MSANII
wa muziki wa mduara, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ amejikuta katika wakati
mgumu baada ya kuandika juu ya uzushi wa kifo cha msanii mkongwe, Said
Ngamba ‘Mzee Small’ kupitia mtandao wa Instargram.
Shilole
ambaye baada ya kugundua kuwa hakuwa sahihi kuandika juu ya kifo hicho
kwani haikuwa kweli, alilazimika kukanusha na ndipo akaanza
kuporomoshewa ‘mvua’ ya matusi.
Baadhi
ya maneno makali yaliyoandikwa mtandaoni humo kumtukana Shilole,
ambayo hayawezi kuandikika kwa kuzingatia maadili, yalimtaka kujiepusha
na tabia ya kudandia na kueneza mambo pasipo kuyafanyia uchunguzi.
Mwandishi
wetu alipomtafuta msanii huyo kuzungumzia juu ya suala hilo, alikiri
kuandika juu ya kifo hicho huku akionesha majuto ya hali ya juu.
“Ni
kweli niliandika maneno ya taarifa za kifo cha Mzee Small, japo
nilikuwa nikiandika jinsi ambavyo msanii huyo amezushiwa kifo, sasa watu
wakadhani mimi ndiye nimeandika kwa kujitungia, najuta sana kuchapisha
ujumbe huo,” alisema Shilole.