MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Talib Ali Talib, amesema wanachama na viongozi wanaohoji Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa kutengenezewa fulana zenye picha yake na ujumbe wa ‘Friends of Lowassa’ (Marafiki wa Lowassa) ni washamba.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, mjumbe huyo alisema
haikuwa sahihi kwa Waziri Mkuu mstaafu John Samuel Malecela kushangaa
fulana za kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Lowassa za kuwaletea
maendeleo wananchi kupitia makundi ya jamii.
Alisema mtu anayefanya jambo zuri, anastahili kuungwa mkono na
kukumbukwa kwa njia mbalimbali zinazokubalika kama kuchapisha fulana na
kuweka picha yake au kufanyiwa sherehe kama inavyotokea kwa viongozi
wengine ndani na nje ya nchi.
“Watu wanaohoji fulana za Lowassa ni washamba, mbona hawahoji fulana
za Bob Marley, Mandela, Mwalimu Nyerere?” alisema Talib, mjumbe wa NEC
kupitia Wilaya ya Mjini, Zanzibar.
Kauli hiyo imekuja baada ya Malecela kudai haikuwa sahihi kwa Lowassa
kuanza kampeni za urais kabla ya wakati kwa kuchapisha fulana zenye
picha na ujumbe wa ‘Friends of Lowassa’.
Hata hivyo, Talib alisema imefika wakati viongozi wa CCM kujadili
mambo yenye maendeleo badala ya mambo ya mitaani ambayo hayasaidii
kujenga umoja na mshikamano katika kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Kuhusu kauli ya Katibu Uhamasishaji Chipukizi wa UVCCM, Paul Makonda,
kwamba Lowassa hatoshi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wala Amiri
Jeshi Mkuu kutokana na kutokuwa muadilifu, alisema kijana huyo
amemvunjia heshima Lowassa na anapaswa kujadiliwa na kuchukuliwa hatua
za kinidhamu.
Alisema UVCCM hakuna kikao kilichowahi kukaa kiwe cha sekreterieti au
Baraza Kuu kujadili watu wanaotajwa kuwa na nia ya kugombea urais na
kushangazwa na kauli ya Makonda kuchukuwa uamuzi wake binafsi na
kuugeuza kuwa msimamo wa jumuiya hiyo.
Alisema kwamba madhumuni ya kuanzishwa UVCCM ni kuwatayarisha vijana
kuwa viongozi wa baadaye, na kushangaa kitendo cha Makonda kumshambulia
Lowassa hadharani bila ya kuzingatia tofauti yake ya umri.
>>Tanzania daima
>>Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment