BASI la kampuni ya Hood Limited aina ya Scania lenye namba za usajili T 159 AXM lililokuwa likitoka jijini Mbeya kueleka Arusha limepinduka kwenye kona kali iliyopo eneo la Melela-Mlandizi wilayani Mvomero, Morogoro leo majira ya saa nane mchana na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi 27.
Majeruhi kadhaa katika ajali hiyo wamekimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
Mashuhuda wa ajali hiyo walidai kwamba chanzo chake ni dereva wa lori aliyejaribu kulipita gari lingine kwenye kona hiyo.
"Mimi nilikuwa natoka Mbeya naenda Moshi kwa ajli ya sikukuu ya Krismas, dereva wetu amefanya kazi kubwa sana ya kuokoa maisha yetu.
"Tulipofika hapa kwenye kona, dereva wetu baada ya kuona lori limejaa upande wetu akaamua kukwepa kugongana nalo uso kwa uso na kuingia huku lilipo. Binafsi nampa pongezi nyingi dereva wa hili basi letu" alisema Bi. Ruth Mwambogoso abiria katika basi hilo