
Mfanyabiashara wa Mbuzi na kusaga nafaka katika kijiji cha Kintandaa Adamu Shaban Hole (46) (mbele mwenye kofia baraghashia) na aliyekuwa tabibu msaidizi katika dispensari ya Tumaini mjini Singida, Godlisten Raymond (37) aliyefunika uso, wakisindikizwa gerezani kwenda kuanza kutumikia kifungo cha miaka 10 baada ya kutiwa hatiani na mahakama kuu kanda ya kati kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi na kuitoa na kusababisha kifo chake.Mwanafunzi huyo Hamida Athumani (16) alifariki dunia siku chache kabla ya kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi. (Picha: Nathaniel Limu/MODewji blog).
**
MAHAKAMA Kuu kanda ya kati iliyomaliza vikao vyake hivi karibuni mjini Singida, imewahukumu aliyekuwa tabibu msaidizi wa dispensari ya Tumaini Godlisten Raymond (37) adhabu ya kutumikia jela miaka 10 baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kutoa mimba kwa njia isiyo sahihi kwa mwanafunzi na kusababisha kifo chake.
Mshitakiwa Godlisten anadaiwa kumtoa
mimba mwanafunzi wa shule ya msingi Kintandaa tarafa ya Sepuka wilaya ya
Ikungi, Hamida Athumani (16) Septemba 7 mwaka 2006 na alifariki dunia
Septemba 17 mwaka huo huo wa 2006, siku chache kabla ya kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Pia
katika kesi hiyo, mfanyabiashara wa mbuzi na kusaga nafaka mkazi wa
kijiji cha Kitandaa tarafa ya Sepuka wilaya ya Ikungi, Adamu Shabani
Hole (46), naye amepewa adhabu ya kutumikia jela miaka 10 baada ya
kupatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi Hamida Athumani (16) na
kisha kushiriki kutoa mimba hiyo na kusababishia kifo mwanafunzi huyo.
Ilidaiwa
mahakamanai hapo kuwa mshitakiwa wa pili ambaye ni mfanyabiashara ya
mbuzi, Adamu katika kipindi hicho hicho, alimpa mimba mwanafunzi
mwingine, Rukia Juma aliyekuwa akisoma darasa moja na Hamida (marehemu).
Rukia
baada ya kutolewa mimba na mshitakiwa, alilazwa katika hospitali ya
mkoa mjini hapa, na aliweza kunusurika kufariki dunia baada ya kupatiwa
matibabu.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mwendesha mashitaka
wakili wa Serikali Mkuu Mfawidhi kanda ya Singida, Neema Mwanda,
aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali ya kifungo cha maisha jela kwa
washitakiwa, ili iwe fundisho kwao na watu wengine wanaotarajia kuwatoa
mimba wasichana wadogo na kisha kusababisha vifo vyao.
“Vitendo
vya watu wazima kufanya mapenzi na wanafunzi na kisha kuwapa ujauzito,
havikubaliki kabisa,kwa sababu zinaharibu maisha ya wanafunzi husika na
wakati mwingine vinasababisha vifo. Pia madaktari na tabibu wasaidizi
wenye tabia ya kutoa mimba kwa njia isiyo salama, nao wanakwenda kinyume
na sheria za taaluma zao,” amesema Mwanda.
Kwa upande wake
wakili wa kijitegemea kutoka Dodoma mjini Deus Nyabiri aliyekuwa
anamtetea mshitakiwa wa kwanza, Godlisten, aliiomba mahakama hiyo impe
adhabu nafuu mteja wake ikizingatia kuwa kosa hilo ni la kwanza kwake na
pia anategemewa na familia yake na ya wazazi wake ambao kwa sasa, wana
umri mkubwa.
Naye wakili wa kujitegemea wa mjini hapa, Raymond
Kimu aliyekuwa akimtetea mshitakiwa wa pili, Adamu, aliiomba mahakama
hiyo impe adhabu nafuu mteja wake na kiwezekana imwachie huru, kwa madai
kuwa baada ya kuwapa mimba wanafunzi wawili waliokuwa darasa la saba,
mke wake amemkimbia na familia yake imemtega.
Akitoa adhabu hiyo,
jaji Cresensia Makuru, amesema kwa mazingira ya kawaida, kosa
walililofanya washitakiwa, hawastahili huruma ya mahakama.
Amesema
vitendo vya wasichana wadogo kupoteza maisha kwa kutolewa mimba kwa
njia isiyo salama, licha ya kusababisha vifo vyao, pia vinachangia ndoto
za wazazi kwa watoto wao, kupotea.
Aidha, Jaji Makuru amesema
Katiba ya nchi inatamka wazi kwamba uhai wa mtu ni lazima uheshimiwe na
kulindwa, hata sheria za Kimataifa nazo zimetamka hivyo hivyo.
0 comments:
Post a Comment