Rehema
Chalamila aka Ray C jana alifunguka kupitia kipindi cha Mkasi jinsi
ambavyo wasanii wenzake walimtenga wakati alipokuwa amelazwa hospitali
kupatiwa matibabu ya ‘uraibu’ (addiction) wa madawa ya kulevya.
Ray
C alisema japokuwa mama yake alitoa kwa umma mawasiliano yake na
maelekezo ya namna ya kumsaidia, simu hiyo iliyokuwa busy saa 24,
ilikuwa ikipokea simu na ujumbe kutoka kwa mashabiki wake pekee na sio
msanii yeyote anayemfahamu.
Muimbaji
huyo aliyewahi kutamba na vibao vingi vikali vikiwemo ‘Niwe Nawe
Milele’ Uko Wapi na Sogea Sogea, alisema hiyo ilimpa funzo kuwa mtu
maarufu huwa na marafiki pale tu anapokuwa juu lakini akipata matatizo
hutengwa na hata watu wake wa karibu
Katika
kipindi hicho pia, Ray C aligusia jinsi ambavyo Lord Eyez alimuingiza
kwenye matumizi ya madawa ya kulevya ambapo alikuwa akimchanganyia unga
kwenye bangi bila ya yeye kufahamu na kwamba alifanya hivyo kwa mwaka
mzima.
Alisema
baada ya kujigundua kuwa tayari ameingia kwenye tatizo kubwa aliamua
kuchukua uamuzi wa haraka wa kuachana na rapper huyo ingawa anasema
alikuwa akimpenda kwa dhati.
Katika
hatua nyingine, Ray C alisema hakuna mtu anayeweza kumshukuru zaidi
kama Rais Jakaya Kikwete ambaye alimuelezea kuwa ni mtu mwenye moyo wa
kipekee kwakuwa amemsaidia kwa hali na mali na kumtoa kutoka kwenye
janga la uteja.
Aliongeza kuwa Rais Kikwete amekuwa akiwasaidia vijana wengi wenye matatizo hayo na sio yeye peke yake.
Alisema
kwa sasa tayari amesharekodi nyimbo takriban 12 na watayarishaji
tofauti wa muziki akiwemo Tudd Thomas na Ema The Boy na kwamba hivi
karibuni ataachia wimbo wake mpya.
SOURCE: TIMES FM