UMUHIMU WAKO KWA MWENZI WAKO UKO WAPI?

KUNA wakati inatokea kwenye uhusiano, mmoja wao  akadhauriwa na mpenzi wake na kuonekana wa kawaida tu. Athari kubwa zaidi katika kuonekana wa kawaida au kudharauliwa ni kuachana wakati wowote – kwa ghafla.
Mara nyingi tendo la kuachana kwa wenzi wa aina hii huwa hakuna sababu kubwa sana. Jambo dogo tu linaweza kukatisha uhusiano lakini kumbe ndani kuna siri nyingine kubwa zaidi; kushuka thamani – kupoteza umuhimu kwa mwenzako.
Marafiki zangu, wakati uhusiano unapofikia kwenye hatua hii huwa ni hatari sana na uamuzi wa kuachana hupewa nafasi kubwa zaidi kwa pande zote. Habari mbaya zaidi ni kwamba, hata kama wahusika watakuwa wana ndoa, huwa si kigezo kikubwa sana kwao, badala yake hufikiria kuachana kama ndiyo kitulizo cha mioyo yao.
PANUA MAWAZO
Nazungumzia kuhusu thamani. Ni somo linalohitaji utulivu mkubwa wa akili na utayari wa ubongo. Ninaposema kushuka thamani namaanisha kupungua kwa umuhimu au kupotea kabisa.
Kubwa ambalo utakuwa umebaki nalo (labda) ni kukutana kwa ajili ya mapenzi tu. Hawezi kukushirikisha katika mambo yake kwa sababu huna thamani kwake.

Kwa bahati mbaya ni kwamba, ukishushwa thamani, mara nyingi unaweza usigundue hilo hivyo kuendelea na maisha kama kawaida katika mtindo ambao kumbe tayari mwenzako ameshakubadilisha daraja.
UMUHIMU KUPUNGUA...
Ninachohitaji kuzungumza nanyi marafiki zangu ni namna ya kujipandisha thamani ili mpenzi wako asikuchoke wala kukushusha au kukuona wa kawaida. Kila wakati akuone wa muhimu na akufanye namba moja katika maisha yake.

Kabla sijafika hapo nataka kwanza mfahamu dalili atakazozionyesha mwenzako zinazoashiria kuwa amekushusha thamani.
(i)  Mawasiliano
Hapa inategemea na kasi ya mawasiliano mliyokuwa nayo mwanzo lakini kwa kiwango chochote kile huanza kupungua. Kama alikuwa na kawaida ya kuwasiliana nawe mara kwa mara akikueleza mambo mbalimbali – hata madogo tu, kuhusu mwenendo wa siku yake, ataacha.

(ii) Anaanza kuwa msiri
Kulingana na kiwango cha uhusiano wenu, ataanza kuwa msiri kwa baadhi ya mambo yake. Hata kama anafanya jambo fulani zuri kwa ajili ya maisha yenu ya baadaye, hatakuambia. Unaweza kushtukia tu kusikia kwa watu kuwa mwenzako ameagiza gari au amenunua kiwanja mahali  na pengine ameshaanza ujenzi bila kukujulisha.

(iii) Atakupuuza
Kama awali alikuwa na kawaida ya kukusikiliza, sasa ataanza kukupuuza. Unaweza kumwambia jambo lenye manufaa makubwa kwenu lakini asilichukulie umakini. Hii ni dalili kwamba wewe huna thamani kwake.

MENGINE...
Kama umeshushwa thamani unakuwa kwenye hatari ya kuachwa. Hata kama mwenzako alikuwa ameshafikiria suala la kuingia kwenye ndoa lakini kwa sababu ameshakushusha thamani ndoa inaweza kuyeyuka.

Ukiwa kwenye ndoa ni hatari zaidi maana mwenzako hukuchukulia wa kawaida – mazoea huzidi na hapo ndipo uhitaji wa kuwa na mwingine wa pembeni unapoanza. Haoni cha muhimu tena kwako, ndiyo maana wazo hilo huvamia ubongo wake kwa kasi.
Itafikia hatua, kama upo ndani ya ndoa, mwenzako atagoma kuongozana na wewe na kama ikitokea hivyo mkikutana na rafiki zake njiani hatakutambulisha. Hisia kwamba hamuendani humwingia.
Yapo mambo ya kujifunza zaidi kuhusu mada hii. Je, ukigundua hayo, nini cha kufanya? Wiki ijayo nitakuwa hapa kwa mwendelezo wake.

USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini