WAJUMBE WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA WAASWA KUTOKUWA WATUMWA WA VYAMA VYAO


WAJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba wameshauriwa kutokuwa watumwa wa kupokea maagizo ya vyama vyao vya siasa kwa hofu ya kupoteza madaraka, kwani wakifanya hivyo watakuwa hawatendei haki wananchi.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana na mfanyabiashara wa mjini Dodoma, Augustino Ndejembi alipokuwa akielezea jinsi mchakato mzima wa Bunge la Katiba unavyoendelea.
 
Alisema ikiwa wajumbe wa Bunge hilo wataamua kuingiza mapendekezo ya viongozi kutakuwa ni ndoto kupatikana kwa katiba itakayogusa maisha ya Watanzania.
 
“Ni muhimu wabunge kukataa kuwa watumwa wa kupokea mapendekezo kutoka kwa viongozi hao bali tunachotaka kila mmoja awakilishe mawazo yake mwenyewe hapo tunakuwa tumeipata katiba inayohitajika kwa hivi sasa,”alisema Ndejembi.
 
Ndejembi alisema kuwepo kwa wabunge hao bungeni kunatokana na matakwa ya wananchi na siyo kwa kuagizwa na viongozi wa siasa ambao wanataka waingize itikadi za vyama vyao.
 
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Gospel Catholic Tanzania, Daud Chidawali aliwataka wajumbe hao, kutonunuliwa na viongozi wa siasa na dini ili wapitishiwe miswada wanayopenda wao.
 
Alisema kwa kufanya hivyo nchi inaweza kuingia pabaya na kusababisha hata migogoro, inayoweza kuzaa vita kama nchi za jirani zilivyo kwa hivi sasa.
 
Chidawali alisema Watanzania wanahitaji kuipata katiba isiyofungamana na upande wowote ule, ambao utaonekana kama katiba hiyo ni ya kwao.
 
Katibu Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Dalai, Rashid Bura alisema wajumbe wa Bunge la Katiba, wakae wakijua wanayo dhima mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kazi waliyotumwa na wananchi na si vyama vyao.
 
Alisema wajumbe wameanza kujadili jambo la Muungano zaidi na serikali tatu, badala ya kujadili mambo ya msingi ambayo ni mengi ikiwemo, kufikiri wasomi watakwenda wapi wanapokosa ajira ili isije ikaleta machafuko katika nchi, maana palipo na wasomi wengi na hakuna ajira machafuko huwepo.
 
Alitaja mambo mengine muhimu yanayotakiwa kujadiliwa ni haki za msingi za wananchi, kama kupata haki katika Mahakama, Polisi na sehemu mbalimbali ambapo haki inatakiwa kutendeka.
 
“Pia kuna haki za msingi za wastaafu baada ya kumaliza utumishi wao wanatakiwa kuishi vipi tumeona mpaka sasa baadhi ya wastaafu hawajapata haki zao kwa miaka zaidi ya 20 hayo ni masuala ya msingi ya kujadili katika Katiba na si malumbano kama ilivyo sasa,” alisema.

>>Habari leo

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini