Mshambuliaji mpya wa Yanga, Emmanuel Okwi kutoka Uganda ametua
nchini kuja kuitumikia klabu hiyo na kusema ataichezea kwa mapenzi
makubwa. Mchezaji huyo wa zamani wa Simba alitua
jana saa 9:30 na kulakiwa na viongozi wa Yanga na mashabiki wachache wa
klabu hiyo waliojitokeza kumpokea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar
es Salaam.
Okwi aliyesajiliwa Yanga kwa mkataba wa
miaka miwili na nusu alitua nchini na ndege ya Shirika la Rwanda na
kupokewa na Abdallah Binkleb, Musa Katabalo na Seif Ahmed ‘Magari’.
Akizungumza
mara baada ya kutua uwanjani hapo, Okwi ambaye alizaliwa Desemba 25,
1992 alisema: “Mimi ni mchezaji na mpira ni kazi yangu, nimekuja
kuichezea Yanga na nitaitumikia kwa mapenzi yangu yote. Nimekuja kufanya
kazi na si kuiangalia Simba. Mkataba wangu na Simba ulishaisha.”
Kuhusu
utata wa usajili wake Yanga, Okwi alisema: “Mimi hayo mambo siyajui,
nimeyaacha mikononi mwa viongozi wa Yanga ndio watakaomaliza hilo
suala.”
Akizungumzia mechi ya Yanga na Simba
itakayofanyika Jumamosi alisema: “Mimi nipo fiti. Nipo tayari kucheza
mechi ya Simba. Nimejiandaa kikamilifu, ila mwenye uamuzi wa mwisho wa
mimi kucheza au kutocheza ni kocha, kama atanipanga nitafurahi zaidi.”
Okwi
amejiunga kambini na wenzake jana jioni jijini Dar es Salaam kwa ajili
ya maandalizi ya mechi yao ya Nani Mtani Jembe, Jumamosi.
Simba
ilimuuza Okwi kwa Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dola 300,000
za Marekani ambazo klabu hiyo ya Msimbazi haijalipwa hadi sasa.
Simba
walikubaliana na klabu hiyo walipwe hadi Septemba mwaka huu, lakini
haikuwa hivyo na kufungua kesi kwa Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa)
ikidai fedha hizo.
Wakati Simba ikidai fedha hizo,
Okwi aliikacha Sahel akidai hajalipwa mishahara yake na Fifa ikaamua
kumpeleka SC Villa ya Uganda ili acheze kwa miezi sita kulinda kiwango
chake baada ya Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa) kuomba kwa Fifa.
Villa imemuuza kwa Yanga na Fufa kubariki lakini imeandika barua Fifa kuulizia uhalali wa usajili wa mshambuliaji huyo.
Picha na GPL