NI jambo lililotoa mshtuko kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani ambapo Desemba 10, mwaka huu, walikuta mwili wa binadamu ukiwa ndani ya gari lililopinduka, pembeni mwa Barabara ya Kisarawe - Mwaneromango.
Mbali na mwili, ndani ya gari hilo aina ya Toyota RAV 4 (milango mitatu new model) lenye namba za usajili T 273 AKP kulikutwa bastola moja, risasi 85 na magazini mbili.
Utata ukaanzia hapo, polisi wa wilaya hiyo wakiongozwa na mkuu wao (aliomba jina lisitiriwe kwa sababu si msemaji) wakajiuliza ni nani mtu huyo ambaye alikuwa amefariki dunia? Kumbe alikuwa Suleiman Muhema (42), bilionea kijana mkazi wa jijini Dar es Salaam.
polisi waliuchukua mwili wake na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Wilaya mpaka ndugu walipokwenda kuuchukua kwa mazishi.
SULEIMAN MUHEMA NI NANI?
Suleiman Muhema ni mkazi wa jijini Dar, amejenga jumba la kifahari Kijitonyama ambako aliishi na mke wake, Zihji Mvungi (42).
Mpaka kifo chake alikuwa mfanyabiashara wa magari kutoka Japan akiyauza Dar, pia alikuwa na kampuni ya usafirishaji, sifa zote kwa pamoja zinamfanya aitwe bilionea.
MAISHA SIKU CHACHE KABLA YA KIFO
Habari zinadai kuwa, marehemu alikuwa ndani ya mgogoro wa kifedha na mtu ambaye hakutajwa jina lakini ni wa karibu naye.
Inadaiwa kuwa, mgogoro huo ni wa muda mrefu na ulikuwa ukisuluhishwa na Dawati la Jinsia, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar.
SIKU YA TUKIO
Siku ya tukio inadaiwa marehemu alikuwa Magomeni na watu (idadi yao haikujulikana). Baada ya hapo aliondoka kwenda kusikojulikana lakini baadaye alimpigia simu ndugu wa karibu na kumwambia kuwa yuko mahali (hakupataja) ametekwa na sauti anayoitoa inaweza kuwa ya mwisho kisha akakata simu.
MAELEZO YA POLISI SASA
Kwa mujibu wa chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi Wilaya ya Kisarawe, Desemba 10, mwaka huu, usiku wa saa nane, marehemu alionekana akiwa ndani ya gari jeusi umbali wa kilomita saba kutoka Kisarawe Mjini lakini aliondoka baada ya kuliona gari la ‘patroo’ ya polisi.
Chanzo hicho kikasema kuwa dakika chache mbele polisi waliokuwa katika shughuli za ulinzi usiku huo waliliona gari hilo likienda pembezoni mwa barabara na kupinduka.
“Tulilifuatilia, tukalikuta limepinduka, ndani ya gari tulimkuta mtu amekufa kwa kujipiga risasi kwani sehemu ya kidevuni na kwenye utosi kulikuwa na tundu la risasi,” kilisema chanzo hicho.
MAREHEMU ALIDHANIWA MHALIFU
Habari zinasema katika upekuzi wa awali ambapo polisi walimkuta marehemu akiwa na bastola, risasi 85 na magazini mbili walidhani alikuwa mhalifu aliyetaka kutekeleza uhalifu mahali ndani ya walaya hiyo.
NDUGU WA MAREHEMU WANA NENO
Kwa upande wao ndugu wa marehemu ambao waliomba majina yao yawekwe pembeni, walisema kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu kifo cha ndugu yao huyo kwa sababu hata kifo chake hawakielewielewi.
Akizungumza kwa hisia ya uchungu, ndugu mmoja alisema katika maisha ya jijini Dar, yeye ndiye baba wa marehemu lakini hakuna alichojua toka kifo hadi kuzikwa.
Alisema hata mazishi ya marehemu alishtukizwa kwamba anazikwa siku hiyo jambo lililompa wakati mgumu kufikiria.
“Sisi kama ndugu wa marehemu, tulipenda akazikwe nyumbani, Makete (Njombe), lakini ghafla tukaambiwa anazikwa hapahapa Dar tena siku hiyohiyo tuliyopewa taarifa,” alisema ndugu huyo.
MKE WA MAREHEMU NAYE
Kwa upande wake mke wa marehemu Zihji alipoulizwa na mapaparazi wetu juzi kuhusu sakata la kifo cha mumewe alijibu kuwa kila mtu anaweza kuongea jambo lolote.
Aliongeza kusema anachojua yeye ni kwamba kifo cha mumewe kilitokea kama ambavyo mtu mwingine angeweza kufa.
KAMANDA WA POLISI ANASEMAJE?
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, ACP Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa marehemu alikutwa akiwa na jeraha la risasi moja hali ambayo ilionesha alijipiga risasi mwenyewe pengine kutokana na mambo yaliyokuwa yakimsonga kichwani.
BILIONEA AZIKWA DAR
Marehemu Muhema alizikwa Desemba 11, mwaka huu kwenye Makaburi ya Sinza jijini Dar. Ameacha mke na watoto watatu wa kike. Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina.
MASWALI TATA
Kifo cha Muhema kina maswali tata mengi. Kwanza, kama kweli alipanga kujiua kwanini alikwenda mbali na Jiji la Dar es Salaam?
Pili, kwa nini damu ndani ya gari ilikuwa kidogo wakati uzoefu unaonesha kuwa, mtu anayepigwa risasi ndani ya gari huacha damu nyingi?
Tatu, ndugu mmoja wa marehemu alikiri kuwa, Muhema alinunua bastola mwaka huu ili kujilinda, sawa kabisa. Je, kwa nini akutwe na risasi nyingi kiasi hicho kama alikuwa anakwenda kufanya uhalifu?
Nne, ilidaiwa alimpigia simu ndugu mmoja akidai ametekwa na huenda asisikike tena. Polisi walikuta simu kwenye gari lake, kwa nini waseme alijipiga risasi mwenyewe?