Shule
ya Msingi Mtambani iliyoko Kinondoni jijini Dar es Saalam, haina
samani hali inayosababisha wanafunzi kukaa chini, wakati walimu
wanalazimika kutandaza khanga wanazokalia chini ya miti.
“Shule hii ina upungufu wa madawati, nusu ya wanafunzi wanakaa chini,
hatuna ofisi za kutosha za walimu wale wasio na nafasi wanakaa chini
ya miti”, alisema Mwalimu Mkuu Emmanuel Munisi.
Aliongeza kuwa tatizo hilo linawalazimisha wengine kutandika khanga
chini ya miti ili kufanya kazi kwa sababu ya ukosefu wa meza za
kufanyia kazi na kwamba mvua inaponyesha wanalazimika kujikusanya pamoja
na wanafunzi madarasani, alisema Munisi.
Shule ya Mtambani iko taabani wakati serikali ilipata chenji ya rada ya
shilingi bilioni 43 ambayo ilielezwa kuwa pamoja na kununua vitabu
mashuleni pia itawezesha upatikanaji wa madawati.
Serikali ya Uingereza ilirudisha fedha hizo kuanzia mwaka jana na
kwamba jukumu la kununua vifaa hivyo liliachwa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambayo inasimamia shule za
serikali za msingi na sekondari.
Shule hiyo ina walimu 41 na wanafunzi 1,830 inakabiliwa na uhaba wa
madawati, viti na meza za walimu kwa mujibu wa Munisi. Aliiambia
NIPASHE Jumamosi kuwa mazingira mabovu ya shule hiyo ni pamoja na
upungufu wa vyoo, ukosefu wa sakafu madarasani badala yake madarasa
yana mahandaki na vumbi kila wakati. Akifafanua, alisema kuwa shule
hiyo ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa na wanafunzi 77 na ofisi moja ndongo
kwa ajili ya walimu. Hata hivyo, kwa sasa ina wanafunzi 1,830 wa kike
917, wavulana 913 na walimu 41.
Alisema hakuna maji safi ya kunywa na wanafunzi wengi wanakabiliwa na matatizo ya njaa yanayosababisha kudondoka mara kwa mara.
Alieleza kuwa wastani wa kuanguka ni kati ya watoto watano na zaidi
ambao hutibiwa kwa kuwekewa drip za kuongeza maji na sukari mwilini.
Madaktari wanasema tatizo ni ukosefu wa chakula na nguvu mwilini kwa
hiyo wanapotundikiwa drip wanapona.
Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa Mtambani, Steven Ngonye, akizungumzia
tatizo hilo alisema litashughulikiwa pamoja na upatikanaji wa maji na
ukarabati wa shule hiyo.
Naye Diwani wa Kata ya Mtambani Maji Safi Sharifu, alisema serikali
inalitambua tatizo hilo na imetenga bajeti ya Sh. milioni 108 kwa ajili
ya madawati na ukarabati wa vyumba vya madarasa na kwamba hadi sasa
madawati 50 yameshapelekwa shuleni hapo.
Akifafanua zaidi alisema kuna mpango wa kuongeza vyumba vya madarasa
mawili pamoja na kufikisha maji safi kazi itakayogharimu Sh. milioni 20.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment