Na.Mhariri wa Moblog
Ingawaje Tanzania inaitwa nchi masikini pamoja na kwamba wahisani na
wadau wa maendeleo wanasema ni nchi inayoendelea lakini kwa ujumla na
kwa yeyote anayeijua nchi yetu kwa maana ya hali ya maisha ya wananchi
wake, ni jambo la hatari kwa kikundi kidogo cha watu waliokalia ofisi za
umma na kujipangia utaratibu fulani wa kujinufaisha.
Kikundi hiki kidogo tena kilichochaguliwa na wananchi kama
wawakilishi wao (wabunge) na ndio watunga sheria kujinufaisha kwa jasho
la walipa kodi kwa kisingizio cha sheria ambazo wametunga wao wenyewe
kwa kujipendelea.
Ni aibu zaidi kusikia kwamba wabunge wengi na hata baadhi ya mawaziri
kukejeli juhudi binafsi za baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania wenye kuogopa kodi za wananchi na kutaka mabilioni
hayo kuelekezwa katika miradi ya maendeleo ya wananchi kwa maslahi
mapana ya taifa.
Tumeamua kusema hayo bila kuficha kwamba ni muhimu kwa Serikali
pamoja na Bunge kufikiri upya mtindo huu wa kifisadi wa kulipana posho
ya kukaa (Sitting Allowance) wakati wana mishahara mikubwa kuzidi
wafanyakazi wenye kufanya kazi usiku na mchana kama vile madaktari
wanaosubiri kulipwa posho ya (overtime) ya shilingi elfu kumi ambayo
hukaa hadi miezi mitatu mpaka sita haijalipwa.
Tunasema na kusisitiza kuwa ujira wa vikao ambavyo ni kazi halali za
ubunge ni mshahara na si posho! Posho ni wizi wa fedha za umma mchana
kweupe kwa sababu kazi ya Mbunge ni uwakilishi na pale anapokaa kwenye
vikao vya bunge na kamati mbalimbali anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa
sheria na katiba ya nchi iweje alipwe Posho?
Mwaka juzi kwenda mwaka jana 2011/2012 Serikali ililiomba Bunge
kupitisha sh bilioni 987 kwa ajili ya psoho mbalimbali za watumishi wa
Serikali wakiwamo wabunge. Hii ni hatari kwa mustakabali wa taifa changa
kama Tanzania.
Huu ni kweli kwamba mabilioni ya shilingi zikiwa ni kodi za wananchi
kila mwaka wa fedha yanatengwa kwa ajili ya posho tu, na hata mwaka jana
Benki ya Dunia na wahisani wa maendeleo walihoji uwepo wa posho za
kukaa kwa watumishi wa serikali na wabunge lakini bado tatizo hili la
kuzoea posho linaitafuna nchi yetu bila huruma.
Serikali kupitia wizara ya fedha mwaka 2011/2012 iliahidi kwamba
posho ambazo hazina tija zitaondolewa kauli iliyoonekana kama mwanzo wa
mageuzi ya kweli, lakini leo asubuhi niliposikia kipindi cha tuongee
magazeti juu ya Wabunge kutafuna posho ovyo wote wa chama tawala na
upinzani ni ishara kwamba serikali ilitaka kauli ile ieleweke kinyume
nyume.
Gazeti la kila wiki la Raia Mwema limeongoza leo na habari za wabunge
kutafuna posho hovyo hovyo na Mbunge kijana Joshua Nasari amekiri
kwamba alichukua posho ya kwenda safari Malaysia lakini ikatokea dharula
ya Harambee jimboni kwake akaona ni busara kujumuika na wananchi wake
bravo kwake.
Bila kutafuna maneno Tanzania ni nchi maskini, kwani kipato cha mwaka
cha mwananchi wa kawaida ni Sh 770,463 hivi, wastani wa kama Sh 2,140
kwa siku, kwa mantiki hiyo Mtanzania wa kawaida kuishi katika maisha ya
leo kwa kipato hiko ni kwa kudra za mwenyezi mungu kama si rushwa dogo
dogo zinazomwezesha kumaliza mwaka.
Lakini wakati wananchi walio wengi wakiishi katika umaskini wa
kutupa, wapo watu waliaomua kusaka nafasi za uongozi katika nchi hii si
kwa nia ya kusaidiana na wananchi kutokomeza umaskini ulioelemea taifa
hili, ila kujitenga nao kwa kutengeneza utaratibu mbaya na kandamizi wa
kujilipa mafao manono kama hizi zinazoitwa posho za vikao za wabunge.
Kwa maelezo yoyote yale, posho hizi si halali hasa zinapolipwa na
taifa maskini kama Tanzania ambalo haliwezi hata kujitegemea kwa kuwa na
bajeti yake walau kwa mwaka mmoja tu bila kutembeza bakuli kwa
wafadhili ili kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa mtanzania yeyote makini atakubaliana nasi kwamba walioweka
utaratibu huu ama walipotea njia kwa ama walitanguliza mbele maslahi
binafsi lakini wananchi wameamka na wanajua kinachoendelea na
wanawasubiri 2015 kwenye uchaguzi watawaita wabunge wa posho na vitambi
vya posho kama si mchemsho na kiti moto na bia kaeni chonjo uchaguzi
unakuja!
Na kuna taarifa za kutisha kwamba siku hizi hata kazi ambazo ni
wajibu wa watumishi wa umma kuzifanya watu hawafanyi mpaka kuwepo na
posho (Bahasha) yaani ofisa wa serikali kukaa kwenye kikao cha kazi
ambayo ni wajibu wake, anadai mshiko tumekwisha!
Kwa utaratibu huu watanzania itatuchukua muda mrefu mpaka kuja kupata
maendeleo ya kweli na hakuna jambo lolote linalokwamisha uwezo wa
serikali kutimiza wajibu wake zaidi ya maposho yasiyo kuwa na kichwa
wala miguu ndugu zangu tukafanye kazi tuliotumwa na wananchi tuache
rongo rongo za posho zisizo kuwa na tija kwa maslahi ya vizazi vya sasa
na vijavyo.
Naomba kuwasilisha !
Damas Makangale
Mhariri Mkuu