RAIS KIKWETE AWAPONGEZA MAWAZIRI WALIOJIUZULU, ASEMA WAMEONYESHA UKOMAVU WA KISIASA



Rais Jakaya Kikwete, amewapa pole mawaziri wanne waliofutwa nyadhifa zao kutokana na matatizo yaliyowakuta na kuwapongeza kwa uamuzi wa kukubali kuwajibika kwa makosa yaliyofanywa na maofisa wa chini yao wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.

Mawaziri ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais Kikwete ni Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani); Mathayo David Mathayo (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na Shamsi Vuai Mahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) huku Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, akijiuzulu.

Hatua hiyo ilichukuliwa Desemba 20, mwaka huu baada ya wabunge kuchachamaa kufuatia kuwasilishwa kwa ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ambayo iliainisha mateso, manyanyaso, mauaji ya wananchi na wengine kupoteza mali yao wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo katika maeneo kadhaa nchini.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Mwenyekiti wa kamati, James Lembeli, alisema pampja na mambo mengine, mawaziri hao walishindwa kusimamia operesheni hiyo badala yake jukumu hilo lilibakia kwa watekelezaji chini ya viongozi wakuu wa vyombo vya usalama.

Akilihutubia Taifa juzi usiku kutoa salamu za Mwaka Mpya wa 2014, Rais Kikwete alisema mawaziri hao wameonyesha ukomavu wa kisiasa na kiuongozi wa hali ya juu na moyo wa uzalendo.

Alisema kuwa ataunda Kamisheni ya Uchunguzi itakayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu na kwamba uchunguzi wa kina utafanywa kuhusu kadhia yote hiyo.

“Makosa yaliyofanyika yataainishwa na waliofanya kutambuliwa ili wachukuliwe hatua zipasazo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.

“Ni muhimu kufanya hivi ili haki itendeke ipasavyo. Mtindo wa mzigo wa makosa ya watumishi wa umma kubebwa na viongozi wa kisiasa pekee, tena wasiokuwa na hatia ya moja kwa moja, siyo sahihi. Lazima kila mtu abebe mzigo wake inavyostahili. Ni matumaini yangu pia kwamba katika siku za usoni kunapotokea matatizo ya namna hii uchunguzi uwe wa kina ili wale hasa waliohusika na kutenda makosa wawajibishwe,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Uwajibikaji wa wana-siasa peke yao hautoshi, kwani huwaacha waharibifu waendelee na kazi isivyostahili. Mtindo huu utawafanya watumishi wasione umuhimu wa kutokurudia makosa. Hata hivyo, pale kwenye ushahidi wa wazi kwamba kiongozi wa kisiasa angeweza kuchukua hatua za kuzuia madhara, lakini hakufanya, hivyo lazima kiongozi huyo awajibike.”

Alisema serikali inakamilisha matayarisho ya kuanza awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza. Na kwamba ni muhimu kuendelea nayo kwani bila kufanya hivyo, hivyo majangili wataendelea na vitendo vyao viovu.

“Hali ni mbaya sana kwa upande wa uwindaji wa ndovu. Nilipolihutubia Bunge tarehe 7 Novemba, 2013, nilieleza kuwa tutafanya sensa ya ndovu katika Pori la Hifadhi la Selous. Sensa hiyo imekamilika, lakini taarifa yake inatisha. Kuna ndovu 13,084 tu wakati mwaka 1976 walikuwa 109,419. Tusipoendelea na Operesheni hii baada ya miaka michache ijayo hakutakuwa na ndovu hata mmoja,” alisema na kuongeza:

“Hali kadhalika, zoezi la kuondoa mifugo katika mapori ya hifadhi ya taifa litaendelea. Katika awamu ya pili ya Operesheni hii, washiriki watasisitizwa kutokutenda maovu yaliyofanyika katika awamu ya kwanza.”

MAFANIKIO YA OPERESHENI
Mbali na kasoro za operesheni hiyo, Rais Kikwete alisema kazi nzuri imefanyika chini ya Operesheni hiyo na kwamba mafanikio ya kuleta matumaini yameweza kupatikana.

“Mitandao ya ujangili imeweza kutambulika na wahusika wake kadhaa wametiwa nguvuni. Mitandao hiyo inahusisha watu wa aina mbalimbali.

Wamo raia wa kawaida, wapo watu maarufu, wapo watumishi wa idara mbalimbali za Serikali wakiwamo wa Idara za Wanyamapori na Misitu. Watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha za kijeshi 18, za kiraia 1,579 na shehena kubwa za meno ya ndovu na nyara nyingine navyo vilikamatwa.Watu kadhaa tayari wameshafikishwa
Mahakamani,” alisema.
 

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini