ODAMA AELEZA ALIVYO KUTANA NA MAREHEMU RECHO

MTOTO mzuri mwenye asili ya Kihaya, Jenifer Kyaka ‘Odama’ aliyesoma shule ya msingi mkoani Kigoma kisha kuhamia jijini Dar na kupitia kozi tofautitofauti kabla kutupa karata yake katika anga la filamu ndiyo tupo naye leo katika Exclusive Interview.
Mtoto mzuri mwenye asili ya Kihaya, Jenifer Kyaka ‘Odama’ akiwa na marehemu Recho Haule enzi za uhai wake.
Awali, hakuwahi kuwaza kama siku moja anaweza kuwa mwigizaji, lakini baadaye upepo ulibadilika na kujitengenezea jina la kazi, Odama. Kwenye makala haya amefunguka mambo mengi kuhusiana na safari yake ya uigizaji, twende pamoja:
Mwandishi: Wasomaji wetu wangependa kujua historia yako kifupi?
Odama: Nilianzia masomo yangu kule Kigoma baadaye nikahamia Shule ya Msingi Mburahati, sekondari nikamalizia Moshi mwaka 2000.

Mwandishi: Nini kilifuata baada ya kumaliza masomo yako ya sekondari?
Odama: Nilisoma kozi mbalimbali za kompyuta kisha ndipo nikajikuta nimekita nanga katika masuala ya filamu.

Mwandishi: Ulianzaje na nani ambaye alikuunganisha na fani hiyo?
Odama: Nilivutiwa na uigizaji ghafla, nikajiunga na Kikundi cha Kidedea, nikafanya mazoezi lakini bahati mbaya mmiliki wa kikundi hicho, Peace alifariki kikasambaratika hivyo nikawa nimepoteza uelekeo wa kisanaa.

Mwandishi: Ulifanya nini baada ya kundi hilo kufa?
Odama: Nilikaa kwa muda kisha baadaye nilikutana na ‘camera man’ mmoja anaitwa Musa Banzi ambaye alinikuta Holliday Inn, Posta nikiwa na rafiki yangu ndipo wakaniomba kushuti katika kipande cha wimbo wao baada ya mtu waliyekuwa wamempanga aje kuchelewa, baada ya kumudu uhusika vizuri katika video hiyo, kila mtu aliyekuwepo hotelini hapo aliguswa na mimi. Wakanishauri nijikite katika uigizaji.

Jenifer Kyaka ‘Odama’
Mwandishi: Wazazi wako walikupokeaje ulipoanza kujishughulisha na sanaa?
Odama: Nashukuru Mungu walinipokea vizuri, walinitia moyo na kuamini kwamba naweza kujiingizia kipato kupitia sanaa.

Mwandishi: Ugumu gani ulipitia kwenye sanaa?
Odama: Kujifua kwenye mazoezi pasipo kujulikana na watu kwa muda mrefu ndiyo changamoto kubwa niliyopitia. Kidogo nilianza kuona mwanga wa mafanikio nilipokutana na wasanii wenzangu kina Riyama, Shumileta na wengineo katika Kundi la White Elephant ambalo lilikuwa chini ya Banzi.

Mwandishi: Katika upande wa filamu, muvi gani ilikuwa ya kwanza wewe kuigiza?Odama: Sikuwa muhusika mkuu katika muvi ya kwanza kuigiza lakini ilikuwa ni Shumileta ambayo ilimpa jina mwenzangu Jenifer Mwaipaja, kila mtu akamtambua kwa jina la Shumileta.
Mwandishi: Kwa nini majina ya umaarufu zamani yalikuwa yanazalishwa na jina la filamu?
Odama: Basi tu ilikuwa inatokea hivyo, mashabiki walikuwa wakipenda kutumia jina la filamu hususan ile ambayo umecheza vizuri na kukubalika ndiyo maana hata mimi jina langu lilizaliwa mwaka 2005 nilipocheza filamu ya Odama.

Mwandishi: Ulianza lini  kujitegemea mwenyewe rasmi na kusimama katika soko la filamu?
Odama: Ilikuwa ni mwaka 2009 baada ya kufanikiwa kuanzisha kampuni yangu ya filamu, J Film 4 Life.
Mwandishi: Ulipata wapi mtaji wa kuanzisha kampuni?

Odama: Nilikuwa nafanya biashara zangu tu ambazo zilinipa mtaji wa kwenda kununua vifaa vyangu na kufungua ofisi.
Mwandishi :Inasemekana mapedeshee ndiyo ambao walikupa mtaji wa kufungua kampuni ya filamu, ni kweli?
Odama: Sijawahi kupewa mtaji na pedeshee, sina pedeshee aliyeniwezesha na wala sitakuja kuwa naye.
Mwandishi: Mlikutana wapi na marehemu Recho (Sheila Haule).
Odama: Recho nilikutana naye kipindi f’lani nilipokuwa nikifanya kazi na Bajomba (prodyuza) ambapo nilikutana na Lamata (muongozaji), tukakutana na Recho na kuanza kufanya naye kazi.

Mwandishi: Unakumbuka muvi ya kwanza kucheza na marehemu Recho?
Odama: Nakumbuka, ilikuwa ni muvi iliyofahamika kwa jina la Candy.
Mwandishi: Hebu tuambie mlikutana wapi na boifrendi wako wa kwanza?
Odama: Heeee! Swali gumu…anyway ni hivi….

Usikose wiki ijayo ili kujua Odama alikutana wapi na ‘boyfriend’ wake wa kwanza.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

1 comments:

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini