SIRI NZITO YAVUJA: RAIS HAVUNJI BALAZA LA MAWAZIRI

SIRI nzito imevuja! Ni dhahiri kwamba, Rais Jakaya Kikwete ‘JK’ hatavunja baraza la mawaziri kufuatia kusitisha kwake uteuzi wa mawaziri wanne na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mipango na Uchumi,  Dk. William Augustao Mgimwa kama wengi wanavyoamini bali atabadilisha tu, Risasi Jumamosi lina cha kushika mkononi.
Waziri Mkuu, Mh. Mizengo Pinda.
Mawaziri ambao uteuzi wao ulitenguliwa ni Emmanuel John Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Mathayo David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Balozi Khamis Juma Kagasheki (Maliasili na Utalii) aliyejiuzulu kutokana na ukiukwaji wa maadili na haki za binadamu katika Oparesheni Tokomeza Ujangili.                                   Mhe.Nchimbi.
KWA NINI HAVUNJI BARAZA?
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani serikalini, JK hana mpango huo kwa sababu kuu mbili. Kwanza kuvunja baraza la mawaziri ni kumuweka kando waziri mkuu wa sasa, Mizengo Kayanza Peter Pinda na kuteua waziri mkuu mwingine.
Pili, atakuwa  anaongeza mzigo kwa serikali kwa kuwa waziri mkuu akiondoka madarakani huendelea kulindwa na serikali na kupokea stahiki zake mbalimbali.

NI NYERERE
Tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ni Baba wa Taifa tu, hayati Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyewahi kuwa na mawaziri wakuu wanne.
Alianza na Rashid Mfaume Kawawa, akafuata Edward Moringe Sokoine, Salim Ahmed Salim (baada ya kifo cha Sokoine) na Cleopa David Msuya.

AWAMU YA MWINYI
Katika awamu ya pili, Rais Ally Hassan Mwinyi, mawaziri wakuu walikuwa Joseph Warioba, John Malecela na David Msuya.
Katika awamu ya tatu ya Rais Benjamin William Mkapa kulikuwa na waziri wakuu mmoja tu, Frederick Tuluwayi Sumaye.

WAZIRI MKUU HADI 2015
Kwa sababu hiyo, chanzo kikasema kuwa Pinda ataendelea ‘kuula’ kwenye nafasi yake ya kuwa waziri mkuu wa Tanzania hadi mwisho wa muhula wa awamu ya nne, mwaka 2015.

WATAENDELEA KUPANGUA
Hata hivyo, kwa mujibu wa chanzo hicho, JK na rais ajaye wataendelea kukumbwa na shinikizo la kupangua baraza la mawaziri kila wakati kutokana na mfumo wa madaraka uliopo sasa.
“Unajua mfumo wa sasa uko hivi; waziri anateuliwa na rais, katibu mkuu wa wizara pia anateuliwa na rais. Katibu mkuu wa wizara ana uwezo wa kumfukuza kazi mkurugenzi wa halmashauri bila waziri kujua, lakini waziri hana uwezo huo.
“Nguvu kubwa ya kazi ipo kwa makatibu wakuu ambao ndiyo watendaji wakubwa wa wizara. Kinachotokea ni kwamba kama wizara itampata waziri mwenye kusimamia sawa majukumu yake kiasi cha kutishia ulaji wa makatibu wakuu, atawekewa zengwe mpaka ang’oke.
“Ndiyo maana utakuta mawaziri kwenye wizara kila siku wanawajibika kisiasa lakini makatibu wakuu wapo tu. Ni mfumo mbaya wa kimadaraka hivyo JK atabadili kila siku, hata rais ajaye naye atakuwa katika harakati hizo,” kilisema chanzo hicho.

MAWAZIRI ZAIDI
Chanzo kikaenda mbele zaidi kwa kunyetisha kwamba, wapo mawaziri ambao wanakalia kuti kavu na huenda wakang’olewa kabisa kutokana na utendaji kazi wao usioridhisha.

