu la kumtunza mtoto huyo ni lake na kwamba kutokana na sababu hiyo muhimu ameamua kutuma mtu alete fedha ya matunzo kwa mtoto wake.
 
Kati ya fedha aliyoleta mahakamani hapo, alisema kuwa Sh 480,000 ni matunzo kwa miezi sita kuanzia Des 10, 2013 hadi Juni 10, 2014 ikiwa ni Sh 80,000 kila mwezi ambapo Sh 100,000 ni kwa ajili ya matibabu na gharama ya mavazi kwa mtoto huyo.
 
Hakimu Njau amemtaka mlalamikiwa kuleta kiasi hicho hicho tena hapo ifikapo Juni 10, mwaka huu vinginevyo kesi itafufuliwa. “Ilichokuwa inataka Mahakama hii ni fedha za matunzo kwa mtoto huyu, basi .... hilo sasa limefanyika.
 
"Sioni sababu ya kuendelea na shauri hili labda hapo mlalamikiwa atakaposhindwa kuheshimu amri ya Mahakama.” alisema Hakimu Njau aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo.
 
Padri Makuri, ambaye alikuwa Katibu wa Askofu Jimbo Katoliki Singida kabla ya kuingia kwenye kashfa hii, anatuhumiwa kushindwa kutunza mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minane (jina limehifadhiwa) aliyezaa na Maria Boniphace (26), mkazi wa eneo la Mitunduruni mjini Singida ambaye anadai alikuwa mfanyakazi jimboni hapo.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini