NAIBU MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AIOMBA MAHAKAMA KUU IITUPILIE MBALI KESI YA KIKATIBA INAYOMKABILI WAZIRI MKUU, MIZENGO PINDA


NAIBU Mwanasheria Mkuu, Mhe George Masaju (pichani) amedai mahakamani katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) dhidi  ya  Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba kwa mujibu wa katiba mamlaka ya mahakama kuingilia mwenendo wa bunge yameondolewa. 

 Pia, Mhe Masaju amedai kuwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi bunge halina mamlaka ya kuingilia mwenendo wa mahakama na kwamba kesi iliyopo mahakamani haina mashiko ya kisheria  hivyo  mahakama iitupilie mbali. 
 
Kesi hiyo ya Kikatiba inasikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu, akisaidiana na Jaji Augustine Mwarija na Dk. Fauz Twaib. 
 
Mhe. Masaju alitoa madai hayo jana wakati akijibu hoja za upande wa walalamikaji kwamba kesi iliyopo mahakamani ina mashiko ya kisheria. 
 
“Watukufu majaji, kwa mujibu wa kifungu cha 4 kidogo cha 4 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinaeleza kwamba kila chombo kitaundwa na kutekeleza majukumu yake… mahakama haina mamlaka ya kuingilia mwenendo unaotokea bungeni na kwa utaratibu huo, wabunge wanazuiliwa kujadili masuala yaliyoko mahakamani” alidai Mhe Masaju. 
 
 Mbali na Mhe Masaju upande wa walalamikiwa, mawakili wengine ni, Mawakili wa Serikali Wakuu, Gabriel Marata, Sara Mlipano na Alesia Mbuya. 
 
 Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo  ambapo upande wa walalamikiwa watato hoja zao. Katika madai ya msingi LHRC na TLS waliwasilisha madai mahakamani wakidai wanapinga kauli iliyotolewa na Mhe. Pinda bungeni, Juni 20, mwaka huu, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo.  
 
Mhe.Pinda anadaiwa kutoa kauli inayolalamikiwa alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyetaka kujua msimamo wa serikali na mambo mengine, malalamiko dhidi ya vyombo vya dola katika baadhi ya maeneo kama Mtwara, kuwapiga wananchi.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini