SOMO SAHIHI LA KUPUNGUZA MAWAZO NA KUONGEZA FURAHA-2


MUELEZE HUJISIKII VIZURI
Ikibidi sema unaumwa. Mpenzi bora atapunguza maswali au baadhi ya vitu na kukuacha upumzike. Hiyo itakusaidia kuingiza hewa kichwani ambayo itakuongezea nafasi na mwisho kichwa kitakuwa chepesi.
Maneno ya hapa na pale ukiwa na msongo wa vitu kichwani, utaona kama ni vuvuzela zinapulizwa masikioni. Unapomuomba mwenzio akupe nafasi ya kupumzika kwa sababu hujisikii vizuri, itakusaidia kupunguza uzito wa kichwa.

ANGALIZO;
 Unapaswa kuwahi kujieleza kabla mwenzako hajaanza yake, kwa maana akisema yeye halafu wewe ndiye ufuate, atajua umeamua kumkwepa.

 
LALA USINGIZI Tafuta usingizi kisha utokomee kwenye njozi, ukiamka hutokuwa yule yule. Angalau kichwa kitakuwa kimepumua na uzito umepungua.

MUELEZE KINACHOKUSUMBUA
Ni tiba kwako endapo utafungua kinywa na kumueleza mwenzio kile ambacho kinakusumbua. Atajua kinachokusibu, kwa hiyo atajua jinsi ya kukuzoea kuliko kufika na kukaa kimya au kumjibu mkato au kufoka bila mpango.


CHAGUA KINACHOKUFURAHISHA, FANYA
Unapenda kungalia filamu au kingine chochote na unaamini ukikifanya kitakuondolea hasira, basi fanya ili kujiweka vizuri kisaikolojia mbele ya mwenzi wako. Kuna wale ambao hasira zao hutoweka baada ya kupanda kitandani, nalo si tatizo ilimradi kutibu hasira.

Angalizo ni kwamba kupanda kitandani kunahitaji uhuru wa hisia. Utazungumza vipi na mwenzi wako mpaka mkubaliane kupeana hiyo dawa? Muhimu ni kumueleza kinachokusibu, akikuhurumia, basi huo ndiyo uwe mwanzo wa kutii kiu.

UVUMILIVU
Yote ni muhimu lakini uvumilivu ni kitu cha msingi. Jifunze kusikiliza vitu bila kutoa majibu. Acha baadhi ya mambo yawe fahari ya masikio. Inawezekana umesikia na jibu unalo lakini unatakiwa uitambue hali uliyonayo, kwa hiyo endelea kunyamaza.

Ukiweza hili basi umefaulu mtihani mgumu na haitatokea ugombane na mwenzio kisa umeudhiwa kazini kwako au kwenye daladala.

HITIMISHO
Zingatia hayo ambayo nimekudokezea mwanzo mpaka mwisho. Hivyo ndivyo unavyoweza kuongeza furaha yako na kupunguza mawazo. Nakusisitiza kupiga vita msongo wa mawazo kwa sababu mara nyingi hupoteza njia. Mhusika hukosa mwanga wa kupata ufumbuzi.

Unapokosa ufumbuzi, itakusababishia kufanya uamuzi ambao siyo sahihi, hivyo kukuelekeza kwenye majuto ya baadaye. Hakuna sababu ya kujuta, shughulikia mambo yako kwa utaratibu. Makala haya ni dira yako katika kukupunguzia mawazo na kukuongezea furaha.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini