Ushawishi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeipasua Jumuiya ya Vijana ya chama hicho (UVCCM).
Mmoja wa viongozi wake ametoa taarifa iliyojaa maneno makali
akimshambulia Lowassa na baadhi ya viongozi wa dini akiwahusisha na
kampeni za uchaguzi wa urais mwakani.
Bila kutaja jina la kiongozi yeyote wa dini, ila tu kurejea kwa ujumla
wao kama maaskofu na masheikh, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa
UVCCM, Paul Makonda, aliwataka kwenda kwa Lowassa kama wanataka fedha za
haraka. Hakusema ni fedha za nini.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana, Makonda alisema hawawezi kukaa kimya wakati viongozi wa CCM
wakishambuliwa na watu aliosema hawana mapenzi mema na chama chao.
Alisema wapo watu aliodai wanafadhiliwa na Lowassa ili kuwashambuliwa
viongozi wa sekretariati ya CCM, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kwa kuwa anautaka urais
mwakani.
Aliwataja makada wa CCM aliodai wanaosukumwa na Lowassa kuwa ni
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai na Mwenyekiti mstaafu
wa CCM Dar es Salaam, John Guninita.
Makonda aliwatuhumu makada hao kuwa ni wahaini, waongo na wazandiki, na
kueleza kuwa kama nia yao ni kusaka urais kwa ajili ya Lowassa, basi
wajue kuwa amekosa sifa za kuteuliwa na chama hicho kuwania wadhifa huo
katika uchaguzi mkuu wa mwakani.
Hata hivyo, muda mfupi tu baada ya kauli ya Makonda, Makamu Mwenyekiti
wa UVCCM, Mboni Mhita, alisema kauli hiyo siyo msimamo wa UVCCM.
Msindai alikaririwa hivi karibuni akielezea msimamo wa kumuunga mkono
Lowassa katika masuala ya maendeleo, wakati Guninita alimkosoa Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kutokana na kauli zake za kuwaita
baadhi ya mawazi ‘mizigo’ kwa kuwa wameshindwa kutekeleza ilani ya CCM
ya mwaka 2010-2015.
Pia alimlaumu Nape kwa kukosoa uteuzi mpya wa baraza la mawaziri uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete Januari 19, mwaka huu.
Guninita alimkosoa Nape akisema kuhoji uteuzi huo ni sawa na kuingilia mamlaka ya Rais katika kutimiza wajibu wake kwa kikatiba.
Katika mkutano na waandishi wa habari jana Makonda alisema: “Tutaendelea
kuwajibu akina Msindai (Mgana) ama Guninita (John), lakini kuna mtu
anayewatuma kutoa kauli hizo, na huyu ni Edward Lowassa.”
NIPASHE iliwasiliana na Lowassa kwa njia ya simu jana, lakini ikapokewa
na mtu aliyeagiza suala hilo aulizwe mmoja wa wasaidizi wake wa masuala
ya vyombo vya habari.
Msaidizi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema Lowassa hawezi kuzungumzia madai ya Makonda.
Makonda alisema UVCCM imemuandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara,
Philip Mangula, kuhusu vitendo vya Lowassa kuwatumia viongozi na makada
wa chama hicho kutoa kauli zenye mwelekeo wa kumchonganisha Rais Kikwete
na sekretarieti ya chama hicho.
Alisema barua hiyo (hakuionyesha) ililenga kumuomba Mangula, asaidie ili kanuni za chama hicho zitumike kumdhibiti Lowassa.
NIPASHE ilimtafuta Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Hamisi Juma, kuzungumzia
kauli ya Makonda kama ndiyo msimamo wa jumuiya hiyo, lakini simu yake
haikujibiwa wala ujumbe mfupi wa maneno (sms) hadi tunakwenda mitamboni
jana
Akifafanua kauli hiyo Mhita alisema ni ya Makonda kama mkuu wa kitengo cha uhamasishaji.
“Kama utafika wakati ikahitajika kuzungumzia jambo lolote la kitaifa,
basi mzungumzaji mkuu ni Mwenyekiti wa UVCCM au Makamu Mwenyekiti,”
alisema Mhita pasipo kufafanua zaidi.
NIPASHE ilipowasiliana na Msindai na Mangula, simu zao ziliita bila kupokelewa wakati ile ya Guninita haikupatikana.
Awali, Makonda alisema ziara ya Kinana na Nape (iliyowaibua mawaziri
mizigo) ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa kanuni, misingi na katiba ya
CCM, vinavyotoa jukumu kwa chama hicho kuwa kiungo kati ya serikali na
wananchi.
Alisema CCM ni chama kinachoiunganisha serikali na wananchi, na kwamba
ziara ya Kinana iliyokuwa na wajumbe kadhaa akiwamo Nape, ilifanikisha
kuibua kero kadhaa zilizopo kwenye jamii.
Makonda alisema kupitia ziara hiyo, ujumbe wa Kinana ulibaini kuwapo
kero zilizowasilishwa serikalini kwa nia ya kupatiwa ufumbuzi, hivyo
inashangaza kuibuka kwa baadhi ya wana-CCM wanaoikejeli.
Kwa mujibu wa Makonda, ziara kama iliyofanywa na Kinana, haijawahi
kufanywa na kiongozi yeyote wa ngazi hiyo kwa miaka ya karibuni, na
kusema wanaoipinga hawana nia njema na wananchi wanaokabiliwa na kero
mbalimbali za kijamii.
“Chama hiki ni cha wanyonge, maskini wa taifa hili, haiwezekani matajiri
watake kukihodhi na waratibu mikakati ya kukihujumu kwa fedha, hali
sisi vijana tukitazama, tunasema tutakilinda na tutawalinda viongozi
wetu waadilifu,” alisema.
Makonda alisema viongozi wanaobezwa (Kinana na Nape) wamechangia
kurudisha imani ya wananchi kwa CCM, akitoa mfano wa kukutana na
`kuzichukua’ kero za wafugaji, walimu, wakulima wa pamba, korosho na
wananchi wa kawaida.
UVCCM RORYA YAMVAA MAKONDA
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Rorya, Sango
Kasera, amemtaka Katibu Mkuu wa Umoja huo, Sixtus Mapunda, kueleza kama
tamko lililtolewa na Makonda ni la kamati ya utekelezaji au ni lake
binafsi.
Pamoja na kumtaka Mapunda kueleza hilo, pia amemtaka Makonda kufanya
kazi za kufufua chipukizi na kueleza kazi walizofanya kama UVCCM hadi
sasa, kwani tangu ateuliwe amekuwa akiishia tu kutoa matamko, ambayo
hayana tija kwa vijana wa Kitanzania.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment