BUNGE LA KATIBA: WAPENTEKOSTE WASHIKANA UCHAWI....MWENYEKITI WA USHIRIKA WA WACHUNGAJI AMTAKA KATIBU WA BARAZA LA MAASKOFU AJIUZULU


BARAZA la Maaskofu wa Kipentekoste nchini (PCT), limeshauriwa kuonesha kitabu kilichosainiwa na watumishi Ofisi ya Rais, Ikulu baada ya kuwasilisha majina yaliyopendekezwa kwa ajili ya uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji wa Kipentekoste nchini, Askofu Pius Ikongo, alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Majira.

Alisema ili kumaliza utata uliopo kati ya Ikulu na baraza hilo, Katibu Mkuu wa baraza hilo anapaswa kuonesha kitabu hicho ili waumini waweze kupata ukweli wa jambo hilo.

Aliongeza kuwa, kama kitabu hicho kipo ni fursa nzuri kwa Maaskofu kuendelea kuibana Serikali ili kujua kwanini haijawapa haki yao ya msingi kama ilivyo kwa wengine.
"Kama Katibu Mkuu atashindwa kuonesha kitabu hiki ni vyema akajiuzulu kwa kuwagombanisha waumini na Serikali kwani ndio dalili zinazoonekana kutokea," alisema.

Alisema Mwenyekiti wa baraza hilo, Askofu David Batenzi, anapaswa kuitisha kikao cha waumini na kuwaonesha majina yaliyopelekwa Ikulu kwa ajili ya uwakilishi wa Bunge hilo.
 
"Waumini wakioneshwa majina na ikibainika majina hayo hayajapelekwa Ikulu, Serikali iombwe radhi kwa kilichotokea kwani waumini hawawezi kupotoshwa na mtu mmoja, lazima suala hili lifuatiliwe kwa undani," alisema.

Hivi karibuni, PCT lilitoa tamko la kusikitishwa na kitendo cha Serikali kuwabagua katika uteuzi wa wajumbe wa Bunge hilo kwani wao ni miongoni mwa taasisi kubwa za kidini iliyowasilisha majina serikalini kama walivyoagizwa.

Tamko hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Askofu David Batenzi, ambaye aliongeza kuwa, Serikali inapaswa kukomesha mara moja ubaguzi wa kidini nchini ambao kimsingi umekuwa ukigawa watu kwa makundi ukitawaliwa na siasa, udini na ukabila.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini