WANAFUNZI wa vyuo vikuu nchini wameshauriwa kuacha kujihusisha katika biashara zisizofaa za kuuza miili yao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha. Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na vijana lijulikanalo kama Restless Development, Joseph Bukula, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa upimaji afya kwa hiari uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Bukula
alisema vijana wanachotakiwa kufanya kwa wakati huu ni kuhakikisha kuwa
wanajitambua kwa kufanya kile kilicho wapeleka chuoni na si kujiingiza
katika biashara zisizofaa na zinazoshusha maadili yao.
Alibainisha
kuwa vijana wengi hasa waliopo katika vyuo mbalimbali wamekuwa
wakiingia katika mitego inayowapelekea kujikuta wakipata maambukizi ya
virusi vya Ukimwi kutokana na wao kushindwa kujitambua.
"Kijana
kama atajitambua anaweza kufanya mambo yake bila hofu yoyote pia
haitakuwa rahisi kwa yeye kudanganyika kwani kujitambua kwake
kutamjengea kujiamini," alisema Bukula.
Aidha
alisema bado kuna changamoto kubwa ya elimu kwa vijana juu ya masuala
ya upimaji Ukimwi kwa hiari kutokana na kutokwepo kwa idadi kubwa ya
watu wanaojitokeza.
Alisema
lengo la kuendesha zoezi hilo la upimaji katika chuo hicho ni
kuwasaidia vijana kutambua afya zao pia kupata elimu ya maambukizi hayo
na kuweza kujikinga.
"Restless
inatoa elimu kwa vijana juu ya ugonjwa wa Ukimwi kwa vijana wa chuo
hiki lakini ambapo pia tumezindua bango chuoni hapa lenye ujumbe kwa
jamii linalosema eneza elimu na si virusi," alisema Bukula.
Naye
Mratibu wa miradi wa shirika hilo Selestine Ngowi, alisema kuwa mradi
huo wa kutoa elimu kwa vijana utakuwa endelevu ili kuweza kuwasaidia
vijana walioko chuoni na mitaani kuweza kujikinga na virusi vya Ukimwi.
Ngowi
alisema kuwa pia wamekuwa wakitumia njia mbalimbali ikiwemo redio
kuwafikishia vijana elimu inayohusu masuala ya virusi vya Ukimwi na
Ukimwi ili kuweza kupunguza maambukizi mapya kwa vijana.
Habari leo:
Habari leo: