POLISI YAKIRI KUWAPIGA BOMU WANAKWAYA SITA WA KANISA KATOLIKI MKOANI ARUSHA



Siku moja baada ya taarifa ya kupigwa bomu wanakwaya wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Usa River, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, amefafanua kuwa polisi walitumia bomu la machozi kuwarushia watu kwa lengo la kudhibiti vurugu akidai kuwa waliwarushia polisi mawe, usiku wa mkesha wa mwaka mpya.
 
Katika tukio hilo, waumini sita waliokuwa wakitoka kwenye ibada ya mkesha wa mwaka mpya katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Karoli Lwanga, eneo la Kisangani Usa River walijeruhiwa maeneo ya miguuni kwa kuchanwa na vitu vilivyosababishwa na mlipuko huo.
 
Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, waliojeruhiwa ni Aneth Baltazar Makoi (17), mkazi wa Magadini ambaye alijeruhiwa miguu yote miwili na sehemu ya paja la mguu wa kushoto na mwingine ni Mary Melkiori Kwayu (40) mkazi wa Leki Tatu ambaye alijeruhiwa miguu yote miwili na wote wamelazwa Hospitali ya West Meru.
 
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu, juzi aliwatambelea majeruhi watano waliokuwa wamelazwa katika hospitali inayomilikiwa na kanisa hilo ya Shirika la Mapadre wa Roho Mtakatifu iliyopo Usa River.
 
Alihoji kwa nini waumini wake wanapigwa kwa mabomu.
“Ninashangaa kutokea tukio hili likiwa limekuja huku bado hatujasahau tukio lingine kubwa lililotokea katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Mei 5, mwaka huu,” alisema.
 
Alihoji waumini hao walikuwa na kosa gani hadi kupigwa bomu na kujeruhiwa na akashangaa ukimya wa  polisi kulitolea maelezo tukio hilo.
 
Pia alishangaa kwanini taarifa hizo zilikuwa hazijatangazwa tangu tukio hilo lilipotokea na akataka waliohusika wachukuliwe hatua na kuwajibishwa.
 
Mganga Msaidizi wa hospitali ya kanisa hilo, Dk. Frederick Mathew, alikubali kuwapokea majeruhi watano wa mlipuko huo wa bomu na akasema hali yao inaendelea vizuri.
 
Pamoja na hao majeruhi aliowataka Kamanda Sabas, majeruhi wengine ni Alphonce Nyigo (19), Philip Ambrose (22), Theresia Lesitare (33).
 
NIPASHE Jumamosi ilipotembelea jana hospitalini hapo ilielezwa na Mganga Msimamizi, Sista Anna Kipendi, kuwa majeruhi wengine wameruhusiwa isipokuwa Mary Melkioni Kwayu,  Anneth Baltazar Makoi na Theresia Lesitare (33).
 
Alisema Aneth Baltazar alihamishwa hospitalini hapo kutoka hospitali ya wilaya ya Arumeru kwa matibabu zaidi.
 
Akizungumzia zaidi tukio hilo, Kamanda Sabas alisema majira ya 6:10 usiku ambao ni siku ya Januari mosi, eneo la Ngarasero baadhi ya wananchi wa eneo hilo ambao hawakutaka kutii wito walianza kufanya fujo kwa kuchoma matairi barabarani, kuharibu mali za watu pamoja na kupiga mawe magari yaliyokuwa yanapita barabarani.
 
Alisema askari waliokuwa doria eneo hilo waliendelea kuzima moto na kuwadhibiti watu hao ambao walikuwa wanafanya fujo lakini waliendelea kuwashambulia kwa kuwarushia mawe askari waliokuwa wakizima moto na kusababisha kuwajeruhi askari watatu.
 
Aliwataja maaskari hao kuwa ni mkaguzi msaidizi wa polisi Athumani ambaye alijeruhiwa mguu wa kulia, askari G. 3475 Ramadhan aliyejeruhiwa kichwani na shavu la kushoto huku mgambo mwenye namba 97658 Jacob alipata majeraha katika shavu la kulia chini ya jicho.
 
Alisema pamoja na idadi ya askari kuongezeka eneo hilo kwa nia ya kudhidibiti vurugu, bado wananchi hao waliendelea kurusha mawe ndipo amri ya kutumia mabomu ya moshi ilipotolewa kwa madhumuni ya kuwatawanya.
 
Alisema askari waliojeruhiwa walitibiwa katika hospitali ya West Meru na kuruhusiwa na kwamba watu wanne wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo.
 
Aliwataja watu hao kuwa ni Seleman Hamis (24), mkazi wa Majengo Usa River, Patrick Richard (21), Jabu Yasini (25) na Hamisi Juma wote wakazi wa Kisambare na walitarajiwa kufikishwa mahakamani jana.

CHANZO: NIPASHE

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini