MBOWE AMPONDA ZITTO KABWE NA KUMTABIRIA YAFUATAYO

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amemvaa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na kusema kamwe chama hicho hakiwezi kuvumilia usaliti wa aina yoyote.
 

Akizungumza mjini Mwanza  jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Malimbe, alisema kwa namna yoyote ile hawatamfumbia macho mtu yeyote anayekwenda kinyume cha katiba na taratibu za chama hicho.

Alisema Chadema ambayo imejengwa kwa damu za Watanzania haiwezi kukubali kuona mtu yeyote anatoboa ‘boti’ yake iendayo kasi katikati ya bahari wakati huu wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwakani.

Mbali na kumshukia Zitto pia amekirushia kombora Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kusema kinatumia mbinu chafu kutaka kuiua Chadema kabla ya mwaka 2015.

Alisema kamwe mbinu hizo hazitafanikiwa maana Chadema ipo kwa mpango wa Mungu.

Ingawa Mbowe hakumtaja Zitto kwa jina lakini hotuba hiyo ilionekana dhahiri kumlenga Zitto, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba waliovuliwa nyadhifa zao zote za uongozi ndani ya chama hicho hivi karibuni.

“Tumejenga chama makini, tumaini la Watanzania, kwa hiyo hatuwezi kumfumbia mtu au watu macho pale anapokwenda kinyume na misingi ya chama.

“Yaani mpo safarini ndani ya bahari au ziwa, halafu mnafika katikati mtu au watu wanaanza kubotoa boti yetu, hivi huyo mtu tutamuacha hivi hivi? Mkimuacha lazima mzame, kwa hiyo lazima huyo msaliti mumshughulikie,” alisema Mbowe.

Alisema chama hicho hakitishiki wala kubabaishwa na propaganda na njia pandikizi zinazofanywa kwa kuandamana na mabango kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema uliofikiwa hivi karibuni na kitaendelea na wembe ule ule wa kuwanyoa wasaliti ndani ya chama hicho.

Alisema yeye au Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, wapo tayari kuvuliwa nyadhifa zao ikiwa ni pamoja na kufukuzwa uanachama pale watakapobainika kuanza kuingiza hujuma kwa lengo la kutaka kukiua chama.

“Bahati mbaya Mbowe sinunuliki. Fedha sina na sina njaa lakini sinunuliki na nzuri zaidi Katibu wetu wa Chadema, Dk. Slaa, naye hanunuliki na CCM wanalijua hili,” alisema.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro alisema kuongoza chama kikubwa cha upinzani kama hicho ni kazi kubwa na haihitajiki majaribio na aliwaomba wanachama wenye mtazamo thabiti na chama hicho wajitokeze kugombea nafasi yoyote.

Kuhusu CCM na Serikali yake alisema imekuwa ikiwalisha upepo wananchi masikini kwa kuwadanganya na ndani ya Bunge Serikali imekuwa haiwaelezi uhalisia wa mambo wananchi wake badala yake inawahadaa kwa kutoa matamko ya kuwapumbaza wananchi.

Alisema chama hicho kimejizatiti vema katika safari ya kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu na safari ya kwenda Ikulu ipo pale pale.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini