WAKATI Bunge Maalum la Katiba likisuasua katika kuunda kanuni za kuongoza wajumbe wake, taarifa zinaonesha katika muundo uliopo wa serikali mbili, mbali na kuimarisha umoja na mshikamano wa Taifa, pia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imekuwa ikinufaika nao kiuchumi.
Taarifa
hizo za kiuchumi, zinaungana na taarifa za kisiasa na kijamii
kusisitiza umuhimu wa muundo wa Muungano wa serikali mbili, tofauti na
wa serikali tatu uliopendekezwa na rasimu ya Katiba mpya,
zilizokwishatolewa na baadhi ya wasomi na viongozi mbalimbali katika
jamii.
Viongozi
hao, akiwemo Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycapy Kadinali Pengo na Profesa Bonaventura Rutinwa wa Shule
Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamebainisha kuwa
umoja na mshikamano wa Watanzania unalindwa vizuri na muundo wa
serikali mbili, kuliko itakavyokuwa na serikali tatu.
Mhadhiri
wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Hamphrey Moshi,
katika sura aliyoandika katika kitabu cha Katiba Bora Tanzania,
amebainisha kuwa katika muundo uliopo, SMZ imekuwa ikipata huduma za
mambo ya Muungano bila kulipia, huku baadhi ya madeni yake yakilipwa na
Serikali ya Muungano tofauti na itakavyokuwa katika muundo wa serikali
tatu.
“Kama
muundo huu (serikali tatu), utakubalika, SMZ lazima ijitegemee katika
kugharimia shughuli zake za kinchi na kwa kuwa Zanzibar itakuwa sawa na
Tanganyika, haitakuwa na maana Zanzibar kuacha kulipia ghama za Muungano
sawa na idadi yake ya watu,” amebainisha Profesa Moshi katika kitabu
hicho kilichochapishwa hivi karibuni.
Gharama za Muungano
Kwa
mujibu wa Profesa Moshi, tangu kuasisiwa kwa Muungano, takwimu
zinaonesha SMZ imechangia gharama za shughuli za Muungano mara tatu tu.
Mara
ya kwanza ilikuwa mwaka wa fedha 1964/1965, ambapo takwimu zinaonesha
kuwa gharama za mambo ya Muungano zilikuwa Sh milioni 107 na SMZ
ilichangia Sh milioni 10, sawa na asilimia tisa ya gharama za
uendeshaji.
Mwaka
wa fedha 1965/1966, takwimu hizo zinaonesha gharama za mambo ya
Muungano ziliongezeka na kuwa Sh milioni 153, na mchango wa SMZ
uliongezeka na kufikia Sh milioni 12 ingawa tafsiri yake ni kwamba
mchango huo ulipungua na kuwa asilimia nane ya gharama hizo.
Takwimu
za mwisho za mchango wa SMZ katika shughuli za Muungano, zimetajwa kuwa
ni za mwaka wa fedha 1966/1967, ambapo gharama zilikuwa Sh milioni 176
na mchango wake ulipungua zaidi na kuwa Sh milioni 8.1, sawa na asilimia
tano ya gharama hizo.
Profesa
Moshi amebainisha kuwa hakuna takwimu zaidi zinazoonesha mchango wa SMZ
katika shughuli za Muungano baada ya mwaka wa fedha 1966/1967, wakati
gharama hizo zikiongezeka mara dufu.
Kwa
mfano mwaka 2000 Bajeti ya mambo ya Muungano iliyotolewa na Serikali ya
Muungano, ambayo sasa inashutumiwa kuwa ni Serikali ya Tanganyika
iliyovaa koti la Muungano, imetajwa ilikuwa Sh bilioni 474 wakati mwaka
2006, mambo ya Muungano yalichukua Sh bilioni 556.1.
“Kwa
wastani kwa miaka mitano kati ya 2005 mpaka 2010, Tanzania Bara imekuwa
ikitenga asilimia 22 ya Bajeti yake kugharamia shughuli za Muungano.
Inaonesha
kuwa Zanzibar imeshindwa kutoa mchango wowote katika miaka hii mitano.
“Pamoja na Zanzibar kuonekana kushindwa kuchangia gharama za shughuli za
Muungano, jambo ambalo linapingana na Ibara ya 133 ya Katiba iliyopo,
hakuna ushahidi kwamba SMZ imewahi kuitwa kujieleza kwanini haitoi
mchango wake,” ameeleza Profesa Moshi.
Jaribio la Kurekebisha
Kwa
mujibu wa Profesa Moshi, mwaka 1977 Kamati ya Shelukindo, ilitakiwa
kupendekeza fomula ya haki na ya wazi ya mchango wa SMZ katika gharama
za uendeshaji wa shughuli za Muungano.
“Mapendekezo
yalikuwa Zanzibar ilipe asilimia 3.9 ya matumizi yote ya shughuli za
Muungano. Hata hivyo, inavyoonekana hili halijawahi kutekelezwa. “Mbali
na Kamati ya Shelukindo, mapendekezo kama hayo yalitolewa kwa mara
nyingine ili kutatua kero hiyo na Tume ya Nyalali (1992) na Tume ya
Kisanga (1998),” amefafanua Profesa Moshi.