SHUKURU KAWAMBWA
Huyu anadaiwa kung’oka wakati wowote kutokana na madai ya walimu.
Chanzo kilisema kuwa Kawambwa pia anaponzwa na mfumo kwani kwa kawaida mwalimu anaajiriwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi lakini usimamizi wake unakuwa chini ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Ikadaiwa kuwa mwalimu anapandishwa cheo na Wizara ya Utumishi, lakini mshahara analipwa na Wizara ya Fedha, Mipango na Uchumi (hazina).
“Sasa mwalimu akipandishwa cheo na utumishi, nyongeza ya mshahara inatakiwa itoke hazina. Hazina nao wanakuwa hawana habari kwa sababu ya mawasiliano duni, matokeo yake mwalimu analia na mwajiri wake ambaye ni Wizara ya Elimu. Hili la walimu litamng’oa Kawamba,” kilisema chanzo.
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, mama Anne Kajumulo Tibaijuka.
ANNA TIBAIJUKA
Chanzo kilidai kwamba Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, mama Anne Kajumulo Tibaijuka naye yupo mguu pande, sawa kwa sababu ya migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mfano: “Wakulima wanaopakana na Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu, Manyara, wamekuwa wakilalamikia kitendo cha mazao yao kuunguzwa na mbolea hiyo, waziri ameshaambiwa akajibu atafuatilia, sasa atafuatilia mpaka lini?
“Kuna kamati iliundwa kufuatilia suala hili. Pia inadaiwa kuwa vigogo mbalimbali wa serikali wamejimegea maeneo makubwa ya ardhi mkoani Morogoro hivyo kusababisha migogoro isiyoisha kati ya wakulima na wafugaji wanaogombea ardhi kiduchu iliyobaki, huenda ikawa miongoni mwa mambo yatakayomng’oa madarakani Mheshimiwa Tibaijuka,” kilisema chanzo.

CHRISTOPHER CHIZA
Huyu ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika. Wizara yake inakabiliwa na tuhuma ya kuzembea kwenye eneo la mashamba ya mpunga katika Kijiji cha Kapunga, Mbarali, Mbeya.
“Kuna kaburu mwekezaji alinunua shamba hilo lililokuwa la Nafco, hajalilima matokeo yake  analikodisha kwa wanakijiji vipandevipande. Sasa mtu ataitwaje mwekezaji wakati ni mbangaizaji tu, hii ni kashfa, wizara ipo na haisemi lolote.
“Naamini ripoti ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyokuwa ikiongozwa na Profesa Peter Msolwa itaanika madudu yote haya,” kilisema chanzo.

WANAVYOTAKA WANANCHI
Risasi Jumamosi wiki iliyopita liliingia mitaani kusikiliza maoni ya wananchi juu ya watu wanaotakiwa kuwa mawaziri kushika nafasi zilizoachwa wazi.
Katika kila wananchi kumi, nane walitaka mawaziri na wizara zao wawe hivi:
Benard Membe, Waziri wa Fedha, Mipango na Uchumi. Asha-Rose Mtengeti Migiro (Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Lazaro Samuel Nyalandu (Waziri wa Maliasili na Utalii) na Anne Kilango Malecela (Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi).
Wananchi hao walisema, Harrison George Mwakyembe na John Pombe Magufuli waendelee kwenye wizara zao  kwa vile utendaji kazi wao ni mzuri, hauna shaka huku wakitaka George Huruma Mkuchika awe Waziri wa Ulinzi.

“Ila Amos (Gabriel) Makalla awe waziri kamili wa habari, yule mama (Fenella Mukangala) apelekwe wizara nyingine. Waziri wa Mambo ya Ndani sisi wananchi tunamwona. Halafu yule mama anaitwa Joanista (Joackim) Mhagama aingizwe kwenye Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,” alisema mkazi wa Kijitonyama, Dar aliyejitambulisha kwa jina la Kadoda, fundi wa magari, Bamaga, Mwenge.  

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini