Wananchi wa kijiji cha Charangwa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, wamefunga barabara kuu ya kutokea Mbeya kuelekea mikoa ya kaskazini kama vile Mwanza, Tabora, Singida na Manyara kwa zaidi ya saa tano, wakipinga kitendo cha Serikali kumuuzia mwekezaji mlima wao ambao wamekuwa wakichimba dhahabu kwa miaka mingi bila ya kuwashirikisha.
Barabara hiyo ilifungwa jana kuanzia saa 11:00 alfajiri na kusababisha
usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo mpaka ilipofunguliwa saa
4:00 asubuhi na Mkuu wa wilaya hiyo, Deodatus Kinawiro.
Baada ya Kinawiro kushirikiana na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU), kufanikiwa kufungua barabara hiyo na kuruhusu magari kupita,
aliwaomba wananchi kukusanyika kwenye uwanja wa mpira kijijini hapo ili
kuzungumzia tatizo hilo kwa kina.
Wakiwa uwanjani hapo, wananchi hao walimweleza Mkuu huyo wa wilaya kuwa
sababu za wao kuchukua uamuzi wa kufunga barabara ni hatua ya Serikali
kuuza mlima wao wa dhahabu bila kuwashirikisha.
Askari wakidhibiti hali ya usalama eneo la mkutano
**
Askari wakidhibiti hali ya usalama eneo la mkutano
**
Mmoja wa wananchi hao, Samideo Hussein, alisema baada ya mwekezaji huyo
kuuziwa, alitaka kuanza shughuli zake bila hata ya uongozi wa kijiji
kujua na ndipo walipomzuia na kumtaka kwanza alete nyaraka zinazompa
uhalali wa kumiliki mlima huo.
Alisema mwekezaji huyo aliondoka, lakini baada ya siku chache alirejea
kinyemela na kuanza kuweka mawe (bicorn), kuzunguka eneo la mgodi na
ndipo walipoamua kumfukuza.
Alisema baada ya kumtimua mwekezaji huyo, alikwenda Polisi ambako
alifungua kesi ya kutishiwa kuuawa na jana usiku wa manane askari Polisi
walifika kijijini hapo na kuanza kuvunja milango ya nyumba za baadhi ya
wananchi na kuwakamata.
Kwa mujibu wa Hussein, kijana mmoja alifanikiwa kuwatoroka Polisi na
kukimbia akiwa na pingu mikononi na huyo ndiye aliyewaeleza wananchi
wengine juu ya uwApo wa askari kijijini hapo.
Alisema wananchi baada ya kupata taarifa, waligonga kengele ya kuashiria
hali ya hatari kijijini hapo, wakakusanyika na kuanza kuandamana, hali
iliyosababisha askari waliokuja usiku huo kuwaachia vijana waliowakamata
na kutimua mbio kabla ya wananchi kufikia uamuzi wa kufunga barabara
kwa lengo la kushinikiza mwenzao aliyekimbia na pingu afunguliwe pingu
hizo na kuachiwa huru na pia kupinga mlima wao kuuzwa.
“Kutokana na kitendo cha eneo letu la uchimbaji kuuzwa bila sisi
kushirikishwa, kisha askari wanaingia kijijini kinyemela bila uongozi wa
kijiji chetu kujua na sisi wanyonge tumeamua kufunga barabara ili
viongozi wetu wa juu watusikie, kwani tusingefanya hivyo hata wewe mkuu
wa wilaya leo usingekuja hapa,” alisema Hussein.
Mwananchi mwingine, Mwandamba Kosonga, alisema utaratibu wa Polisi
kuingia kijijini na kwenda kuwakamata watu moja kwa moja bila ya
kuujulisha uongozi wa kijiji, ni kosa kisheria na kuwa wao hawakubaliani
nao.
Alisema suala hilo limekuwa ni kero kwani mara kwa mara Polisi wamekuwa
wakiingia kijijini hapo na kukamata watu bila ya Serikali kujua, huku
vijana wote hapo kijijini wakijihusisha na ulinzi shirikishi kwa
kusaidia na Polisi.
“Hapa kijijini vijana wanao umoja wao wa ulinzi shirikishi, kuna uongozi
wa kijiji, lakini Polisi wamekuwa hawafuati taratibu wanaingia ovyo na
kukamata watu, sasa kama wanafanya hivyo hii serikali ya kijiji na
kikundi cha ulinzi shirikishi vina maana gani, suala la kupiga watu
kujichukulia sheria mkononi lisianzie kwa wananchi tu, Polisi nao
wasichukue sheria mkononi,” alisema Kosonga.
Aidha, wananchi hao kwa umoja wao walimweleza Mkuu wao wa wilaya kuwa
jambo hilo haliwezi kupata suluhu kama mwenzao aliyekimbia na pingu
hatafunguliwa pingu hiyo na kuachiwa huru.
Akizungumza na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kinawiro, aliwataka
kutoendelea na tabia ya kujichukulia sheria mikononi na badala yake
linapotokea jambo wajitahidi kufuata sheria kwa kuwatumia viongozi
kuanzia ngazi ya vitongoji hadi taifa.
Kinawiro aliagiza kuwa wakati mgogoro wa mlima huo wa dhahabu
ukishughulikiwa, kuanzia sasa hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kwenda
kwenye eneo hilo wala kufanya shughuli za aina yoyote mpaka suala hilo
litakapopatiwa ufumbuzi.
“Natoa tamko la Serikali kwamba, kuanzia sasa suala la mtu kujichukulia
sheria mkononi ni marufuku, sitaki kusikia tena mkifunga barabara na
kuanzia sasa hakuna mtu anayeruhusiwa kwenda kwenye mlima wenye mgogoro
mpaka suala hili litakapokuwa limeshughulikiwa na kupatiwa suluhu,”
alisema.
Naye Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Robert Mayala,
alisema hata kama wananchi hao wanayo madai ya msingi, wanapaswa kufuata
sheria kudai haki yao badala ya kuchukua sheria mkononi.
Mohammed Katembo akitokea mafichoni baada ya kuwakimbia Polisi
Mohammed Katembo akifunguliwa pingu na askari Polisi baada ya wananchi kutaka aachiwe huru bila ya masharti vinginevyo wangekata pingu
Hili ndilo eneo lenye mgogoro .Mwananchi akiendelea kuchimba licha ya mkuu wa wilaya kupiga marufuku
Sehemu ya mlima unaolalamikiwa kumilikiwa na mwekezaji
Mkuu wa wilaya ya Chunya Deotatus Kinawiro akipokea nyaraka toka kwa afisa mpelelezi wilaya ya Chunya
Mohammed Katembo akitokea mafichoni baada ya kuwakimbia Polisi
Mohammed Katembo akifunguliwa pingu na askari Polisi baada ya wananchi kutaka aachiwe huru bila ya masharti vinginevyo wangekata pingu
Hili ndilo eneo lenye mgogoro .Mwananchi akiendelea kuchimba licha ya mkuu wa wilaya kupiga marufuku
Sehemu ya mlima unaolalamikiwa kumilikiwa na mwekezaji
Mkuu wa wilaya ya Chunya Deotatus Kinawiro akipokea nyaraka toka kwa afisa mpelelezi wilaya ya Chunya
Moja ya nyaraka hizo
Wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya Chunya
0 comments:
Post a Comment