Hisa za Zanzibar
BoT
Tofauti na ilivyo kwamba Zanzibar imekuwa ikishindwa kutoa mchango wake
katika gharama za Muungano, Serikali ya Muungano kupitia Benki Kuu
(BoT), imekuwa ikitoa gawiwo la hisa za Zanzibar kwa SMZ la asilimia 4.5
kila mwaka.
Hisa
hizo zinatokana na kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
ambayo Zanzibar na Tanzania Bara zilikuwa nchi wanachama na wanahisa
katika Bodi ya Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACB).
Baada
ya kuvunjika kwa Jumuiya, Zanzibar haikupata hisa zake asilimia 11.05,
zilizokuwa zikionesha umiliki wake katika EACB na kugeuka kuwa sehemu ya
kero za Muungano.
“Hata
hivyo mwaka 1994, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), lilishauri
Zanzibar ipate asilimia 4.5 ya gawiwo kutoka BoT,” ameeleza Profesa
Moshi.
Kiwango
hicho cha gawiwo kimekokotolewa kwa kuzingatia sehemu ambayo Zanzibar
inachangia katika uchumi wa Tanzania na idadi ya Watanzania, ambayo ni
wastani wa asilimia tatu.Profesa Moshi amebainisha kuwa tangu 1995, SMZ
imekuwa ikipata gawiwo hilo kutoka BoT.
Madeni
Profesa
Moshi ameeleza kuwa uwezo wa SMZ kukopa ni mdogo, kwa kuwa Waziri wa
Fedha katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ndiye mwenye mamlaka ya
kukopa kwa niaba ya serikali zote.
“Hii
maana yake ni kwamba SMZ, haina mamlaka ya kutafuta mkopo kwa ajili ya
matumizi yake na kama inataka mkopo, lazima iombe kupitia Serikali ya
Jamhuri ya Muungano. “Serikali ya Jamhuri ya Muungano baada ya kupokea
maombi ya Zanzibar, itaomba mkopo kutoka nje na ikifanikiwa, itatoa
sehemu ya mkopo huo iliyoombwa na Zanzibar na kuipa SMZ,” ameeleza
Profesa Moshi.
Ameeleza
kuwa kwa juu juu, inaonekana kuwa Zanzibar inaumizwa kiuchumi, lakini
uchambuzi wa ndani unaonesha namna SMZ inavyonufaika katika mfumo huo.
Yasiyolipika
Kwa
mujibu wa Profesa Moshi, kwa kuwa mikopo ya Zanzibar inadhaminiwa na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano, mpaka mwaka 2002 utaratibu ulikuwa SMZ
ikishindwa kulipa deni, linalipwa Serikali ya Muungano kwa niaba ya SMZ.
Kuanzia
mwaka wa fedha 2001/2002, Profesa Moshi amebainisha kuwa SMZ imekuwa
ikiruhusiwa kukopa kwa kuuza hati fungani kupitia BoT.
Hata
hivyo kwa mujibu wa Profesa Moshi, BoT ililazimika kuunda akaunti
maalumu, ili SMZ iliposhindwa kulipa deni, benki hiyo ilipe na kukata
katika gawiwo ambalo linapaswa kutolewa kwa SMZ.
Pamoja
na madeni hayo ya kiserikali, Zanzibar pia imetajwa kuwa na madeni
makubwa ya kibiashara, likiwemo la Shirika la Umeme (Tanesco) kwa
Shirika la Petroli Zanzibar (ZSFPC).
“Ingawa
ZSFPC imeandaa mpango wa kulipa deni lake kwa Tanesco kwa miaka 15
mpaka 2018/19, uzoefu wa nyuma unaonesha kuwa Serikali ya Muungano
huenda ndiyo itakayolipa deni hilo,” ameeleza Profesa Mushi.
Maoni CUF
Akizungumzia
uchambuzi huo wa Profesa Moshi, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar,
Julius Mtatiro, alisema uchambuzi huo si wa kweli na mfumo wa serikali
mbili unaonesha Tanganyika inajikomba kwa Zanzibar.
Alitoa
mfano wa Sekta ya Utalii, kwamba kungekuwa na muundo mzuri wa Muungano,
Zanzibar wangekuwa na ushirikiano na nchi za kimataifa na kufanya mambo
makubwa.
“Tuwaachie
walipe polisi wao wenyewe, wanajeshi wao wenyewe wataweza kwa kuwa wao
ni wachache…Tume mbalimbali zimeundwa zimeshauri serikali tatu, hata
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ina wazalendo waliofunzwa na Mwalimu
Nyerere, wameona hilo,” alisema Mtatiro.
Alisema
ndio maana Katiba ya Zanzibar imeonesha kutangulia kutoka uhuru wake,
lakini Tanzania Bara imekuwa iking’ang’ania Zanzibar kuwa ni sehemu ya
Tanzania,” alisema.
>>Habari Leo
>>Habari Leo
0 comments:
Post a Comment