Kila Mtanzania bila kujali kama ni mtoto, mzee au mfanyakazi anadaiwa Sh. 600,000 miongoni mwa watu milioni 45 raia wote wa Tanzania.
Hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa deni la Taifa kufikia Dola za
Marekani bilioni 17.10 (Sh. trilioni 27.04 hadi kufikia Desemba mwaka
jana.
Kwa mtumishi wa serikali anayelipwa kima cha chini cha Sh. 150,000 kwa
mwezi atatakiwa kulipa deni kwa miezi minne mfululizo bila kubaki na
chochote.
Deni hilo ni bajeti ya serikali ya mwaka mmoja na nusu kwa mujibu wa bajeti ya mwaka 2013/14 ya Sh. trilioni 17.7.
Kati ya fedha hizo, Dola bilioni 12.79 (Sh. trilioni 20.23) ni deni la nje na la ndani ni Sh. trilioni 6.81.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, jijini Dar es
Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea utekelezaji wa
majukumu ya wizara hiyo.
Hata hivyo, alisema pamoja na kuongezeka kwa deni hilo, serikali
itaendelea kukopa kwa sababu bado ina sifa za kukopa kwa kuwa kiwango
cha deni ni asilimia 28 wakati ukomo wa kukopa ni asilimia 50.
Aliongeza kuwa itakopa fedha kwa masharti nafuu ambazo zitaelekezwa
kwenye miradi ya maendeleo ya miundombinu ambayo aliitaja kuwa ni
barabara, reli, bandari, mkongo wa Taifa, bomba la gesi, viwanja vya
ndege Zanzibar na Songwe.
Waziri Mkuya alifafanua kuwa sababu za kuongezeka kwa deni ni mikopo
iliyopokelewa na serikali ambayo muda wake wa kulipa haujafika kutoka
vyanzo vya masharti nafuu na ya kibiashara na malimbikizo ya deni la nje
kiasi cha dola za Marekani milioni 801.7 kwenye nchi zisizo wanachama
wa jumuiya ya wahisani.
Aliongeza kuwa serikali itajadiliana na nchi hizo kuhusu msamaha wa kufutiwa deni hilo.
Alisema Serikali inatoa kipaumbele kwa miradi ya ubia kati ya serikali
na sekta binafsi ili kuiwezesha kuchangia maendeleo ya uchumi na
kuipunguzia serikali mzigo wa madeni.
Alisema Septemba mwaka jana serikali kwa kushirikiana na taasisi za
kimataifa ilifanya thathmini kuangalia uhimilivu wa deni la taifa kwa
kutumia vigezo vilivyowekwa na kutambuliwa kimataifa na kwamba
ilionyesha deni ni himilivu kwa sababu viashiria vyote bado viko chini
ya ukomo unaotakiwa.
MATUMIZI YA EFD
Akizungumzia matumizi ya mashine za kielektroniki EFD, alisema
wataendelea kuyazitolea ufafanuzi na kuyasimamia vema kwa madhumuni ya
kukusanya kodi kwa ufanisi zaidi ili kuongeza pato la taifa na kupunguza
ukwepaji kodi.
Alisema serikali itaendelea kutoa elimu kupitia Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kwa wafanyabiashara kwa kuwa huo ndiyo msimamo wa
serikali. Alifafanua kuwa serikali iliwapa uhuru wafanyabiashara
wanaolalamikia mashine hizo kuunda kamati na kwenda kutembelea nchi za
China na Bulgaria zinapotengenezwa na kuangalia uhalisia wa bei, lakini
walikataa.
Kuhusu ukuaji wa uchumi, Mkuya alisema umekua kwa kiwango kikubwa na
unaendelea kuimarika kwa wastani na kwamba pato la taifa lilikuwa kwa
asilimia saba kwa kipindi cha miezi tisa ya mwanzo wa mwaka 2013.
MFUMUKO WA BEI
Kwa upande wa mfumuko wa bei, alisema umeendelea kushuka hadi asilimia
5.6 Desemba mwaka jana kulinganisha na asilimia 19.8 mwaka 2012. Alisema
kupungua kwake kulitokana na sera thabiti za fedha na kibajeti pamoja
na kuimarika kwa uzalishaji na usambazaji wa chakula.
Alisema matumizi ya fedha za kigeni katika mzunguko wa uchumi Mtanzania
asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote nchini kwa fedha hizo
isipokuwa sehemu za utalii na ada za shule za kimataifa.
Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia vyema suala hilo ikiwamo kuwachukulia hatua wanaokiuka utaratibu huo.
SARAFU MOJA EAC
Akizungumzia matumizi ya sarafu moja kwa nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), Mkuya alisema wanaendelea na mchakato na watalipeleka
bungeni kwa majadiliano zaidi kabla ya maamuzi.
Akizungumzia Bunge la Bajeti, alisema licha ya kufanyika kwa Bunge la
Katiba, wanatarajiwa kuwa bajeti itawasilishwa, kupitishwa na kuanza
kutumika Julai Mosi, mwaka huu, lakini alisema kama kutakuwapo na
viashiria, serikali itatoa taarifa.
Alipoulizwa kuhusu baadhi ya wanasiasa wanaohoji uwezo na uzoefu wake wa
kusimamia wizara hiyo, alijibu kwa kifupi kuwa hataki maswali hayo
kwani ni historia na kwamba Rais Jakaya Kikwete amekwisha kumteua na
anaendelea kuchapa kazi.
Kuhusu madai ya baadhi ya watumishi wa serikali na watoa huduma
serikalini, alisema tatizo liko katika halmashauri kwa kuwa fedha
zinatumwa na kuwa kinachofanyika ni uzembe. Hata hivyo, Mkuya aliahidi
kwamba serikali itafuatilia.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment