Mtoto Ismail Barihegi.
MTOTO Ismail Barihegi, mwenye umri wa miaka 12 mkazi wa Kijiji cha
Fukayosi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ameokotwa akiwa amekatwa
mapanga baada ya kudaiwa kuipeleka mifugo yao katika mashamba. Barihegi ambaye amelazwa katika Jengo la Mwaisela Wodi na 17, Muhimbili, alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba siku ya tukio (hakumbuki)alikuwa akichunga ng’ombe porini lakini ghafla walitokea watu na kumwuliza kwa nini aliwaachia ng’ombe wake kufika shambani.
Alisema aliwakatalia watu hao kwamba mifugo iliyokuwa shambani haikuwa ya kwao, na hata kuwaonesha ng’ombe wao, lakini watu hao hawakumwelewa.
“Walianza kunikata mapanga kichwani, begani na sehemu zingine za mwili, nililia sana huku nikiwaomba wanisamehe hawakunisikia.
“Wenye ng’ombe walishakimbia, waliniambia ni lazima waniue, niliwaomba wasiniue, lakini hawakunijali, niliishiwa nguvu, damu nyingi ilikuwa imenitoka,waliondoka na kuniacha porini peke yangu.
“Nilipiga kelele ili nipate msaada lakini hakuna aliyejitokeza, nilikata tamaa, baada ya saa kadhaa mtu mmoja alipita na kuniona, akawaita watu akiwemo Mwenyekiti wa kijiji chetu, wakaja kunichukua na kunikimbiza katika zahanati,” alisema mtoto huyo.
Kijana huyo alisema kwamba baada ya huduma ya kwanza katika zahanati hiyo, alihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya hali yake kuonekana mbaya zaidi na kwamba ana uhakika wazazi wake hawajui alipo kwani hadi sasa hawajafika kumtembelea.
“Ninamshukuru sana mwenyekiti kwa kunipa msaada mkubwa, sasa hivi amerudi kijijini, najua atawapa taarifa ndugu zangu, ninawashukuru madaktari na wauguzi kwa kuokoa maisha yangu kwani kwa sasa nina nafuu tofauti na nilivyookotwa katika msitu mnene,” alisema Barihegi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani, Athumani mtasha alipoulizwa kuhusiana na tukio alisema kuwa amehamishiwa makao makuu.
Kamanda wa polisi wa mkoa huo, SACP Urich matei yupo nje ya mkoa kikazi ila kaahidi kufuatilia sakata hilo kwa undani.
0 comments:
Post a Comment